

Mtu unayetarajia kuungana naye katika ndoa, anatakiwa awe na vigezo vya kutosha. Nitakuambia jambo moja muhimu; wengi huishi kwa kipindi kirefu zaidi na wake/ waume zao kuliko walivyoishi na wazazi wao nyumbani.
KWA NINI?
Chukulia kwamba mtoto anazaliwa kwa wazazi wake, analelewa, anaanza kusoma na kuhitimu chuo. Kwa wastani anaweza kumaliza masomo yake akiwa na umri wa kati ya miaka 18 – 25. Baada ya hapo, vijana wengi (hasa wavulana) huanza kujitegemea kabla ya baadaye kuingia kwenye ndoa.
Ukiangalia hapo, utagundua kuwa wengi huishi kwa vipindi vifupi zaidi na wazazi wao nyumbani kuliko na wanandoa wao. Kwa maana hiyo basi, ni muhimu sana kuangalia mtu unayetaka kuungana naye.
Hebu leo nizungumze kidogo na wavulana, nitawasaidia kujua mambo muhimu zaidi kuhusu msichana anayefaa kuolewa na akawa mke bora kwenye familia.
MITAZAMO YA WENGI
Vijana wengi wa sasa huongozwa zaidi na hisia za nje. Mitazamo yao huangalia kwenye uzuri na mvuto wa mwanamke badala ya kuangalia mwenye sifa halisi za kuwa mke mwema.
Ndugu zangu, suala la uzuri wa nje si muhimu. Unaweza kuoana na mwanamke mzuri sana lakini akawa na tabia za hovyo, matokeo yake nyumba inakuwa haina amani, migogoro kila kukicha na mambo mengine yasiyopendeza.
Sisemi kwamba wanawake wazuri hawafai kuolewa hapana! Labda nifafanue zaidi – wanawake wote wanaweza kuwa wazuri, lakini uzuri wa nje isiwe kigezo cha uchaguzi wa mke bora.
Mke anaangaliwa tabia. Unaweza kukutana na mwanamke asiye na mvuto wa kutisha au asiye na mvuto kabisa lakini akawa na kiburi, dharau na tabia nyingine ambazo zitasababisha ndoa iwe chungu.
MKE SAHIHI NI YUPI?
Nimeshafafanua mambo kadhaa kwenye kipengele kilichopita, lakini sifa kuu ambayo inabeba mengine yote kwa mwanamke anayefaa kuwa mke ni upendo wa dhati wa pande zote mbili.
Hapa namaanisha kuwa, lazima umpende naye akupende.

Kuna baadhi ya watu huamini kuwa mtu anaweza kubadilika taratibu. Kwamba unaweza ukaoana na fulani hata kama ana tabia mbaya, atabadilika ndani ya ndoa. Si kweli.
Lazima tabia zake zikuridhishe ipasavyo ndipo uchukue jukumu la kupeleka posa na mambo mengine.
UTAMJUAJE?
Kuna njia nyingi za kumchunguza mwanamke ili kumjua kama anafaa. Mengi nilishaandika huko nyuma, kuhusu kumpima kwenye mambo mbalimbali na kuona kama kweli ana vigezo bora.
Ukitaka kumjua vizuri mwanamke sahihi mchunguze kupitia ndugu, marafiki na watu wake wa karibu. Chunguza familia yao, ni watu wa namna gani? Wanaishi vipi na watu?
Misingi yao ya kiimani ikoje? Siku zote mtoto huiga tabia za wazazi na watu wake wa karibu hivyo bila shaka yoyote kupitia ndugu zake unaweza kumjua vyema mkeo mtarajiwa.
Marafiki, kuna baadhi ya mambo huwa kama ya kurithi.
Kwa mfano, ukiona familia, mama ana tabia mbaya, anagombana na watu kila siku, anaoekana kwenye kumbi za starehe na utu uzima wake, tuhuma za usaliti zinamuandama na mengine, ujue hapo huwezi kupata mke sahihi.
SIFA ZA ZIADA
Mwenye mapenzi ya dhati utamjua kwa mambo mengi rahisi; hatakuwa mtu wa kutaka sana fedha, atakuheshimu na kukusikiliza. Atakujali na akisikia umepata tatizo atalichukulia kama lake, hata kama hatakuwa na uwezo wa kukusaidia, lakini utaona namna alivyoguswa.
Mengi nimeshazungumza kwenye mada zilizotangulia. Naamini mpaka hapo nimesomeka vyema, tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine, USIKOSE!
Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Saikolojia ya Uhusiano anayeandikia Magazeti ya Global Publishers. Kwa sasa anaandaa kitabu chake kipya cha Maisha ya Ndoa.
0 comments:
Post a Comment