Gazeti la The Mail on Sunday la Uingereza limemwaga upupu baada ya kuchambua jinsi biashara ya meno ya tembo na pembe za faru ilivyokithiri nchini.

The Mail on Sunday ambalo ni gazeti dada la The Daily Mail, lilikuwa likitoa utangulizi wa habari kuhusu mkutano ulioitishwa na mwana wa mfalme wa Uingereza, Prince Charles, kujadili viumbe walio hatarini kutoweka, wakiwamo tembo na faru.

Katika mkutano huo Rais Jakaya Kikwete ni miongozi mwa viongozi wa nchi 50 walioalikwa. Hivyo gazeti hilo lilikuwa likiangalia kasi ya mauaji ya tembo nchini huku likidai kuwa Rais Kikwete amefumba macho.

Lakini kabla Uingereza pia taarifa hiyo haijakauka, televisheni ya ITV ya Uingereza imefanya uchunguzi wa biashara hiyo hapa Tanzania, na kuionyesha jinsi inavyofanyika.

Taarifa hiyo imekuwa shubiri kwa Serikali. Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, amelaani vikali gazeti hilo huku Ikulu ikisema ni ya kipuuzi.

Kuna taarifa kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali anajipanga kulishtaki gazeti hilo. Nisingependa kuingilia kesi hiyo inayoandaliwa, lakini nadhani bado kuna chembechembe za ukweli wa habari ile.

Tena ukweli unatokana na Serikali hiyo hiyo inayoruka kimanga. Tatizo tu ni kwamba ukweli siku zote unauma.

Mtu akishaambiwa ukweli, basi hutafuta njia za kujikosha ili aonekane mwema mbele za watu.

Hakuna ubishi kwamba kumekuwa na kasi kubwa ya mauaji ya tembo, nchini kiasi kwamba Serikali yenyewe iliamua kuanzisha Operesheni Tokomeza ambayo hata hivyo ilisitishwa.

Kwa mfano katika pori la akiba la Selous peke yake, tangu mwaka 1976 tembo wamepungua kutoka 110,000 kubakia 13,000. Ina maana kwamba tembo 100,000 wameshauawa.

Kwa mujibu wa mhifadhi mkuu wa pori hilo, Benson Kibonde, mwaka 1989 tembo walipungua na kufikia 30,000. Ndipo juhudi za kuhifadhi ikiwemo operesheni ya uhai, zilirejesha matumaini ambapo mwaka 1996 walifikia 70,000.

Lakini tatizo hilo limezidi hivi karibuni ambapo mwaka 2009, ndiyo kilikuwa kilele cha mauaji hadi idadi ya tembo imefikia 13.5 waliopo hadi sasa. Hii ni taarifa ya Serikali.

Takwimu nyingine za Serikali zinaonyesha kuwa, mwaka 2010 jumla ya tembo 10,000 waliuawa Tanzania peke yake. Hii ni sawa na tembo 37 kila siku.

Hali ikawa mbaya zaidi mwaka 2012 ambapo jumla ya tembo 23,000, waliuawa sawa na wastani wa tembo 63 kila siku.

Kutokana na kasi hii ya ujangili, inakadiriwa kuwa ifikapo mwaka 2017/2018, Tanzania haitakuwa na tembo hata mmoja. Kwa takwimu za hivi karibuni, Tanzania ina tembo kati ya 150,000 na 170,000.

Waziri Nyalandu mwenyewe alisema hivi karibuni kuwa, baada ya kusitishwa kwa Operesheni Tokomeza, takribani tembo 60 waliuawa ndani ya mwezi mmoja.

Hivi inawezekanaje tembo wote hao kuuawa tu na majambazi wa kawaida kama siyo kuwa na uhusiano na watendaji serikalini? Au basi tuseme kwamba Idara ya Wanyamapori imekwenda likizo. Haiwezekani.

Ni kweli inawezekana kukawa na kasoro za hapa na pale za kiuandishi katika gazeti hilo, lakini ukweli uko wazi kwamba , tembo wanakwisha usiku na mchana na Rais Kikwete ambaye ndiye mkuu wa kaya yuko madarakani. Nini kimefanyika?

Ni kweli pia kwamba Serikali imefanya jitihada zake, kwa mfano wanasema wamekamata watuhumiwa 320. Je, watuhumiwa hawa wanakamatwa wakati gani? Au ni wale wanaokamatwa wakati mzigo umeshafikishwa bandarini? Mara wamekamata shehena za meno, kwa nini wasizuie mauaji, wanasubiri hadi meno yafike bandarini?

Nasema hivyo kwa sababu biashara hiyo ni mnyororo mrefu. Kuna wakubwa wanaomiliki ‘mzigo’ na kuna wengine wanatumwa tu kutekeleza.

Inawezekana hao 320 ni ‘vidagaa’ tu vinavyotumwa kutekeleza, lakini wahusika wakuu hawakamatwi.

Mbona majina yalishatajwa hadi bungeni na kwenye mikutano ya hadhara, na bado wahusika ‘wanadunda’ tu?

Hatuombei lakini kama wanayotabiri wataalamu ni kweli, basi imebaki miaka mitatu tu tembo waishe wote.Wakiisha viongozi wa Serikali watakuja na takwimu na picha za tembo kutusimulia. Watasema Rais Kikwete amefanya kazi kubwa, tumekamata maelfu ya majangili, tumekamata meno ya tembo na msururu wa maneno, lakini tembo hawapo tena. Itakuwa ni historia tu kwa vizazi vijavyo.

Kinachoonekana hapa ni kutaka kuficha ukweli kwamba tembo wanauawa, na kusisitiza kuwa Serikali imechukua hatua kubwa.

Badala ya Serikali kuanza kulaumu gazeti la Mail on Sunday au ITV ya Uingereza, watumie taarifa hizi kama changamoto ya kuongeza juhudi.

0754 897 287

 

 

0 comments:

Post a Comment

 
Top