WIKI iliyopita Rais wetu, Jakaya Kikwete, alikuwa jijini London pamoja na
Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, (naambiwa ni marafiki wa
karibu) kuhudhuria mkutano wa kimataifa wa namna ya kukomesha biashara haramu
ya pembe za ndovu duniani.
Rais alitumia fursa hiyo ya kuwepo Uingereza ‘kujisafisha’ dhidi ya habari
zilizoandikwa na gazeti la Sunday Mail la nchi hiyokwamba serikali yake
hajachukua hatua zozote kupambana na biashara hiyo haramu nchini.
‘Kujisafisha’ huko pia kulifanywa na Nyalandu kwa kuzungumza na vyombo vya
habari vya hapa nchini kabla ya safari hiyo ya London. Kwenye mkutano huo
Nyalandu alisema lengo la gazeti hilo lilikuwa ni kuchafua jina la Tanzania
kabla ya mkutano huo wa London.
Ni kwa lengo hilo la ‘kujisafisha’, Rais Kikwete aliweza kupata fursa ya
kuzungumza na mwandishi maarufu wa CNN, Christine Amanpour na pia Idhaa ya
Kiswahili ya BBC.
Sina hakika iwapo ni yeye Kikwete aliyeomba mwenyewe kuhojiwa na CNN na BBC
kuhusu suala hilo au ni vyombo hivyo viwili vyenyewe vilivyoomba kumhoji.
Hilo, hata hivyo, si la msingi katika tafakuri yangu ya leo; bali la msingi
ni kuangalia iwapo ripoti hiyo ya gazeti la Uingereza, ambayo imemkera Kikwete
na Serikali yake ina ukweli wowote au ni “upotoshaji mtupu na upuuzi”
kama Kikwete mwenyewe alivyoiambia BBC.
Labda nianze na takwimu. Sensa ya tembo iliyofanywa na Serikali mwaka jana
inaonyesha kuwa idadi ya tembo nchini imepungua kwa asilimia 66 ikilinganishwa
na idadi ya sensa ya mwaka 1990. Selous -Mikumi wamebakia tembo 13,084 tu
wakati Ruaha - Rungwe wamebakia 20,000 tu! Kwa wastani tembo 11,000 huuawa
nchini kila mwaka na majangili.
Kama nilivyoeleza mwanzo, gazeti hilo liliandika kuonyesha kwamba Serikali
ya Tanzania haijachukua hatua zozote kupambana na biashara ya pembe za ndovu
nchini, na ndiyo maana idadi ya tembo inazidi kupungua. Je, ni kweli Serikali
haijachukua hatua zozote? Jibu langu ni ‘si kweli’.
Jibu langu ni hilo kwa sababu Serikali imechukua hatua kadhaa na sote
tunazijua; huku ya hivi karibuni kabisa ikiwa ni kuanzisha Operesheni
Tokomeza.
Kama jibu ni ‘si kweli’, ukweli ni upi? Kwa mtazamo wangu, ukweli ni kwamba
Serikali imechukua hatua kadhaa kupambana na tatizo hilo, lakini hatua hizo
hazijaleta matokeo yoyote makubwa, na ndiyo sababu biashara hiyo bado imepamba
moto hata sasa nchini.
Katika hali hiyo, usahihi wa ripoti ya Sunday Mail ungekuwa kwamba;
Serikali ya Tanzania inachukua hatua mara kwa mara kupambana na biashara haramu
ya pembe za ndovu, lakini hatua hizo zimeshindwa, mpaka sasa, kuleta matokeo
makubwa. Huo ndiyo ukweli usiopingika.
Ni kwa nini hatua hizo za Serikali zimeshindwa, mpaka sasa, kuikomesha
biashara hiyo hapa nchini? Swali hili nitalijibu baadaye, lakini kwa sasa
tukubaliane tu kwamba serikali – kuanzia ya Mwalimu Nyerere, Ali Hassan Mwinyi,
Benjamin Mkapa, na sasa ya Jakaya Kikwete, zimekuwa zikichukua hatua
kukabiliana na hali hiyo, lakini ujangili bado umepamba moto.
Tukirejea kwenye suala la habari hiyo ya Sunday Mail, mimi nadhani
Kikwete na waziri wake Nyalandu walikasirishwa nayo sana bila kwanza
kuzingatia maudhui ya jumla ya ripoti hiyo ya gazeti hilo la Uingereza ambayo
ni kwamba ujangili bado ni tatizo kubwa Tanzania.
Natambua wazi wajibu wa rais, waziri na kwa hakika kila Mtanzania, wa
kuonyesha hisia za kizalendo kila nchi yetu inapoguswa kwa mabaya na vyombo vya
habari vya nje, lakini hiyo haihalalishi kauli za kupitiliza (over reacting)
kwenye suala lenye ukweli fulani ndani yake.
Kwa mtazamo wangu, Kikwete kuiita ripoti ile ya Sunday Mail kuwa
ni “uzushi na upuuzi mtupu” ni ku-over react kwa jambo lenye
ukweli fulani ndani yake.
