Uzoefu wetu wa muda mrefu umetuonyesha pasipo shaka
kwamba mambo mengi yanayotendeka Tanzania hayawezi kutendeka katika nchi
nyingine.
Tanzania imekuwa taifa la ajabu na masikitiko yetu ni
kwamba mporomoko wa maadili katika jamii yetu umeziba mitima na dhamira za
viongozi wetu na jamii nzima kwa jumla kiasi cha kuyaona matendo hayo kama
mambo ya kawaida.
Tunayo mifano ya matukio lukuki ya ajabu na ya
kushtusha yaliyowahi kutokea hapa nchini lakini yakaonekana kama ya kawaida.
Fikiria wafanyabiashara walioiba mabilioni ya fedha za
Epa ambao muda mfupi kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2005 walikwenda Benki Kuu ya
Tanzania (BoT) wakati wa siku za mapumziko na kukwapua mabilioni hayo kwa njia
za udanganyifu. Fikiria wezi hao walivyoahidiwa kwamba iwapo wangezirudisha
wasingechukuliwa hatua yoyote.
Ebu fikiria nchi ambayo kiongozi wake anakwenda
ughaibuni na kutangaza kuwapo kwa majangili mapapa 40 na kusema kiongozi wao
yuko mikoa ya Kaskazini, badala ya kusema hayo akiwa nchini, ikiwa ni pamoja na
kuyakamata majangili hayo na kuyachukulia hatua.
Ebu fikiria matukio haya mawili ambapo Waziri Mkuu
anatamka bungeni kwamba ni sawa tu kwa Jeshi la Polisi kuwapiga wananchi
‘wakorofi’, huku mkuu wa nchi akikiagiza chama chake cha siasa ambacho yeye ni
mwenyekiti kuwapiga wapinzani anaodai wanafanya vurugu dhidi ya wafuasi wa
chama chake. Ni nchi gani ambayo viongozi wake wakuu wanaweza kutoa amri hizo
za hatari?
Tumesema yote hayo kutokana na kitendo cha ajabu na
aibu kilichofanywa na Mwenyekiti wa Chama cha National League for Democracy
(NLD), Dk Emannuel Makaidi cha kufanya ulaghai na kujiwezesha yeye na mkewe
kuteuliwa kuingia katika Bunge la Katiba.
Katika utetezi wake, ametoa hoja za kuchefua na
kughadhabisha kuwa, kwa vile mke wake naye ni mwanachama wa chama hicho alikuwa
na haki ya kuteuliwa kama ilivyo kwa Rais Kikwete na mke wake ambao wote ni
wajumbe wa Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM.
Tunasema uteuzi huo haukubaliki hata kidogo kutokana
na kukiuka taratibu zilizowekwa kisheria kwamba vyama vya siasa lazima viwe na
sura ya Muungano katika mfumo na uendeshaji wake.
Ni ujasiri na uthubutu wa kiwango cha juu kujiteua
yeye na mkewe kama vile NLD ni mali ya kifamilia , Kudai kwamba aliteua majina ya wanachama wanne na Rais akamchagua yeye na
mkewe ni uongo wa kupitiliza.
Hii inaonyesha kwamba zilikuwapo mbinu chafu katika
mchakato wa uteuzi huo, vinginevyo wanachama wa Zanzibar wangenyimwa vipi
uwakilishi? Hatua ya chama hicho upande wa Zanzibar ya kumtaka Rais Kikwete
atengue uteuzi wa Dk Makaidi na mkewe lazima iungwe mkono.
Tatizo hapa ni hatua ya Serikali kuendelea kuvibeba kwa sababu za kisiasa
vyama vya siasa vilivyokufa siku nyingi. Ukweli ni kwamba NLD na vyama vingine
vingi ambavyo kwa mujibu wa sheria ya vyama ya 1992 vinapaswa kufutiwa usajili
wa kudumu bado vinatambuliwa kiasi cha viongozi wake kuingizwa katika Bunge
Maalumu la Katiba bila kuwa na sifa stahiki., Hivyo, wananchi wawe tayari
kushuhudia vitimbi vya viongozi wa vyama hivyo ndani ya Bunge. Ndiyo maana
tunasema mambo mengi yanayofanyika Tanzania hayawezi kufanyika katika nchi
nyingine
Src
mwananchi
0 comments:
Post a Comment