KUNA taswira mbili kuu za kuitazama demokrasia ya Afrika kama ilivyo. Taswira ya kwanza ni kuiangalia demokrasia kama ukombozi wa binadamu wote bila kujali asili, rangi, dini, kabila, hali au tofauti nyingine zilizopo.
Ukombozi unaoanzia na msingi mkuu wa utu na usawa wa binadamu na imani kwamba kila binadamu, bila kujali alipo, anastahili heshima ya kutambuliwa na kuthaminiwa utu wake.
Taswira ya pili ni kuiangalia demokrasia inavyoendeshwa leo kama pandikizi la kuendeleza ukandamizaji wa watu wengine, hasa wanyonge. Ukandamizaji unaoruhusu wanasiasa wetu kutumia hila – kwa sababu ya ile asili niliyoijadili awali ya ubinafsi, tamaa na ukatili – kujitwalia madaraka na kujilimbikizia mali huku wakiwatumikia wamiliki vitu wakuu wa dunia waishio duniani.
Ukandamizaji unaohalalisha binadamu wengine waitwe “waheshimiwa” na wengine waitwe “wananchi wa kawaida”. Mantiki rahisi ni kuwa kama kuna ‘mheshimiwa’ basi yupo pia asiyeheshimiwa. Na kama kuna sisi “wananchi wa kawaida” basi mantiki ni kwamba wapo “wananchi maalumu” ambao labda ndio wanaitwa waheshimiwa.
Nitaanza na taswira ya kwanza. Taswira ya kwanza inalitazama Bara la Afrika kwa muktadha wa kule lilikotoka na yale lililoyapitia. Kwa wanaojali kufuatilia historia wanajua Bara hili limepitia madhila gani kufika hapa lilipo leo. Na kwa hakika, kwa binadamu yeyote kutoshtushwa au hata kutokutafakarishwa na historia hii kunakaribisha hatari ya kusababisha historia hii hii ijirudie hata vizazi na vizazi.
Demokrasia ya ukombozi itajaribu kudadisi maswali niliyojaribu kuuliza katika makala yaliyopita: Je, tunawezaje kujenga mifumo ambayo itatusaidia kuishi katika jamii inayoheshimu utu wa kila binadamu; inayojitambua kwa kujua historia ya tulikotoka na inayojua tunapaswa kuelekea wapi; inayotengeneza fursa kwa kila mtu kujiendeleza na kuendeleza taifa lake bila kuruhusu unyonyaji au ukandamizaji unaosukumwa na hulka ya ubinafsi, tamaa na ukatili wa mtu mmoja mmoja au vikundi vinavyojitafutia vitu kwa ulafi?
Je, tunawezaje kujenga jamii ya watu ambao watajua na kudai haki zao, lakini wakati huo huo wakijua na kutimiza wajibu wao pia katika kulinda ustawi wa taifa zima; jamii ambamo viongozi pia wanaheshimu sheria na wanajua maana na umuhimu wa kuwajibika kwa wananchi? Je, tunawezaje kujenga jamii ya watu wanaofikiria miaka 200 na zaidi mbele na si miaka mitano tu ya uchaguzi?
Na umuhimu wa kujenga taifa la namna hiyo, taifa ambalo watu hawaishi kama wanyama wa mwituni ambao kwao mwenye kucha ndefu au pembe ndefu au maguvu kuliko wengine ndiye mwenye haki zaidi; umuhimu wa falsafa ya kuishi katika taifa la aina hiyo hauhimizwi tu katika falsafa za dini mbalimbali, falsafa za Afrika ikiwamo Ubuntu au hata na tafakuri tunduizi (tafakari huru na dadisi) peke yake bali matokeo ya kuishi kinyume chake pia. Kwamba popote pale katika historia ambapo mambo ya msingi kama vile utu, uhuru, usawa, haki, uwazi, ushirikishwaji, yalipuuzwa katika mfumo wa utawala wa dola husika basi matokeo yalikuwa wazi. Kulikuwa na dhahama. Ndiyo maana mataifa 50 yaliyokutana San Fransisco Marekani mwaka 1948 baada ya Vita Kuu vya Pili kumalizika, walipokuwa wakijadili namna ya kuepuka vita waliyokuwa wameshuhudia, walihimiza umuhimu wa haki za binadamu.
Taswira hii ya ukombozi mara nyingi huonekana kama ya kufikirika zaidi isiyozingatia hulka ya binadamu. Lakini mataifa mengi, hasa yaliyoendelea, yamejaribu kupunguza makali ya mfumo wa ubepari kwa kuhakikisha yamejenga taasisi zinazompa kila raia walau mtizamo kwamba utu wake unaheshimiwa na kuthaminiwa; kuna fursa sawa kwa kila anayejituma na kwamba ana uhakika wa kupata haki zake za msingi kama binadamu na kama raia.
