Shikamoo Januari, kwa heri Januari, tangulia Januari. Nakumbuka sana siku ulipoingia, tulikuwa nje tunakusubiri kwa hamu, na ulipofika tukaripuka kwa furaha kubwa, tukapiga miluzi, madebe, na kukumbatiana, bila kujali umemkumbatia nani, mimi mwenyewe kwa mara ya kwanza nilimkumbatia mama mwenye nyumba wangu na tukapeana pongeza kubwa, na kutakiana heri ya mwaka mpya wenye furaha. Nilimkumbatia jirani yangu, baadaye nikamkumbatia mke wake ambaye siku nyingi nilikuwa natamani kukumbatiana naye, siku hiyo nilimkumbatia sana tu, na mumewe alikuwepo akifurahia kitendo kile na kuniambia ‘Jirani tumeuona mwaka mpya, tupendane zaidi jirani.’ Mangi naye akanikumbatia japo ananidai vitu nilivyokopa dukani kwake, na ana maneno huyo hata njia nilikuwa nimebadili ili nikwepe duka lake, siku ile naye alinikumbatia kwa undugu. Wakati huohuo, wengine wakawa wanatuma ujumbe wa pongezi kwenye simu kwa wake zao, wake maboresho, wake academia, michepuko, michepuko maboresho, michepuko academia, basi raha tupu. Tarehe moja Januari ilikuwa kula na kunywa kufurahia mwaka mpya. Nakumbuka nilipita nyumba tatu na kote nikakuta chakula kingi nikala vizuri na kunywa sana tu, kwa kweli sikumbuki nilirudi vipi nyumbani. Lakini kuanzia Januari mbili ndipo nikaanza kujua huyu mgeni niliyemfurahia kumbe hafai hata kulumangia chai. Furaha yote ilianza kuisha taratibu. Nikiwa bado nimelala chumbani kwangu saa kumi na mbili asubuhi nilikurupishwa na mtu anagonga mlango utadhani kaununua mwenyewe, nikauliza kwa ukali, “Nani jamani?” Nilipofungua mlango, kumbe kweli aliyegonga ule mlango ndiye aliyeununua, alikuwa mama mwenye nyumba. Ile kuufungua nikamkuta katoa macho, mkali utadhani siyo yule tuliyekumbatiana kwa furaha juzi tu. Bila salamu akaanza: “We leo tarehe ngapi?” Nikajibu. “Tarehe mbili.” “Haya kodi yangu iko wapi? Uliniambia utanipa tarehe moja, sitaki utani nipe kodi au hama humu ndani.” Mfukoni sikuwa hata na senti tano, na nilikuwa nimejaribu kukopa, kila niliyemwendea alikuwa analalamika, ‘Januari hii mwanangu sijui pesa imeenda wapi’. Hata yule ambaye sikuwahi kusikia ana mtoto, naye alinijibu, ‘Ndugu yangu Januari hii, nimebanwa watoto wanahitaji ada, madaftari na yunifom sina kitu kabisaa.’ Bila hata kufikiri nikaahidi kwa mama mwenye nyumba kuwa nitajitahidi kumlipa siku hiyo jioni. Unajua mama mwenye nyumba anatisha jamani, akiwa anakudai kodi unakuwa mpole kupindukia. Nilitoa ahadi hata sikujua nitapata wapi fedha ya kodi. Siku ile jioni ilipofika nilikuwa mtaa wa pili najishauri jinsi ya kuingia kwenye chumba changu. Tatizo ni kuwa ikifika Januari wenye nyumba wanapenda sana kukaa karibu na mlango wa mbele wa kuingilia na kusababisha ugumu wa mtu kuingia kwenye chumba chake bila kuonekana. Nilijikongoja mpaka uchochoro wa nyumba ya pili toka kwetu nikawa nasubiri akitoka tu nijitome ndani spidi kwenye chumba changu. Nikabahatisha, alitoka kidogo nikapenya huyoo mpaka kwangu, nikajifungia kimyaaa. Hakuna kuwasha TV wala taa, saa moja tu nikaingia kwenye shuka na kutulia hata sikujigeuza maana kitanda kingelia, mbu utafikiri walijua kuwa sitakiwi kujitingisha acha waanze kunishughulikia. Huko nje nikawa namsikia mama mwenye nyumba anauliza: “Huyu mshenzi hajarudi bado? Ngoja arudi leo atanijua mi nani? Atabeba vitanda vyake usiku huu huu. Katoka kwao Iringa huko akajua anakuja kaa bure huku? Atanijua mi nani leo.” Nikakumbuka simu, nikaitoa na kuitega kwenye vibrashen isije ikalia, si, unajua Mchina alivyo na kelele. Wale niliowatakia heri wakati wa mwaka mpya nao si wakaanza kutuma mesej wanaomba hela na baadhi wanadai zawadi zilizowaahidi. Mpaka sasa sijui ilikuwaje nikajikuta nimelipa kodi ya chumba. Pa kulala ninapo ila kula sasa, daa Januari shikamoo lakini katokomee salama.

0 comments:

Post a Comment

 
Top