Kwa ufupi, Serikali haikuwa na sababu yoyote muhimu ya ku-over react,
na haina ushahidi kwamba gazeti hilo lilikuwa na ajenda ya kuichafua sifa ya
Tanzania zaidi ya kuieleza dunia hali ilivyo hapa nchini ya mauaji ya
kusikitisha ya tembo wetu.
Nasema Serikali haikuwa na sababu yoyote nzito ya ku-over react kwa
sababu ya mambo mawili makubwa. Jambo la kwanza ni kwamba hoja kuwa taarifa
hiyo ya Sunday Mail ililenga kuichafua Tanzania haina mashiko kwa kuwa
jina la Tanzania lilishachafuka kwa muda mrefu sasa kuhusu biashara hiyo haramu
ya meno ya tembo, na ushahidi upo.
Lakini pili, maudhui ya ujumla ya ripoti ile ya Sunday Mail ni
sahihi. Ni sahihi kwa sababu ujangili bado umeshamiri sana katika Tanzania, na
watawala wetu japo wanachukua hatua, lakini hatua hizo hazijaleta mabadiliko
yoyote makubwa, na ushahidi wa kitakwimu upo, na unaonyesha kuwa idadi ya tembo
wanaouawa kila mwaka sasa imefikia 11,000.
Labda nitoe mfano kuthibitisha kwamba sifa ya Tanzania kwenye suala la
biashara ya pembe za ndovu duniani ilishachafuka muda mrefu uliopita, na kwa
maana hiyo, gazeti hilo la Uingereza haliwezi kuwa na ajenda ya kuchafua jina
la nchi ambayo tayari limeshachafuka!
Mwaka 2010 katika mkutano wa mwaka wa CITES (Convention on International
Trade in Endagered Species) ambayo Tanzania ni mwanachama, ombi la Tanzania
kutaka kuuza shehena ya meno ya tembo iliyoyakamata iliyofikia tani takriban 90
lilitupiliwa mbali kwa sababu kuu nne.
Moja ni kwamba kama ruhusu hiyo ingetolewa kulikuwa na wasiwasi kuwa meno
ambayo yangeuzwa si yale tu yaliyokuwepo Ivory Room (Dar es Salaam) kwa
wakati ule bali wajanja wangepenyesha na mengine yaliyopatikana kupitia
ujangili.
Sababu ya pili ilikuwa ni kwamba Tanzania ilikuwa “imeruhusu” nchi
yake kuwa njia ya biashara haramu ya meno ya tembo kutoka nchi za Kusini
zikiwemo Zambia na Malawi. Sababu ya tatu ni kwamba Tanzania ilikuwa haifanyi
jitihada za kutosha kulinda tembo wake hasa katika mbuga za hifadhi kama
Selous.
CITES iliona kwamba Tanzania ilikuwa na uwezo wa kulinda tembo wake lakini
haikutekeleza jukumu hilo kwa dhati na hivyo kusababisha ujangili kushamiri.
Na sababu ya mwisho ni kwamba Tanzania haijachukua hatua madhubuti
kupambana na biashara haramu ya meno ya tembo na kwamba serikali haijadhamiria
kukomesha biashara hiyo.
Hiyo ilikuwa ni miaka minne iliyopita. Yaani, kwa ufupi, CITE ilikuwa
inasema kuwa sifa ya Tanzania ya kulinda tembo wake ni mbaya, na ndiyo maana
ombi lake lilikataliwa.
Sasa, kuaje leo Rais Kikwete na Waziri Nyalandu walijie juu gazeti hilo la
Uingereza kuwa linachafua jina la Tanzania; ilhali jina hilo, katika suala hilo
la kulinda tembo wasitoweke duniani, lilishafuka?
Mfano wa pili ni wa Machi mwaka jana ambapo mkutano mwingine wa mwaka wa
CITE uliingiza Tanzania katika orodha iliyoitwa “GENGE LA NCHI NANE” (Gang
of Eight). Orodha hiyo ni ya nchi zilizokubuhu kwa biashara haramu ya pembe
za ndovu duniani. Nchi nyingine katika orodha hiyo ni Kenya, Uganda,
China, Thailand, Malaysia, Vietnam na Phillipines.
Sasa, nchi ambayo tayari ilishaingizwa katika orodha ya dunia ya Gang of
Eight ya nchi zinazoongoza kwa biashara haramu ya pembe za ndovu yawezaje
kulalamikia gazeti hilo kuwa linachafua sifa ya jina lake kimataifa? Sifa gani
ya kulinda katika biashara hiyo ya pembe za ndovu kama tayari jina la nchi limo
katika orodha hiyo ya Gang of Eight?
Ndugu zangu, tuambizane ukweli na ukweli ni huu: Ujangili umekuwepo miaka
mingi nchini tangu enzi za Nyerere na kila mara Serikali imekuwa ikichukua
hatua kukabiliana nao. Hata hivyo, hatua hizo zimeshindwa kuutokomeza kabisa
uhalifu huo nchini.
