Dunia na wapenzi wa soka
kiujumla wamepata fursa ya kuona na kushuhudia vipaji na ufundi mbalimbali
unaoonyeshwa au uliowahi kuonyeshwa na wanasoka mbalimbali ulimwenguni kiasi
ambacho baadhi ya majina ya wanasoka ambao wameamua kutundika daruga la kusakata
mchezo huo wa kabumbu ulimwenguni yakiendelea kukaa vichwani na kutajwa midomoni
mwa wapenzi na mashabiki wa soka ulimwenguni.
Miongoni mwa wachezaji ambao
licha ya kuamua kupumzika na mikikimikiki ya mchezo wa soka bado wamebakia
kuwepo katika ubongo wa wapenzi wa soka ulimwenguni ni kiungo fundi wa
ushambuliaji wa vilabu vya Barcelona na PSV Eindhoven, Phillip John William Cocu
ambaye dunia ilimtambua kwa kifupi cha jina lake Phillip Cocu.
KIPAJI TOKA
EINDHOVEN
Phillip Cocu alizaliwa mnamo
tarehe 29,Oktoba 1970 katika kitongoji cha Zevenaar kilichopo katika jii lenye
wanazi sugu wa soka la Eindhoven. Ikumbukwe kwamba jiji la Eindhoven ndipo
inapotoka timu iliyoweza kutikisa nchini Uholanzi na Ulaya kwa ujumla mwishoni
mwa miaka ya tisini na mwanzoni mwa miaka ya elfu mbili ya PSV
Eindhoven.
Kama ilivyo ada kwa watoto
wengi wanaozaliwa wakiwa na vipaji vya soka, Cocu alijiunga na timu ya watoto ya
mtaani kwao ya DCS kabla ya baadae kujiunga na timu nyingine
iliyopo katika mtaa huo ya De Graafschap ambayo aliichezea mpaka mwaka 1988
ambapo alijiunga rasmi na soka la kulipwa katika timu ya AZ Alkmaar ambayo
aliichezea kwa muda wa miaka miwili tu ambapo baadaye alijiunga na klabu ya
Vitesse .
Akiwa Vitesse, Cocu alipata
majeruhi mwanzoni tu mara baada ya kujiunga na klabu hiyo jambo lililopelekea
kutishia kipaji chake lakini alifanikiwa kupigana na majeruhi hayo ya goti
ambayo na kurudi uwanjani kwa kishindo na kupata nafasi ya kudumu katika kikosi
cha kwanza cha timu hiyo.
AJIUNGA NA
KLABU YA NDOTO ZAKE
Baada ya kuichezea timu ya
Vitesse kwa muda wa miaka mitano katika michezo 137 na kufanikiwa kuifungia timu
hiyo jumla ya magoli 25, Cocu alisajiliwa rasmi na klabu maarufu ya PSV
Eindhoven ambayo inatoka katika jiji alilozaliwa la Eindhoven mnamo mwaka
1995.
Cocu aliuelezea uhamisho huo
kuwa ni ukamilisho wa ndoto zake za muda mrefu za utotoni huku akiishukuru klabu
ya Vitesse na mashabiki wake kwa kumsapoti katika matukio shida na furaha
aliyowahi kukutana nayo ikiwemo majeruhi ya muda mrefu aliyopata pindi
alipojiunga na timu hiyo huku wakimchukulia kama miongoni mwa mashujaa wao
klabuni hapo.
APIGA SOKA LA UHAKIKA
PSV, ATUA BARCELONA
Mara baada ya kujiunga na
klabu ya PSV Eindhoven, Cocu alifanikiwa kupata alifanikiwa kujitengenezea namba
ya kudumu katika timu hiyo akicheza katika nafasi ya kiungo mshambuliaji nafasi
ambayo alikuwa akiimudu vilivyo na kufanikiwa kutwaa mataji mawili maarufu
nchini humo ya KNVB na lile la ligi kuu nchini humo lijulikanalo kwa jina la
Eredivisie mnamo mwaka 1997.
Akiwa hapo, Cocu alifanikiwa
kucheza jumla ya mechi 95 huku akifanikiwa kuifungia timu hiyo jumla ya magoli
31 katika mechi hizo alizocheza.
