Gari hili la chuo cha ualimu Tandala likiwa juu ya mawe (bovu) kwa zaidi ya miaka 10 sasa.
=======
Serikali imeombwa kutoa gari kwa chuo cha ualimu Tandala kilichopo wilayani Makete mkoani Njombe kufuatia chuo hicho kukosa gari kubwa lenye kutosheleza mahitaji kwa zaidi ya miaka 10 sasa
Akisoma risala ya wanafunzi katika mahafali ya 39 ya chuo hicho, msomaji wa chuo hicho Bw. Pius Peter amesema chuo hicho kilipewa lori ambalo lilikuwa likisaidia shughuli mbalimbali za chuo hicho, ila kwa sasa limeharibika na halifanyia kazi kwa zaidi ya miaka 10, licha ya chuo hicho kupatiwa gari lingine dogo ambalo linafanya kazi hadi sasa
Kukosekana kwa gari kubwa chuoni hapo kunasababisha ongezeko la gharama kwa shughuli mbalimbali za chuo ikiwemo kuwapeleka wanafunzi kwenda kufanya mazoezi pamoja na shughuli nyingine zinazohitaji usafiri huo
Aidha wamesema serikali iongeze haraka ya kuleta umeme kwenye chuo hicho, ambapo umeme huo tayari umefika chuoni hapo lakini haujaunganishwa bado jambo linalopelekea jenereta kuwashwa kwa saa 3 na kuzimwa kutokana na chuo kuzidiwa na gharama za kuendesha jenereta kwa zaidi ya muda huo
Bw. Pius Peter akimkabidhi mgeni rasmi risala.
Akizungumza katika mahafali hayo, mgeni rasmi katika mahafali hayo Bw. Uhuru Mwembe kwa niaba ya mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Makete, amewataka wanafunzi hao kuzingatia masomo na kufanya maandalizi mema ya mtihani wao wa mwisho unaoanza Jumatatu Mei 5 mwaka huu ili wote wafaulu
Amesema changamoto zote zilizoainishwa ikiwemo ya chuo kupatiwa gari jingine amesema serikali inalitambua hilo na lazima itatatua kero hiyo kulingana na hali ya uwezo wake wa kifedha, huku akisema uongozi wa chuo unatakiwa kubadilisha mfumo wa umeme wa jenereta ambao upo chuoni hapo na kuweka mfumo wa umeme wa tanesco, kwani kwa mujibu wa tanesco wameshauri mfumo huo usukwe upya
Mgeni rasmi Bw. Uhuru Mwembe akihutubia katika mahafali hayo.
Bw. Mwembe amesema ameambiwa kuwa chuo kina changamoto ya ukosefu wa fedha za kufanya kazi hiyo lakini suala hilo litatazamwa upya kuona ni nini kifanyike ili umeme uingie chuoni hapo kama serikali ilivyoagiza
Mkuu wa chuo Mwl. Clement Kabuye akizungumza katika mahafali hayo.
Awali akimkaribisha mgeni rasmi mkuu wa chuo Mwl. Clement Kabuje amesema wanafunzi hao wameonesha nidhamu na heshima ya hali ya juu wakati wote wakiwa chuoni hapo pamoja na kujenga mahusiano mazuri na vyuo vingine pamoja na jamii kwa ujumla
Wahitimu wakipatiwa vyeti katika mahafali hayo.
src
Eddy Blog
0 comments:
Post a Comment