Uzoefu
wangu wa kufuatilia masuala ya elimu unaonyesha aghlabu matatizo mengi katika
sekta ya elimu yanatokana na Serikali kama mdau mkuu.
Matatizo
hayo yanasababishwa na ama sera na mipango mibovu au kutokuwapo kwa utekelezaji
madhubuti wa mipango bora iliyobuniwa kuendeleza sekta hiyo muhimu kwa Taifa.
Huu
ndio ukweli na kwa kiasi kikubwa Serikali kama msimamizi mkuu wa elimu, haiwezi
kujitenga na lawama kuhusu matatizo yanayotokea katika sekta ya elimu.
Hata
nyumbani watoto wanapokuwa chakaramu, wa mwanzo kunyooshewa vidole ni wazazi
ama walezi wao.
Ukweli
ni kuwa elimu yetu imeshindwa kutengemaa kwa muda mrefu. Kuna viashiria
mbalimbali vinavyoonyesha kuwa elimu inayumba, imejaa migogoro inayohatarisha
mustakbali wa sekta hii mama nchini. Matokeo mabaya ya mitihani ya Taifa ni
mojawapo ya viashiria hivyo.
Hata
hivyo, wakati Serikali ikitupiwa mzigo mkubwa wa lawama kwa kushindwa
kuisimamia ipasavyo sekta ya elimu, swali la kujiuliza ni; kwa kiasi gani
wananchi tunafanya jitihada binafsi au za pamoja kuisaidia Serikali kuiendeleza
elimu yetu?
Tuachane
na masuala ya sera, mipango na mikakati ya kiserikali iliyo nje ya uwezo wa
wananchi. Hebu kwa mfano, tujiulize mimi na wewe tunafanya nini kuhakikisha
shule wanazosoma watoto wetu zinafanya vizuri kitaaluma.
Je,
mazingira katika shule zetu yanakidhi haja ya kuwa mazingira sahihi kwa utoaji
wa elimu? Tunawasimamia vipi walimu kuwajibika na hata kuwahimiza watoto wetu
kujifunza kwa bidii shuleni na nyumbani?
Ieleweke
shule ninazokusudia hapa ni zile za umma, zenye idadi kubwa ya watoto wa nchi
hii. Hivi sasa usimamizi wa shule hizi umegatuliwa, wamepewa wananchi kupitia
Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi).
Katika
maeneo mengi niliyobahatika kufika nchini, nimebaini kuwapo kwa ushiriki mdogo
wa wazazi katika maendeleo ya shule wanazosoma watoto wao. Kibaya zaidi ni pale
wazazi wanaposhindwa hata kufuatilia maendeleo binafsi ya watoto wao.
Sio
ajabu kukuta shule yenye wanafunzi zaidi ya 600, wazazi wanaohudhuria mikutano
ya shule hawazidi 100. Mikutano hii ndiyo majukwaa ya kujadili masuala
mbalimbali, lakini wazazi na walezi wanaisusa.
Tutayajuaje
matatizo ya shule na watoto wetu na namna ya kuyatafutia ufumbuzi, kama kila
siku tunawatuma watumishi wa ndani au vijana wa mtaani watuwakilishe kwenye
vikao, kisa tumetingwa na shughuli za kimaisha?
Hata
tafiti zinaonyesha kuwa ushiriki wa wazazi katika masuala yanayohusu shule
wanazosoma watoto wao hauridhishi.
Moja
ya tafiti hizo ni uchunguzi wa mwaka 2010 kuhusu utoaji wa huduma za jamii
uliofanywa na Uwezo iliyo chini ya asasi ya Twaweza.
Ripoti
ya utafiti huo uliotumia sampuli ya baadhi ya wakazi wa mkoa wa Dar es Salaam,
inasema wazazi wengi hawajui sera, mipango ya kielimu na hawana uelewa wa mambo
mengi kuhusu elimu ya watoto wao shuleni.
“Karibu
nusu tu ya wazazi ndio waliosema wanafuatilia maendeleo ya elimu ya watoto wao
katika baadhi ya mambo kama kuhudhuria mikutano ya kamati za shule na
kuzungumza na walimu kuhusu maendeleo ya watoto,’’inasema sehemu ya ripoti
hiyo.
Kwa
hali hii, tukubali kuwa nasi wazazi na wananchi kwa jumla tunachangia kurudisha
nyuma maendeleo ya elimu nchini. Tusiilaumu Serikali tu kwa kila linalotokea
shuleni.
Source
mwananchi
0754990083
0 comments:
Post a Comment