Kutokana na uwezo wake
mkubwa wa kusakata kabumbu, vilabu mbalimbali barani Ulaya vilianza kuinyemelea
saini yake lakini ilikuwa ni klabu ya Bercelona iliyofanikiwa kuinasa saini yake
mnamo mwaka 1998.
ATESA BARCELONA , APEWA
UNAHODHA
Cocu katika misimu yote
aliyoichezea klabu hiyo ya Hispania inayotokea katika kitongoji cha Catalan,
alifanikiwa kuteka nyoyo za wapenzi na mashabiki wa timu hiyo kutokana na uwezo
wake mkubwa wa kucheza soka jambo ambalo lilipelekea Mdachi huyo kupewa unahodha
klabuni hapo, huku akifanikiwa kuisaidia timu hiyo kutwaa taji la nchi hiyo
maarufu kama La Liga, huku Barcelona ikifanikiwa kucheza katika nusu fainali
mbili za mashindano makubwa na maarufu ya vilabu barani Ulaya yajulikanayo kama
Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Pia akiwa Barcelona, Cocu
alifanikiwa kuweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza wa kigeni kuweza kuichezea
mechi nyingi timu ya Barcelona, ambapo aliichezea timu hiyo jumla ya mechi 205
huku akifunga jumla ya magoli 31
AAMUA KURUDI
NYUMBANI
Baada ya miaka
sita ya mafanikio ndani ya Barcelona, Phillip Cocu aliamua kurudi
katika klabu aliyoipenda ya PSV Eindhoven ambako aliweza kuisaidia timu hiyo
kushinda jumla ya mataji matatu ya ligi kuu nchini humo huku pia akiisaidia timu
hiyo kufika nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa barani Ulaya, huku ikiwa ni nusu
fainali yake ya tatu katika mashindano hayo.
Inasemekana, Cocu aliamua
kurudi zake nyumbani Uholanzi ikiwa ni kama njia ya kumpisha nyota wa Kihispania
aliyekua anachipikia klabuni hapo ambaye baadae ametokea kuwa staa na nahodha wa
tim hiyo, na huyu si mwingine bali ni Xavi Hernandez.
AMALIZIA SOKA
UARABUNI,ANG’ARA TIMU YA TAIFA
Mara baada ya awamu ya pili
ya mafanikio ndani ya klabu ya PSV,Cocu aliamua kutimkia zake Uarabuni ambako
alikwenda kumalizia soka lake katika klabu ya Al Jazira.
Kutokana na soka lake la
uhakika alilolionyesha katika timu mbalimbali, Cocu alifanikiwa kujiwekea nafasi
ya kudumu katika timu ya Taifa ya Uholanzi ambayo aliichezea jumla ya mechi 101
na kuifungia jumla ya magoli 10.
Miongoni mwa matukio ya
kusisimua ya Phillip Cocu akiwa na timu ya Taifa ya Uholanzi, ni kuifungia timu
hiyo magoli mawili katika Fainali za Kombe la Dunia zilizofanyika nchini
Ufaransa mwaka 1998 lakini baadae akaja kukosa penati muhimu dhidi ya Brazil
katika mchezo wa nusu fainali ambapo Uholanzi iliondolewa kwa mikwaju ya penati
na miamba hiyo ya soka ulimwenguni.
AGEUKIA
UKOCHA
Mara baada ya kuamua
kutundika daluga la kucheza soka, kama ilivyo kawaida ya wanasoka wengi
waliostaafu kucheza soka, Cocu aliamua kujikita katika ukocha wa mchezo huo
wenye mashabiki wengi ulimwenguni ambapo hivi sasa anainoa klabu anyoihusudu ya
PSV Eindhoven ambayo ameiwezesha kufika katika hatuanya mtoano ambayo walitolew
na timu ya AC Milan hivi karibuni, huku wakipata nafasi ya kushiriki katika
mashindano ya Europa League.
Imeandaliwa:
CHARLES
ABEL-SAUT
0713
923276
Email:
charlesabel46@yahoo.com
0 comments:
Post a Comment