Katika miaka ya karibuni hali ndiyo imezidi kuwa mbaya. Kumbukumbu
zinaonyesha kuwa hata gari la Ikulu yetu (Toyota Land Cruiser) lilipata
kukamatwa huko Kibiti likiwa na shehena ya pembe za ndovu baada ya kupata
ajali. Si hivyo tu, hata magari ya JWTZ yamepata nayo kukamatwa yakiwa na pembe
hizo!
Rais Kikwete mwenyewe, katika mahojiano ya mwishoni mwa wiki na BBC,
alikiri kuwa hali ni mbaya kiasi kwamba askari wa wanyamapori waliposhindwa
kuidhibiti hali hiyo aliamuru Polisi waingie, lakini nao wakashindwa, na ndipo
alipoamuru JWTZ waingie (Operesheni Tokomeza).
Hata hivyo, ukweli ni kwamba mpaka operesheni hiyo iliposimamishwa,
biashara hiyo haramu ya pembe za ndovu ilikuwa haijatokomezwa kabisa, na
operesheni iliposimamishwa biashara ikarejea katika kasi ile ile ya mwanzo!
Sasa nirejee katika lile swali nililoliacha kiporo la ni kwa nini, pamoja
na hatua zote zinazochukuliwa na Serikali, bado biashara haramu ya pembe za
ndovu inashamiri Tanzania.
Jibu langu kwa ufupi ni kwamba kinachotukwaza ni kuenea kwa utamaduni wa
ufisadi katika kila kona ya maisha yetu. Watanzania tunatafuta utajiri na
maisha mazuri kwa njia ya mkato, na katika miaka ya karibuni tumegundua kuwa
njia nzuri ya mkato ni ya ufisadi!
Tatizo hili (ufisadi) ndilo ambalo Joshua Lawrence, kwenye makala yake
katika gazeti hili, aliliita “anguko la kimaadili” na “virusi vya kimfumo”.
Katika mahojiano yake na BBC, Rais Kikwete alitamka kwamba anayo majina ya
majangili papa 40 nchini, na kwamba wanaongozwa na tajiri mmoja wa Arusha! Mtu
unajiuliza; kama Rais ana majina hayo, mbona hatoi amri wakamatwe?
Utakumbuka pia kwamba Kikwete alishawahi kusema kuwa ana orodha ya majina
ya vigogo wanaojishughulisha na biashara haramu ya madawa ya kulevya, lakini
mpaka sasa hatujasikia kigogo yeyote akikamatwa! Kwa nini?
Jibu langu ni ufisadi. Yawezekana hao wanaopaswa kuwakamata vigogo hao wamo
kwenye “payroll” isiyo rasmi ya mafisadi hao wa biashara hizo haramu za
pembe za ndovu na madawa ya kulevya.
Lakini pia yawezekana vigogo hao wamo katika orodha ya wafadhili wa chama
tawala CCM, na ndiyo sababu kuna kusitasita kuwakamata.Ni ufisadi.
Vyovyote vile, ufisadi huu haufanywi tu na vigogo wa juu wa biashara hizo
bali pia umesambaa mpaka chini kwenye polisi wa kawaida, viongozi wa serikali
za vijiji, wilaya na mikoa, na hata wananchi wa kawaida.
Tumefika mahali pabaya kiasi kwamba hata humo kwenye wanaounda vikosi vya
hizo operesheni wamo wajumbe mafisadi ambao huvujisha siri za operesheni kwa
mafisadi hao ili walipwe mapesa mengi kwa kuwasaidia wasikamatwe. Na hata
wakikamatwa, wapo mahakimu walio kwenye “payroll” za mafisadi hao ambao
huhakikisha hawafungwi!
Hapo ndipo tulipofikia. Ndiyo maana naamini kwamba, bila kwanza kuitokomeza
kansa hii kuu ya anguko la kimaadili (ufisadi), tutaendesha operesheni za kila
aina dhidi ya biashara haramu ya pembe za ndovu, lakini bado itaendelea
kushamiriTanzania, na bado jina la nchi yetu duniani litaendelea kuchafuka, na
haitajalisha Sunday Mail limeripoti au halikuripoti!
Na hiyo ni kwa sababu operesheni zinakuja na kupita, lakini ufisadi
unaachwa ubaki. Kwa hiyo, opereshen ikimalizika na upepo ukitulia, mafisadi
wanarejea tena kazini na kuendelea kuua tembo.
Naamini hicho ndicho Mchungaji Msigwa alichomaanisha katika kauli yake kwa Sunday
Mail, na ndivyo pia gazeti hilo la Uingereza lilivyomaanisha katika ripoti
yake.
Kwa kigezo chochote kile, huwezi kuiita ripoti yao hiyo ‘upotoshaji
mkubwa na upuuzi’ kwa sababu, pamoja na yote, kuna ukweli ndani yake kama
nilivyojaribu kueleza.
Tafakari.
Src –raia mwema
0 comments:
Post a Comment