
Mwendesha baiskeli, Richard Laizer
Kati ya wanamichezo wa Tanzania waliofanikiwa kupitia michezo, hauwezi kuacha kumtaja mwendesha baiskeli, Richard Laizer anayeichezea timu ya Qhubeka Feeder ya nchini Afrika Kusini.
Laizer mwenye miaka 24 mzaliwa wa Olasti mkoani Arusha ni mtoto wa nne kuzaliwa kati ya watoto saba kwenye familia ya Laizer Loning’o.
Anasema akiwa na miaka 16 alikwenda na baba yake mdogo kushuhudia mashindano ya baiskeli yaliyofanyika mkoani humo na hapo ndipo alivutiwa na kuingia kushiriki mchezo huo ambao hivi sasa unampatia maisha mazuri.
“Kilichonivutia ni vile mshindi alivyozawadiwa zawadi mbalimbali pamoja na fedha, nilitamani kuwa kama yule hivyo niliporudi nyumbani nikaanza kujifunza kuendesha baiskeli hizi za kawaida,” anasimulia Laizer.
Anasema baadaye alijiunga na klabu ya baiskeli ya mkoani Arusha na kuwa mwanachama wa klabu hiyo huku akipewa sapoti na baba yake mdogo ambaye amewahi kushiriki mashindano mbalimbali ya baiskeli.
Ilivyokuwa hadi kuwa mchezaji wa kulipwa Afrika Kusini
“Nilikwenda Afrika Kusini kwenye kozi ya mchezo wa baiskeli nikiiwakilisha Tanzania katika kozi hiyo iliyofanyika mwaka 2012 baada ya kozi nikabahatika kupata timu kule baada ya viongozi wa timu hiyo kuona jinsi ninavyoendesha baiskeli na kuvutiwa na mimi,” anasema Laizer.
Anasema alijiunga na timu ya Qhubeka Feeder kama mchezaji wa kimataifa wa kulipwa baada ya timu hiyo kuanzishwa, ambapo wakati wanamalizia kozi iliyompeka Afrika Kusini timu ya Qhubeka Feeder ilikuwa mbioni kuanzishwa.
Anasema wakati timu hiyo inaanzishwa ilikuwa na waendesha baiskeli 13 ingawa sasa timu ni kubwa na imeshiriki mashindano mbalimbali makubwa ya ndani na nje ya Afrika Kusini na kufanya vizuri katika mashindano hayo.
“Katika timu yetu wapo wachezaji wengine pia kutoka Namibia, Eritrea na Rwanda, kwa hiyo timu yetu ni ya kimataifa kwani ina waendesha baiskeli kutoka mataifa mbalimbali,”anasema Laizer.
Tofauti ya waendesha baiskeli wa Tz na Afrika Kusini Afrika Kusini iko mbali sana kwenye mchezo wa baiskeli, hauwezi kuilinganisha na Tanzania hata kidogo,” anasema Laizer.
Laizer anasema Afrika Kusini mchezo wa baiskeli unachezwa kuanzia ngazi za chini tofauti na hapa nchini, ambapo kama usipochezwa Arusha ni Dodoma au Mwanza zaidi ya hapo hakuna hamasa nyingine.
Mafanikio aliyopata kwa kuendesha Baiskeli
Laizer ambaye ni miongoni mwa waendesha baiskeli wa Tanzania waliotajwa kushiriki michezo ya Jumuiya ya Madola mwaka huu anasema amefanikiwa kufanya mambo mbalimbali baada ya kuingia kuendesha baiskeli, lakini kubwa amejenga nyumba.
Malengo aliyonayo kwenye mchezo huo
“Bado akili yangu inaniambia naweza kuwa bingwa wa dunia wa baiskeli ili kudhihirisha hata Watanzania tunaweza katika michezo, nahitaji kufanya kitu cha ziada kuhakikisha natimiza ndoto yangu,” anasema Laizer.
Anaizungumzia vipi timu ya Qhubeka Feeder na ile ya Tz
“Upande wa Tanzania bado kuna changamoto nyingi hasa za vifaa timu zinapojiandaa na mashindano ya kimataifa, pia bado udhamini ni tatizo,” anasema Laizer.
Anasema kwenye klabu ya Qhubeka Feeder wamejipanga, wachezaji wenyewe kwa wenyewe wana ushindani, wana vifaa vya kutosha, baiskeli za kisasa na wanashiriki mashindano mengi.
src
mwananchi
src
mwananchi
0 comments:
Post a Comment