Wabantu kuichukulia salamu kuwa ni habari kamili. Kule Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, usishangae kuulizwa kuku na bata “waghonile”? Mambo yalikuwa analogia kwelikweli; unaandika barua ya karatasi mbili, robo ya barua nzima ikiwa ni salamu: “Mara baada ya salamu natumaini hujambo na unaendelea vyema kusukuma gurudumu la maendeleo.”

Siku hizi unabofya simu na kuanzika herufi mbili tu: “vp”. Jibu linakuja kwa herufi tatu: “poa”. Hayo ndiyo mambo ya digitali. Ni kama Wamisri vile; kipa anarusha mpira kwa beki mbili, anayepiga ndefu kwa winga namba saba. Saba anakunja ya juu kwa namba tisa, kinapigwa kichwa na watu wanarudi wakishangilia.

Ah, Nishakumbuka gemu ya Simba na Pan Africa pale Uwanja wa Taifa. Siku hiyo nilijua nini maana ya uzalendo michezoni. Ngoma ilipigwa hadi nyasi zilibadilika rangi. Ukiutazama uwanja kutoka jukwaani unauona wazi ukifuka moshi. Pan wakapigwa bao la kwanza. Walikuwa na kawaida ya kumuuliza Peter Tino kila wanapofungwa. Akikubali basi wanapeleka mpira kati; akikataa basi mpira utaishia hapo kwa mateke na magumi. Tino alilikubali goli, mpira ukapelekwa kati.
Watoto walicheza mpira kwa nguvu zaidi. Tino aliwapa moyo kuwa analo bao mguuni kwake, na kweli kufuatia kazi nzuri ya Hussein Ngulungu, Gordian Mapango na yeye mwenyewe wakarudisha bao. Ikawa chereko zisizo kifani maana kwenye gemu hiyo Pan walihitaji sare tu ili waende sawa.

Huku nako akina Adam Sabu na Jumanne Hassan (Masimenti) waliliandama lango la Pan kama nyuki. Nadhani siku hiyo kipa wa Pan alilazimika kukanda mikono baada ya mechi. Alimiminiwa makombora hadi alijiuliza kama hawa washambulizi wa Simba walikuwa na nia njema kwake.

Dakika ziliyoyoma na kutishia mpambano huo kuishia katika suluhu. Simba wakaona hapana, imma fa imma (kwa udi na uvumba) lazima ushindi upatikane. Iwe kwa heri au shari; hata ikibidi mbinu za kigaidi zitumike. Wakafosi hadi wakapata kona.

Hilo lilikuwa ni jambo la hatari sana kwa kipa Juma Pondamali. Yeye na Sabu walicheza katika timu hasimu za mchangani, pale Kariakoo. Kama sikosei moja iliitwa Kunkoma Nyani. Ni zile gemu zilizochezeshwa na waamuzi watata kama marehemu King Sabata. Ukimtoa ghafla Sabu kumsachi hutakosa kumkuta na bisibisi kiunoni. Kadhalika Pondamali, kwa hiyo walitambuana vyema.

Basi Mohammed Kajole aliyekuwa mtaalamu wa kupiga kona akaufuata mpira. Hali ilizidi kuwa ngumu kwa Pondamali, maana Kajole alikuwa na uwezo wa kupiga kona ikaingia wavuni bila kuguswa. Hivyo aliwapanga walinzi wake katika nafasi zao, akaweka umakini zaidi kwenye mpira utakaopigwa.

Kona ikapigwa. Kufumba na kufumbua Sabu alikwishafika kwa kipa, akamkanyaga miguuni ili asiweze kuruka. Ponda alimpigia kelele mwamuzi kutoka Lindi (namkumbuka kwa jina moja tu la Msosi), lakini haikusaidia. Mpira ulikwenda kugonga besela la juu, ukarudi. Masimenti akapiga kichwa cha juu, maana ilikuwa siyo rahisi pale langoni. Walitanda akina Jella Mtangwa, Leodegar Chilla Tenga, Jaffari Abdulrahmani na Mohammed Mkweche.
Ngoma ilikwenda kugonga besela kwa mara ya pili. Wakati wote huo Ponda hakuweza kujinasua kutoka kwa Sabu. Mpira uliporejea ukamkuta Mtemi Ramadhani. Hakuwa kwenye nafasi nzuri ya kufunga, hivyo akausindikiza mpira kwa mkono. Mwamuzi akasema “ni bao, weka kati”.

Pondamali alivurugwa kwelikweli. Akamfuata refarii, lakini akarudishwa kwa kadi ya njano. Wenzake walimzunguka kumtuliza, Peter Tino akimhakikishia kusawazisha bao hilo la pili. Ngoma ilikuwa Simba mbili, sisi (oh sorry) Pan moja. Mpaka hapo dakika zilizosalia zilikuwa pungufu ya chache.

Afanaleik! Peter Tino alisawazisha bao kwa shuti la mbali. Pondamali alimkimbilia tena mwamuzi kumtambia “kiko wapi!” Lakini refa alipomwona, akaingiza mkono kwenye mfuko wa ghorofani. Pondamali alipiga hesabu za haraka: “Ule mkono utatoka na kadi. Kwa vile nilishapigwa ya njano, itakayotoka itakuwa nyekundu.”
Basi kama kifutu, alimrukia mwamuzi na kumchota “mtama”. Kwa msioelewa alimpiga ngwala ya kisasa (kwa wakati ule). Acha nimalizie kwa kusema mpira uliishia hapo, ukapokelewa na mchezo wa mchanganyiko wa ndondi, mieleka, judo, karate na mingine ya aina hiyo. Tofauti ni kwamba michezo hiyo ilichezwa kwa uhalisia wake.

Uzalendo uwe imma fa imma (iwe isiwe). Mara nyingi tumekuwa tukiwalalamikia Wamisri kwa michezo wanayotuchezea, bila kuzingatia kuwa wanafanya uzalendo kwa Taifa lao. Mara moja walitufanyia fujo katika uwanja wao, wakatufunga kwa uonevu mkuu. Hatukuwa na la kufanya, tukarudi tukisema “watatukoma kwetu.”

Walipokuja wakapeperusha bendera za Tanzania tangu Uwanja wa Ndege, wakazunguka na bendera zetu uwanja mzima. Tukasahau maovu yao yote, wakacheza kwa amani na kutoa sare. Wao wakaendelea, sisi tukatolewa. Unaona uzalendo?

src
mwnanchi

0 comments:

Post a Comment

 
Top