Uongozi mpya wa shirikisho la soka katika nchi hii (TFF), ulipoingia madarakani, wadau wengi wa soka waliamini wamepata wakombozi wa soka la taifa hili. Hakika hili halipingiki, isipokuwa kwangu ambaye hunichukua muda mrefu kumkubali mtu au watu kwa jambo lolote zaidi ya kujikubali mimi mwenyewe. 
Tabia hii ya kushuku au kuwa na dukuduku katika mambo mbalimbali, hunifanya pengine nikose kufahamu mambo mengi au kujua mambo mengi pasi mwenyewe kufahamu. Hakika sikuwa mwepesi wa kuwahunga mkono viongozi wa TFF walipoingia madarakani, na dukuduku hizi zilijenga ngome katika kichwa changu hasa baada ya uteuzi kwa baadhi ya wajumbe wa kamati za shirikisho hilo. 
Uteuzi huo ulinifanya nianze kupoteza imani kila siku kwa utawala wa TFF. Lakini hilo sio jambo kubwa kwangu linalousumbua ubongo wangu juu ya kuhimarisha soka letu; bali yapo mengi na mambo makuu matatu nionayo mimi yamechafua utukufu ambao TFF ilikuwa nao muda mfupi baada ya kuingia madarakani.

Waswahili, hasa wanabusara wa kale hawakusita kutoa misemo, nahau, methali na hata mazungumzo au nasaha zenye kufunza kwa ndani yake. Kwa kukurupuka, maneno hayo ni vigumu kuyang’amua. Miongoni mwayo ni: mbio za sakafuni huishia ukingoni, si kila king’aacho ni dhahabu, ngoma ikivuma mwishowe hupasuka msamba; mtaka nyingi nasaba hupata mwingi msiba na hakuna kapa isiyokuwa na usubi. Metahli na misemo hii ya Kiswahili ina maana kubwa katika maisha ya binadamu na huaksi maisha au matendo katika maisha yetu. 
Hakika misemo hii inagusa na kuaksi baadhi ya utendaji katika shirikisho la soka hapa nchini. TFF ni baba wa soka mwenye madaraka ya kuendesha soka la nchi hii na kuliboresha ikishirikiana na wadau wa soka pia. Lakini kwa mambo haya yafuatayo inabidi uongozi wa TFF ujitazame upya.

Kwanza, kuna sakata la timu za Kanembwa FC na Stand United, ambapo katika mchezo wao wa kutafuta tiketi ya kufuzu kucheza ligi kuu msimu ujao, kulitokea taflani amabayo ilisababisha mchezo huo kutomalizika kwa muda sahihi. Sakata hilo lilipelekwa TFF, ambapo ilibainika kuwa zilivuka vurugu zilizopelekea mchezo huo kukatika, na ikabainika baadhi ya wachezaji walishiriki kusababisha vurugu na hata kumpiga mwamuzi. Jambo la kushangaza wakosaji hao walipata adhabu ya kuchekesha ambayo kimsingi kwangu mimi naita adhabu ya kuchochea vitendo kama hivyo viendelee kuwepo; kwani, adhabu ya kumpiga mwamuzi ilikuwa ni kila mchezaji aliyetenda dhambi hiyo ni kuhukumiwa kufungiwa ichezo 3. 
Hii ni adhabu ya kushangaza na kujiuliza, hii ndio TFF ambayo inategemewa kuliokoa soka letu? Lakini baada ya hapo iliagizwa mechi irudiwe na tahadhari ikatolewa kuwa hakuna kuchezesha wachezaji ambao walisajiliwa na timu hizo katika dirisha dogo la usajili. Timu moja wapo yaani Kanembwa ikachezesha wachezaji hao na Shinyanga United wakakata rufaa, rufaa ambayo ilisubiria ligi daraja la kwanza iishe na maamuzi yatolewe. Bado najiuliza huu ndio utawala bora uliotegemewa kuzindua soka letu?
   

