HUWEZI
amini!. Mabingwa watetezi wa ligi kuu soka Tanzania bara wameweka rehani nafasi
yao ya kutetea taji lao msimu huu baada ya kufumuliwa bila haruma mabao 2-1 na
wapambanaji wa kukwepa kushuka daraja, Mgambo JKT katika mchezo wa ligi kuu
uliopigwa uwanja wa CCM Mkwakwani, Jijini Tanga.
Yanga
wakiwa na kikosi kamili gado waliingia uwanjani wakiwa na imani kubwa ya kuibuka
na ushindi ili kuwasogelea Azam fc wanaozidi kutesa kileleni.
Maafande
wa Mgambo walianza kushusha kirungu cha kwanza katika dakika ya pili ya mchezo
kupitia kwa mshambuliaji wao hatari, Fully Maganga.
Bao hilo
lilidumu mpaka dakika 45 za kipindi cha kwanza zinamaliza.
Mbaya
zaidi, Mgambo walilazimika kubaki pungufu kwa dakika 60 baada ya mchezaji wao
Mohamed Neto kutolewa nje kwa kadi nyekundu dakika ya 30 kipindi cha
kwanza.
Baada ya
kipindi cha pili kuanza, Yanga waliingia kwa kasi wakihitaji kupata bao la
kusawazisha.
Dakika ya
50, Yanga walifanikiwa kupata penati na nahodha wake, Nadir Haroub `Canavaro`
aliukwamisha mpira kimiani kwa shuti kali.
Dakika ya
69, Mgambo JKT walipata penati iliyokwamishwa kimiani na Malima Busungu na
kuandika bao la pili kwa maafande hao wa Jeshi la kujenga
Taifa.
Mpaka
dakika 90 zinamalizika, Mgambo walikuwa mbele kwa mabao mawili, huku kikosi cha
Hans Van Der Pluijm kikiambulia bao moja la kufutia machozi.
Mechi
nyingine iliyokuwa ikiangaliwa kwa jicho la tatu ni baina ya vinara wa ligi kuu,
Azam fc dhidi ya Simba SC kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es
salaam.
Azam fc
wamefanikiwa kuvuna pointi tatu muhimu baada ya kuikung`uta Simba sc mabao
2-1.
Mabao ya
Azam fc yalifungwa na Hamis Mcha `Vialli` mnamo dakika ya 16 kipindi cha kwanza,
lakini Simba sc walisawazisha dakika ya 45 ya kipindi hicho kupitia kwa Joseph
Owino.
Azam fc
waliandika bao la pili na la ushindi kupitia kwa nahodha wake, John Raphael
Bocco `Adebayor` katika dakika ya 56.
Baada ya
mchezo huo, afisa habari Azam fc, Jafar Idd Maganga amesema bado wanaendelea
kupambana mpaka dakika ya mwisho ili kujua kama watabeba
ubingwa.
“Tunamshukuru Mungu tumeweza
kucheza kadri ya uwezo wetu na kuwafunga Simba mabao 2-1. Vijana wetu
wameendelea kukomaa na kuonesha kuwa wao ni bora. Ligi bado sana, tuna mechi
nyingine, tutahakikisha tunashinda zote na kujihakikishia ubinwa”. Alisema
Jafar.
Kwa upande
wa Simba Sc wameendelea kuwa wapole na kukubali matokeo ya
uwanjani.
Afisa
habari wa Simba, Asha Muhaji alisema mechi ilikuwa ngumu kwao kutokana na ubora
wa Azam fc, hata hivyo timu imecheza vizuri na kupoteza nafasi kadhaa za
kufunga.
“Mpira
ndivyo ulivyo. Matokeo ya uwanjani lazima uyakubali. Wenzetu walitumia nafasi
vizuri na kushinda. Tunasahau ya leo tunajiandaa na mechi ijayo”. Alisema
Asha.
Mechi
nyingine imepigwa katika dimba la Sokoine jijini Mbeya ambapo wagonga nyundo,
Mbeya City FC walikuwa na kibarua kizito dhidi ya Tanzania
Prisons.
Ulikuwa
mchezo muhimu kwa timu zote, lakini ulikuwa muhimu zaidi kwa Prisons kwasababu
wapo katika hatari ya kushuka daraja.
Dakika 90
zimemalizika kwa Mbeya City Kuvuna Pointi tatu muhimu kufuatia ushindi wa bao
1-0.
Bao hilo
limefungwa dakika ya pili ya kipindi cha kwanza kupitia kwa mshambuliaji hatari,
Paul Nonga.
Afisa
habari wa Mbeya City, Freddy Jackson alisema Prisons walijipanga vizuri kwa
lengo la kulipa kisasi cha kufungwa mabao 2-0 mzunguko wa
kwanza.
“Mbeya
City nafasi bado tunayo. Sisi tunafukuzia nafasi mbili za juu. Kufungwa kwa
Yanga leo kwetu ni heri. Tunajipanga kushinda mechi zote. Lolote linaweza
kutokeo, Kupoteza kupo”.