Taswira ya pili ndio uhalisia unaochukua nafasi muhimu ya demokrasia mamboleo. Uhalisia unaoanzia katika ukweli mchungu kwamba demokrasia ya kiliberali inachokifanya Afrika ni kuendeleza zaidi mianya ile ile ya kinyonyaji kwa nchi masikini badala ya kuwakomboa wananchi wa Bara hili.
Demokrasia hii ya kiliberali ilipokuwa ikibisha hodi kuingia Afrika iliorodhesha matatizo ambayo ilikuwa imetumwa kuja kuyaondoa. Miongoni mwa matatizo yale, kulikuwa na: sera mbovu za kiuchumi; umasikini uliokithiri miongoni mwa masikini; watawala kugombania na kung’ang’ania madaraka; ukabila na ubaguzi; ukandamizaji mkubwa wa haki za binadamu; uongozi unaostawi katika rushwa na wizi wa mali ya umma; upendeleo katika kugawa keki ya taifa; nakisi ya uongozi bora na mfumo wa utawala uliokuwa umekosa uhalali.
Na kweli demokrasia hii ilivyoingia tu kuna mabadiliko yalianza kuonekana. Watu wakawa na uhuru wa kutoa yaliyo moyoni. Watu wakawa na uhuru wa kutofautiana. Watu wakawa na uhuru wa kutukana. Watu wakawa na uhuru wa kufanya shughuli za kuwaingizia vipato kutokana na fursa mpya. Takwimu za uchumi zikaanza kupaa. Miundombinu ikajengwa. Chaguzi zikafanyika na kuhusisha washindani. Wawekezaji kutoka nje wakafurika na kuwekeza katika sekta kubwa kubwa kama vile mabenki, madini, viwanda, ujenzi, mawasiliano, huduma, n.k., na wazalendo wachache pia nao wakainukia katika ujasiriamali.
Zipo changamoto za msingi ambazo demokrasia hii haiwezi kuzijibu kwa sababu hata yenyewe haizijui. Iliambiwa tu ije Afrika ifanye kazi kwa misingi fulani (kama vile kufungua masoko, kusaidia upatikanaji wa fursa kwa wenye pesa kuwekeza, n.k.) basi. Changamoto kubwa ambayo demokrasia hii, kama ilivyo, haijajibu ni: Je, maendeleo ni nini? Je maendeleo yanaletwa na nani na kwa ajili ya nani?
Dhana kuu iliyojengwa katika demokrasia hii ni kuwa maendeleo yanaletwa na kukua kwa uchumi. Na kwamba uchumi unakua sana katika nchi iliyojitahidi kuita wawekezaji wengi kutoka nje. Na kwamba wakija wawekezaji wengi na kuwekeza katika madini, mafuta, viwanda, kilimo, mabenki, mawasiliano, n.k. wanatoa fursa za ajira, wanalipa kodi, wanachangia katika mnyororo wa shughuli za kiuchumi kwa ujumla.
Lakini kwa sasa ni dhahiri kuwa uchumi wa aina hii unatengeneza raia wengi zaidi wenye sifa zifuatazo: Consumer (yaani mlaji), customer (yaani mteja) au target audience (yaani walengwa shabaha), na mengine kama haya. Na kama anavyobainisha mwanazuoni wa Marekani Robert Dalh (1998), katika demokrasia ya kiliberali vyama vingi na uchumi wa soko huria ni kama chanda na pete. Wakati kiuchumi raia wengi wanakuwa walaji, wateja na walengwa, katika uwanda wa siasa wanakuwa wafuasi, wapigakura au wapigadebe.
Na katika muktadha wa aina hii inakuwa dhahiri kuwa wananchi hawawezi tena kuendelea kuwa na madaraka ya kudhibiti hatma yao ya maisha katika nyanja za utamaduni, uchumi, siasa na hata teknolojia.
Wakati wawekezaji wakifanya hima kuwekeza katika kila nyanja wawekezewa wanafundishwa kuwa walaji na wateja watiifu, kama walivyo mateja. Na madhali wawekezaji wanakuwa wamewekeza kwa wingi na kuzalisha vitu vingi basi wawekezewa wanajikuta wakitamani na kupenda vitu kuliko hata utu.
Na katika siasa, walaji wale wale wanafundishwa kuwa wapigakura waaminifu au wafuasi watiifu wa kundi fulani la watu walioamua kukamata madaraka ya dola na kuendeleza mradi wa mabeberu wa kufyonza rasilimali za watu masikini duniani. Na madhali wawekezewa wana tamaa ya vitu ambavyo vimekuwa vingi – bila kujali ubora, usalama au faida ya vitu vyenywewe – basi mfumo wa maisha unakuwa kama gulio. Kila kitu, ikiwamo utu, kinakuwa na bei na kinafikishwa sokoni kuuzwa.
