Bomu lililotengenezwa kienyeji limelipuka majira ya saa 2 usiiku katika korido ya nyumba ya kulala wageni iliyopo katika eneo la Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT), Usharika wa Imani, jijini Mwanza na kumjeruhi vibaya mtumishi wa kanisa hilo.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Katibu wa KKKT Dayosisi ya Mashariki ya Ziwa Victoria, Rogart Mollel, alimtaja aliyejeruhiwa katika tukio hilo kuwa ni Bernadetha Alfred, 25, ambaye alikimbizwa katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando.

Mollel alisema lilifungwa katika kifurushi kilichopambwa na karatasi za zawadi na kuwekwa katika mfuko mweusi wa nailoni uliotelekezwa juu ya kreti za soda katika korido ya nyumba hiyo kwa takribani siku tatu.

Kwa mujibu wa Mollel, eneo hilo la korido huwekwa kreti za soda na wageni wamekuwa wakiingia na kutoka kutumia njia hiyo, na wakati mwingine hupata chakula na chai katika eneo hilo, ndio maana watumishi hawakuhisi kwa haraka kama ni kitu cha hatari.

“Jana usiku huo ndiyo mhudumu wetu akakichukua na kukiangalia na kufungua ili kuona ni nini... akidhani ni mzigo wa mtu umesahaulika... na ndipo lilipomlipukia na kumjeruhi vibaya sehemu mbalimbali za mwili, ikiwemo usoni na miguuni na kukimbizwa Bugando kwa uchunguzi na tiba,” amenukuliwa Mollel akiwaambia wanahabari.

Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa Makanisa ya Kikristo Mkoa wa Mwanza, Askofu Zenobius Isaya, alielezea kuwa Bernadetha alichukua kifurushi hicho juzi usiku kwa kuwa kilikuwa kimetelekezwa tangu Ijumaa iliyopita, nia ikiwa ni kufahamu ni la nani na kwa nini lipo kwenye korido hiyo kwa muda mrefu.

Alipoulizwa kuhusu ulinzi uliopo katika eneo hilo la Kanisa Kuu la KKKT, Mollel alisema ulinzi upo katika mageti yote mawili lakini upekuzi huwa haufanyiki kwa kina. 

“Kwa kweli tukio hili limetuchanganya sana. Tumekuwa tukisikia matukio hayo yakitokea maeneo mengine makanisani, kwetu limetokea kwenye nyumba ya kulala wageni, sina hakika waliofanya hivyo walilenga nini,” alisema na kuongeza; “...siwezi kusema kwamba chanzo cha mlipuko huo ni mambo ya kidini japo ulinzi wetu haukuwa mkali kiasi cha kudhibiti watu walioingia na vitu...” “ tunashukuru Mungu haijaleta madhara makubwa sana.”

Baadhi ya watu waliohojiwa walidai waliposikia mlipuko huo, walidhani ni transfoma ya Shirika la Umeme (TANESCO) kwa kuwa mara baada ya kulipuka, umeme ulikatika katika eneo hilo. Mlinzi aliyekuwa zamu siku ya tukio, Charles Mathayo, alidai baada ya mlipuko huo alisikia kilio cha mhudumu Bernadetha akiomba msaada, na walipofika walimkuta akiwa amelala chini akilia huku damu zikimtiririka huku kukiwa na misumari midogo midogo katika eneo hilo. Shuhuda ambaye kwa wakati huo alikuwa amekaa nje kwenye ngazi, Elina Emmanuel, alidai alisikia mlipuko mkubwa na kuona moshi huku waliokuwa vyumbani wakianza kutoka nje. 

Elina ambaye ni mwanafunzi wa chuo cha kompyuta alidai alikuwa kwenye nyumba hiyo na baada ya mlipuko huo wageni walihamishiwa kwenye nyumba nyingine ya kulala wageni.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Valentine Mlowola, alithibitisha kutokea kwa mlipuko huo saa 2.20 usiku na kusema uchunguzi wa awali unaonesha kuwa bomu hilo limetengenezwa kienyeji.

Alisema uchunguzi wa Jeshi la Polisi mkoani hapa unaendelea kubaini nani aliyefanya kitendo hicho na kwa sababu gani, ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yake ingawa mpaka jana hakukuwa na mtu aliyekuwa akishikiliwa kwa tuhuma hizo.

“Bado tunaendelea na uchunguzi wa tukio hilo ili tubaini ni nani kafanya ili kama ni mtu au kikundi kimehusika tuchukue hatua haraka. Natoa wito kwa wananchi kutochukua vitu ambavyo hawa uhakika navyo, wanapoona vitu vya aina hiyo, watoe taarifa kwetu.” Alisema Kamanda Mulowola.

Kamanda Mlowola ametoa wito kwa wananchi wanapoona vitu wasivyo na uhakika navyo na kuwa na wasiwasi navyo wasivishike, badala yake watoe taarifa Polisi.

Mganga Msaidizi wa Idara ya Dharura katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando, aliyejulikana kwa jina moja la Baraka alisema kwa sasa waandishi hawaruhusiwi kumuona, kuongea wala kumpiga picha majeruhi kutokana na hali yake kuwa mbaya na kwa wakati huo hakukuwa na ndugu yake hata mmoja.

Mlipuko huo uliozusha hofu kwa waumini mbalimbali wakiwemo wa Kanisa hilo, umetokea ikiwa ni wiki moja baada ya maadhimisho ya ‘Huduma ya Mtoto’ kwa makanisa mbalimbali ya Kikristo jijini Mwanza yaliyofanyika kwenye kanisa hilo, yakitanguliwa na maandamano kutoka uwanja wa Furahisha hadi KKKT.
 
 
src
Wavuti

0 comments:

Post a Comment

 
Top