
May 2015 Watawala wa taifa huziibia nchi nyingine MIONGONI mwa sifa kuu za utaifa mojawapo ni kwamba katika nchi ambayo imekuwa taifa na watu wake wanajinasibu kama watu wa taifa moja, nchi hiyo haitavumilia watawala wake waiibie nchi yao. Ukiona nchi inao watawala wanaoiibia nchi hiyo na kisha usione hatua zinazochukuliwa dhidi yao, ujue nchi hiyo si taifa: ama haijawahi kuwa taifa. Maelezo yake si magumu. Ni kwamba nchi ya watu wanaojenga utaifa ni nchi ambayo imejitambua kwamba watu wake ni wamoja, sudi yao ni moja, maslahi yao ni mamoja, na mustakabali wake ni mmoja. Watu walio katika hali hiyo wanakuwa wamejenga dhamira ya kuijenga nchi yao na kuifanya taifa, na kuitendea kila jambo lililo jema taifa hilo kwa sababu wanaamini kwamba limewazaa, limewalea na litawatunza, na kwamba litaendelea kuzaa, kulea na kutunza warithi wao ambao nao wataendeleza mema waliyoyafanya watangulizi wao. Ngazi za utaifa zinaweza kutofautiana. Kuna mataifa madogo, na kuna mataifa makubwa. Nilisema mwanzoni mwa ngwe hii ya fikra zangu kwamba tukitaka kujua mataifa ya kweli tuliyonayo inatubidi tuangalie yale tunayoyaita makabila, kwa sababu katika sehemu nyingi nchini haya bado ndiyo mataifa yetu kwa maana kwamba watu wetu wanajitambua zaidi ndani yake kuliko wanavyojitambua ndani ya mataifa tuliyofinyangiwa na wageni kutoka Uropa. Hali hii si ya kwetu pekee; ni kota katika bara la Afrika. Nakumbushia tena kwamba ingawaje tulijaribu kupunguza makali ya utaifa wetu wa asili (makabila) na kujenga taifa moja kubwa, lakini hisisa za utaifa ule wa asili bado ziko, na kama zisipoangaliwa vizuri zinao uwezo wa kuzusha zahma. Labda ni kweli kwamba kwetu nchini hapa tuliweza kufifisha hisia hizo, lakini itakumbukwa nilimnukuu rafiki yangu marehemu JD Ngonya aliyeniambia kwamba lugha ya mama yake ni Kinyakyusa, na haiwezekani ikawa Kiswahili. Ikumbukwe pia kwamba nilisema, nami naamini kwa dhati, kwamba bila lugha hakuna taifa. Lakini tukivinjari nchi nyingine, ambazo nazo zilivishwa utaifa wa mpakazo ulioletwa na wakoloni waliokuwa na nia ya kutuweka pamoja ili tuwatumikie kwa tija zaidi, hili linajitokeza kwa uangavu mkubwa zaidi. Tukiiangalia nchi kama Kenya, ni dhahiri kwamba watu tunaokutana nao mara nyingi wanakuwa ni Wakikuyu kwanza, halafu ndio wanakuwa Wakenya. Ni vivyo hivyo kwa Wakamba, Waluo, Waluhya, Wakisii, na kadhalika. Hali hiyo imeathiri siasa za Kenya kwa kiwango kikubwa mno, kiasi ambacho ni kikubwa mno, na wakati mwingine kinatishia amani na uwepo wa nchi hiyo. Lakini hatuwezi kuwacheka Wakenya kwa sababu tu wao wameng’ang’ania utaifa wao wa kimsingi na wa awali. Hata sisi, tukishindwa kujenga utaifa ulio imara, tutarejea utaifa wetu wa asili kirahisi. Ujenzi wa utaifa mpya, mkubwa na ulio imara ndiyo mada kuu ya makala zangu katika sura hii. Wajenzi wa taifa hawaliibii taifa lao. Watawala wa nchi ambayo inajitambua kama taifa hawamvumilii yeyote miongoni mwao ambaye anaonyesha dalili za kutaka kujinufaisha kutokana na jasho lao, au anayetenda mambo ambayo yanaweza kuligharimu taifa lake kwa namna yoyote ile. Kwa mfano, masuala ya usalama wa taifa lolote ni mambo muhimu kwa kila mzalendo na kwa kila anayejihisi kwamba ni sehemu ya taifa hilo. Lakini usalama siyo tu mambo yanayohusu silaha za wavamizi au ugaidi. Matendo yanayoweza kuhatarisha usalama wa taifa ni pamoja na wizi na udanganyifu, hila na ulaghai unaoelekea kuwanyang’anya watu matunda ya jasho lao na kuwanyima haki zao za msingi. Jamii ambayo ndani yake hakuna haki, watu wanaviziana na kunyang’anyana, jamii ambayo imepoteza kabisa hisia na tabia za utu na uungwana, hiyo ni jamii ambayo inaelekea katika kujichanachana katika misambaratiko na mapigano. Bila haki hakutakuwa na amani na utangamano. Kwa hiyo, narudia kwamba ndani ya taifa hakuna watawala wanaoliibia taifa halafu wakaachwa bila kuchukuliwa hatua. Mataifa huwa yanaiba, na watawala wa mataifa hayo ndio wanaopanga wizi huo. Lakini wizi huo hawaufanyi dhidi ya watu wao; wizi huo huufanya dhidi ya mataifa mengine, au dhidi ya vijinchi vilivyoshindwa kuwa mataifa, na kwa udhaifu wake, vikajikuta ni rahisi kuvipiga na kuvinyang’anya mali zake, hata kuvichukulia watu wake kama watumwa, kama tunavyojua. Kwa hiyo, miongoni mwa mambo ya awali ya kuuliza kuhusu iwapo nchi ni taifa ni je, kuna wizi unafanywa na watawala wa nchi hii? Kama ni kweli, upo, je watawala wanapopanga mbinu za kuiba, na wanapotoka kwenda kuiba, ni nani anaumizwa. Kama wizi huo unaliumiza taifa, na kama wizi huo unaidhoofisha dola ya nchi hiyo, elewa moja kwa moja kwamba nchi hiyo si taifa. Iwapo wizi na uporaji unaofanyika ni dhidi ya nchi nyingine, na matunda ya wizi huo yanasombwa na kuletwa nyumbani ili yatumike kwa maslahi ya nchi, hapo utajua kwamba hilo ni taifa iwapo sifa nyingine za utaifa zimekamilika. Tumekuwa tukishuhudia vitendo vya wizi na uporaji miongoni mwa watawala wetu bila kuona dalili za utashi wa kuadhibu vitendo hivyo. Ndiyo maana ninajiuliza kama kuna watu ambao wana uchungu wa kweli kuhusu nchi hii, kama kweli wanayo nia ya kuifanya iwe taifa, au kama wanaiona nchi hii kama mahali pa kuchumia matumbo ya familia zao. Aidha nitaangalia nchi zilizojenga mataifa, na mataifa hayo yakawastawi na kutamalakiki sehemu nyingi duniani kwa njia za wizi, lakini wizi waliokuwa wakitendewa watu wa mataifa au nchi nyingine -
src
Raia mwema
0 comments:
Post a Comment