Katika demokrasia pandikizi yafuatayo yanafanyika: Kunakuwa na uchaguzi kila baada ya kipindi fulani takriban baada ya miaka mitano ambamo wapigakura huingizwa katika mchakato unaoambatana na kampeni zinazohusisha ushindani wa vitu viwili: Matusi na Ahadi.
Wagombea ambao mara nyingi ama wanakuwa na pesa zao za kutosha – au wanakuwa wamefadhiliwa na wenye vitu – wanapita kwa wapigakura na wafuasi wao, huku wakiambatana na wapigadebe wao, kuomba wachaguliwe “ili wawaletee wananchi maendeleo.” Huko wagombea hushindana kwa umahiri wa kutukanana na kutoa ahadi zisizotekelezeka.
Na kwa vile wapigakura au wafuasi wale ndio wale wale walaji, wateja na walengwa, basi wanasiasa wale kutoka kundi la wenye vitu na wale ambao Profesa Chachage aliwaita Makuwadi wa Soko Huria hutumia mbinu ile ile inayofanana na uhalisia wa majina yao kuwapata wananchi.
Kwanza wagombea hawa ambao leo hii huitwa waheshimiwa huwalenga walengwa wale kwa rushwa. Kisha huwapa walaji pilau na mwisho humalizia kwa kuwapa wateja unga. Wagombea hufanya hivyo wakijua kuwa walengwa wakishalengwa au walaji wakishakula pilau basi wanakuwa wamemalizana. Na wateja wakishabwia unga wanadata kwa miaka mitano mingine.
Baada ya uchaguzi waheshimiwa huelekea mjini kupanga dili na mikakati ya kupata pesa zaidi za kuwalengea walengwa na kuwalisha walaji na kuwanunulia wateja unga ili wao – na kikundi chao – waendelee kuwa waheshimiwa kwa miaka mingi ijayo na wapiga kura wetu waendelee kubaki wafuasi wao na wateja wao.
Rasilimali zitachotwa waziwazi mchana kweupe si kwa sababu walinzi hawajui, la hasha. Katika demokrasia pandikizi walinzi ndo hugeuka kuwa wezi. Na pale wananchi mmoja mmoja au vikundi wanapojitokeza kupaza sauti kwamba rasilimali zao zinaibwa mchana kweupe wanashangaa wanapojikuta wakikamatwa na kuswekwa ndani kwa sababu ya uchochezi.
Katika demokrasia pandikizi inajengwa dola ambayo lengo lake si kulinda maslahi ya wananchi ambao kimsingi ndio wenye nchi. Dola inajengwa kwa misingi ya kulinda waheshimiwa wasije wakaishiwa. Na kadri waheshimiwa wanavyozidi kubadilishana nyadhifa za uongozi wao kwa wao (elites) ndivyo wanavyozidi kuwa na vitu zaidi vya kulengea walengwa, kuwalisha walaji na kuwanunulia unga wateja ili kila kundi libakie pahala pake.
Haya pia yanatokea hata katika nchi ambazo vyama vya upinzani vimeingia madarakani vikiahidi kuleta mabadiliko makubwa yanayolenga ukombozi kamili wa watu wao. Tuliyaona Kenya, Zambia, Zimbabwe, Malawi na kwingineko.
Ndani ya demokrasia pandikizi si tu kwamba waheshimiwa hupenda kuhodhi nguvu za dola peke yake kwa ajili ya kudhibiti wanaotishia raha yao ya kuwa madarakani bali pia huhakikisha hata vyombo vya habari wanavimiliki wao au wanavidhibiti sawasawa ili visiropoke kuhusu dili zao za kupata vitu zaidi.
Mwaka jana kulitokea mzozo kule Kenya baada ya serikali ya nchi hiyo kutangaza muswada wa kudhibiti asasi za kiraia. Katika mazingira ya kawaida ya ukombozi tungelisema ni sawa serikali ina wajibu wa kudhibiti wageni wanaojaribu kuleta fedha zao na kutufundisha ni yepi yanayotufaa sisi kama Waafrika.
Lakini kinachofanyika kule na kwingineko haya yanapotokea ni yale yale ya kundi lile lile linalohusiana na wenye vitu wakuu ambao salama yao ni kudhibiti kila mdomo wenye kelele ilhali wao waendelee na dili zao, wapate vitu zaidi, kwa ajili ya kuwalenga vizuri walengwa wao, kuwalisha walaji wao na kuwanunulia unga wateja wao.

src
RAIA MWEMA
0 comments:
Post a Comment