“Hata hao
wa juu wanaweza kupoteza na ndio maana umeona Yanga wamefungwa. Mungu atapanga
mwisho wa siku nani ashike nafasi hizo”. Alisema Freddy.
Tanzania
Prisons kupitia kwa katibu mkuu wake, Sadick Jumbe wamekiri kuzidiwa maarifa na
Mbeya City, hivyo hawana cha kulaumu zaidi ya kujipanga mechi
zijazo.
“Timu
ilicheza vizuri, lakini tulifungwa mapema na kuharibikiwa na mchezo. Bado
tunasema, nafasi yetu ipo hata kama Mgambo wameshinda leo dhidi ya
Yanga”.
“Ona
maajabu ya Mpira, Yanga wametoka kutufunga mabao 5-0, leo wamefungwa 2-1 na
wanyonge wenzetu. Lolote linaweza kutokea katika soka.” Alisema
Jumbe.
Mechi ya
Azam fc dhidi ya Simba, Mgambo na Yanga, Mbeya City dhidi ya Prisons zilikuwa na
umuhimu mkubwa zaidi kwa mashabiki na makocha wa timu hizo zinazowania nafasi
tatu za juu.
Baada ya
Azam fc kushinda, wametia mguu mmoja ndani mwingine nje katika mbio za kutwaa
ubingwa mwaka huu.
Sasa
wameshatimiza michezo 23 kwa kujikusanyia pointi 53 kileleni, huku Yanga
wakicheza mechi 22 na kuvuna pointi 46 kibindoni katika nafasi ya
pili.
Matokeo ya
Azam yamekuwa faraja kubwa kwa kocha Joseph Marius Omog wa Azam fc kwasababu
sasa ameweka pengo la pointi 7 dhidi ya mabingwa watetezi
Yanga.
Kwa maana
hiyo, Yanga wameweka ubingwa wao reheni na nguvu kubwa inahitajika kuwazuia Azam
fc ambao hawajafungwa mpaka sasa.
Yanga
wamebakika kiporo kimoja dhidi ya Kagera Sugar uwanja wa Taifa jijini Dar es
salaam, April
9mwaka huu.
Hata hivyo
bado watahitaji kujipanga zaidi kwasababu matokeo yanayopatikana uwanjani kwa
sasa yamekuwa ya ajabu kidogo.
Wakati
wanaelekea Tanga, bila shaka walidhani wanaenda kuvuna pointi tatu muhimu mbele
ya Mgambo na kila mtu alikuwa anafikiria hivyo kutokana na ubora wao na kiwango
walichoonesha kwenye mchezo uliopita dhidi ya Prisons.
Mtandao
huu jana uliwapa tahadhari Yanga kuwa wasiende kirahisi na hii ilitokana na
maneno ya kocha msaidizi wa klabu hiyo, Charles Boniface Mkwasa aliyesema kuwa
Mgambo ni timu ndogo, hivyo watahangaika sana, lakini mwisho wa siku wajue Yanga
ni timu kubwa na kongwe.
Hakuna
aliyetarajia matokeo ya leo, na hii imezidi kuwapa hofu zaidi Yanga katika
michezo yao iliyobaki dhidi ya Kagera Sugar, JKT Ruvu, JKT Oljoro na Simba
sc.
Yanga
lazima watulize akili zaidi kuhakikisha wanashinda mechi zote kama kweli
wanahitaji kutetea ubingwa wao.
Nao Azam
fc wamebakiwa na mechi tatu dhidi ya Ruvu Shooting, Mbeya City na JKT
Ruvu.
Katika
mechi hizo tatu, Mbili atasafiri kwenda mkoani Pwani na nyingine atakwenda
Mbeya, baada ya hapo atamalizia nyumbani kwake Azam Complex,
Chamazi.
Mbeya City
baada ya ushindi wa leo, wamefikisha pointi 45, pointi moja nyuma ya
Yanga.
Hii
imezidi kuwapa njia Mbeya City kuwania nafasi mbili za juu.
Kama
matokeo yanayopatikana ndio haya, huwezi kutabiri kirahisi nani anaweza kutwaa
ubingwa.
Nafasi ya
kubeba taji ipo wazi kwa timu tatu za juu na klabu yoyote inaweza kupoteza
mchezo na kujiweka mazingira magumu zaidi.
Katika
mechi nyingine leo hii, Kagera Sugar wameshindwa kutamba katika dimba lake la
nyumbani, Kaitaba, baada ya kulazimisha suluhu ya bila kufungana na Ruvu
Shooting ya Pwani.
Pale
Manungu Complex, Mtibwa Sugar wamewafumua wababe wengine wa Simba sc, Coastal
Union mabao 3-1.
Nao maafande wa JKT Ruvu
wameimaliza kabisa Rhino Rangers baada ya kuifunga mabao 3-1 katika dimba la
Azam Complex, hivyo kuwafanya maafande hao wa Tabora kuendelea na safari yao ya
kuiaga ligi kuu
Na Baraka Mpenja , Dar es salaam
0 comments:
Post a Comment