Vilevile, kuna suala la kumtimua aliyekuwa kocha wa timu ya taifa, “Taifa Stars”, yaan, King Paulsen. Rais wa TFF alitamka kwenye vyombo vya habari, kuwa walifikia mwafaka wa kusitisha mkataba kati ya shirikishao na kocha, wa kuifundisha timu ya taifa. Rais alisema kuwa wamemuachisha kazi Paulsen baada ya kuona mwenendo wa timu ya taifa hauridhishi ukulinganisha na siku za nyuma, huku shahuku kubwa ikitoka kwa wadau wa mpira wa miguu, vyombo vya habari na baadhi ya watu ambao walijitolea kulipa gharama za fidia za kuukatisha mkataba wa kocha. Hili ni jambo ambalo kwa macho ya kwaida, wengi wataliunga mkono, ila wachache kama mimi si rahisi kulikubali. Hivi, uongozi ulio makini na unachokifanya, utamfukuzaje kocha kwa shinikizo la wadau wa mpira ati kisa hawaridhishwi na kiwango cha timu? Au inaingiaje akilini kumfukuza kocha kwa maoni ya waandishi wa habari, tena mbaya zaidi ni wale ambao huandika habari za soka kihisia na si kiualisia? Watu wasiojua soka linakwenda au kuendeshwaje bali wao huishia kutazama mpira unachezwa ama wazi au runingani, lakini ukiwauliza waeleze inakuwaje mchezo ukawa ulivyokuwa hawajui chochote; waandishi ambao wao hulinganisha mafanikio ya timu za ulaya na za Tanzania pasi kujua ni kwa nini timu za ulaya zianafanikiwa. Kocha anafukuzwa ati kwa kuwa kuna watu wana pesa zao wamejitolea kulipa fidia ya kukatisha mkataba, akiwemo kiongozi mwenyewe. Hii inanifanya nishuku kama hakuna watu ambao wanaimiliki TFF! Hivi kweli Tanzania tumefikia hatua ya kumtimua kocha kwa kisingizio ameshindwa kuipa mafanikio timu ya taifa? Kwa kigezo kipi hasa? Kwa aina ipi ya ligi tuliyonayo? Kwa mfumo upi wa soka na kupata wasakata kabumbu maridadi ambao akikabidhiwa kocha akishindwa atimuliwe? Haya ni baadhi ya maswali juu ya uongozi wa lulu wa TFF.
    

Mnamo tarehe 19, mwezi wa 3; afisa habari wa TFF, alitangaza TFF kuitaka Yanga ilipe fidia ya milioni 25 kwa uharibifu ulifanyika uwanjani kwa kuvunja viti kati ya mechi ya vilabu bingwa afrika, Yanga na Al Ahly ya Misri. Mashabiki wa walifanya vurugu na kung’oa viti uwanjani. Ila mshangao ulikuwa ni kutaka kilabu cha Simba nacho kihusike kulipa fidia ya milioni 5 ati kwa hoja ya kuwa uchunguzi umegundua baadhi ya mashabiki wa Simba walihusika katika uharibifu huo. Ni kweli, kwa mazoea kukubali faini hiyo kwa kilabu cha Simba ila kiulweli si sahihi. Kwanini si sahihi?

Kilabu hufungiwa au huadhibiwa kulipa fidia kwa uharibifu uwanjani pale ambapo mashabiki wake wamehusika kuharibu uwanjani huku timu yao ikiwa inahusika katika mechi hiyo. Simba hakika hawakuhusika katika mechi hiyo, kwani yanga ndio waliokuwa wanahusika na mashabiki walioingia uwanjani, walikuwa mashabiki watanzania wa Yanga na Al Ahly. Inawezekana mashabiki wa Simba walihusika kuharibu uwanja ila Simba kama kilabu hakihusiki kabisa na uharibifu huo, wanaohusika ni mashabiki ambao wanasemekana ni wa Simba. Wataalamu wa elimu ya mantiki, hata wataalamu wa sheria pia huhusika katika kuitumia elimu ya mantiki kuamua kesi mbalimbali. Mlolongo wa kuunda hoja yenye mashiko huwa na hatua muhimu tatu, yaani misingi wa hoja (nguzo msingi na nguzo shiriki) hutangulia na huwa na mtiririko usiokanganyika; hatimaye, huleta hitimisho lenye kuleta mantiki ya hoja. Kanuni hii iko hivi:



Hoja:

- Nguzo msingi,

- Nguzo shiriki,

- Hitimisho.

Hapa, katika kutengeneza hoja yenye mantiki, nguzo msingi ya hoja utangulia, hufuatiwa na nguzo shiriki ambayo ina uhusiano na nguzo msingi; baada ya hapo hitimisho hutengenezwa kutokana na uhusiano wa nguzo hizo hasa mzazi wa hitimisho ni nguzo msingi. Hebu tuone hapa;

Nguzo msingi - Adhabu hutolewa kwa timu inayohusika na mchezo pale mashabiki wake wanapohusika katika uharibifu wowote au fujo. Hii ni kwa kuwa tendo hilo linahusika moja kwa moja na timu hiyo, kwa maana kuwa bila timu hiyo kucheza mashabiki hao hawawezi kuangalia mchezo kwa lengo la timu yao. Wanapofanya hivyo si kwa egemeo la timu yao bali ni kwa kuwa wanapenda soka.

Nguzo shiriki - Timu imecheza, mashabiki wake wakaja kuangali mchezo na wakafanya uharibifu ama vurugu.

Hitimisho - Hivyo basi, timu hiyo inaadhibiwa kwa utovu wa nidhamu wa mashabiki wake.

Hoja hii ina mantiki, kwani taratibu zimefuatwa katika kuunda hoja na hivyo ina mashiko. Tuangalie maelezo yafuatayo, kama hoja zake zina mantiki na mashiko?

Yanga wamecheza mechi ya vilabu bingwa afrika, na timu kutoka Misri. Mashabiki wanaohusika ni watanzania amabo watakuwa wakiishangilia timu yao muwakilishai, yaani yanga. Na wale wa pili watakuwa ni wa timu ya Misri.

1. Hoja:

Nguzo msingi – mechi imechezwa kati ya Yanga na Al Ahly, mashabiki wa mchezo huo walifanya vurugu na fujo kwa kuvunja viti vya uwanjani.

Nguzo shiriki – mashabiki walioangalia mechi walikuwa wa Yanga na Al Ahly na ndio waliofanya fujo na kuvunja viti uwanjani.

Hitimisho - adhabu imetolewa kwa vilabu amabvyo mashabiki wake walishiriki kuvunja viti uwanjnani wakati wa mechi baina ya timu zao. Hivyo, Yanga na Al Ahly ndio wanaohusika kutoa faini kwa fidia ya uharibifu wa mashabiki wao.

2. Hoja :

Nguzo msingi - mechi imechezwa kati ya Yanga na Al Ahly, mashabiki wa mchezo huo walifanya vurugu na fujo kwa kuvunja viti vya uwanjani.

Nguzo shiriki - mashabiki walioangalia mechi walikuwa wa Yanga na Al Ahly na ndio waliofanya fujo na kuvunja viti uwanjani.

Hitimisho – Yanga na Simba wanaadhibiwa kwa mashabiki wao kugundulika wamefanya uharibifu uwanjani kwa kung’oa na kuvunja viti uwanjani. Hivyo Yanga na Simba ndio wanaohusika kutoa faini kwa fidia ya uharibifu wa mashabiki wao.

Kwa hiyo tukiangalia katika maelezo ya kifungu cha pili kuna hoja ya kwanza ambayo kimsingi inamatiki na ni ya mashiko kwani hitimisho limetokana na uhusiano wa nguzo msingi. Lakini hoja ya pili haina mantiki ndani yake na si ya mashiko kwani hitimisho lake limezaa mhusika ambaye hakuwemo katika mkururo wa matukio hayo. Kwa maana hiyo, TFF inabidi washukiwe kwa kutoa maamuzi ambayo hayana msingi wowote. Si kwamba mashabiki wa Simba hawakufanya vurugu, la hasha! Yawezekana uchunguzi uliofanywa na TFF ni sahihi, lakini Simba kama kilabu haihusiki kabisa na dhambi hiyo, kwani, mchezo haukuwa wao. Jambo ambalo lilibidi lifanyike ni kuwaaadhibu hao mashabiki kwa nafsi zao kwa kufanya uharibifu huo na wala sio Simba. Kama TFF waliweza kubaini kuwa ni mashabiki wa Simba basi bila shaka wanao uwezo wa kuwaadhibu pia na wala sio kukivisha mzigo usikihusu kilabu cha Simba.

Hakika TFF ni taasisi kubwa wanahitaji kutafuta wataalamu wa mambo mbalimbali ili aweze kushirikiana hasa katika kuboresha soka la nchi hii, na wala sio kukurupuka na kufanya maamuzi pasipo kufuata utaratibu. Bado mashaka ni makubwa kuamini kuwa TFF hii itatofautiana na watangulizi wao. Yote haya ni kutaka kuerkebisha soka letu na wala si vinginevyo. KWA PAMOJA TUTALIINUA SOKA LETU.

Mpenzi wa soka: MUSHUMBWA ALCHERAUS
 
src
shaffihdauda

0 comments:

Post a Comment

 
Top