
Rehema Michael akiwa kitandani kwenye Hospitali ya Mkoa wa Rukwa alipolazwa kwa matibabu baada ya kunusurika kifo wakati wa kujifungua. Picha na Fredy Azzah
Huu ni ukatili ambao wanafanyiwa
wajawazito si kule Rukwa pekee, bali nchini kwa jumla
Sumbawanga. Siyo jambo geni kusikia wanawake wakiwalalamikia
wauguzi ama kwa kuwapiga au kuwatukana wakati wa kujifungua.
Hata hivyo, matukio ya mama
kupoteza maisha ama mtoto aliye tumboni kufariki kwa ajili ya vitendo hivyo
vimekuwepo, lakini siyo kwa wingi.
Rehema Michael (18), mkazi wa
Kijiji cha Tentula Sumbawanga Vijijini ni mmoja kati ya waliokutana na chungu
ya kutukanwa na kupigwa na muuguzi wakati wa kujifungua.
Rehema ambaye ilikuwa ni mimba
yake ya kwanza, amepoteza mtoto na yeye mwenyewe kunusurika kifo kutokana na
hali yake.
Rehema akiwa mchovu anasimulia
kwa uchungu kisa chote tangu alipopata uchungu wa kujifungua mpaka
alipofikishwa hospitali.
“Nilisikia uchungu siku ya
Jumatatu, nikamwambia mama mkwe ,tukaondoka naye kwenda kwenye
zahanati ya pale kijijini Tentula.
“Tulipofika hatukumkuta muuguzi
wa zamu na daktari tuliyemkuta hakuwa na funguo ya chumba kwa hiyo akatubeba
kwenye pikipiki mpaka kwenye kituo cha afya cha Ikozi.
“Nilipofika hapo nikaingizwa
kwenye chumba cha kuzalia, nikawa najitahidi kusukuma mtoto, nesi akanipiga ili
nisukume mtoto, nilijitahidi kusukuma mtoto mpaka kichwa kikaanza kutoka
hadi kufikia kidevu, lakini kwa kuwa nilivyokuwa napigwa nikaishiwa nguvu.
Muuguzi akaniambia niache uvivu,
“Sukuma, acha ujinga, nani alikutuma?” akaendelea hivyohivyo, kwa kweli
nilikuwa nasikia maumivu sana.
Nilipoishiwa nguvu aliendelea
kunipiga ili nisukume mtoto, lakini nikashindwa ndiyo ikabidi gari liitwe ili
niletwe hapa kwenye hospitali ya mkoa.
Nilifika huko mtoto akining’inia, hivyo mpaka ninafika
hapo, nilipotoka huko mpaka mtoto alikuwa hai, lakini mpaka nafikikishwa hapo,
nikaambiwa mtoto ameshakufa.
Nilipofika hapo nesi akanichoma
sindano na kumtoa mtoto kirahisi, lakini ndiyo akawa ameshakufa, na mimi
nilikuwa nimechoka.
Kilichonifanya niishiwe nguvu ni
kwa sababu ya kupigwa, kama mtu anajitahidi kusukuma mtoto mimi sioni ni kwa
nini apigwe.
Gari kutoka katika eneo hilo
mpaka Sumbawanga mjini ni mwendo wa kama saa mbili.”
Anasema alifika hospitalini hapo
akiwa amechoka, madaktari wakamchoma sindano na kumtoa mtoto huku tayari akiwa
ameshafariki.
Wataalamu wa afya kwa upande wao
wanasema kuwa, mimba ya kwanza ni moja ya kiashiria cha hatari kwa mama
mjamzito hivyo wauguzi hutakiwa kumshauri mama huyo kuhakikisha
anajifungulia kwenye hospitali kubwa.
Rehema anasema kuwa, licha ya kwamba alikuwa
anahudhuria kliniki siku zote hakuwahi kuambiwa kwamba anatakiwa kujifungulia
kwenye hospitali kubwa.
Naye Grace Kamungwi (27), kutoka
Mtowisa, pia katika Manispaa ya Sumbawaga alipoteza mtoto naye kunusurika
kifo kutokana na kile kinachoonekana kuwa ni uzembe wa wauguzi.
Akisimulia kilichomkuta, anasema:
“Nilipata uchungu, Jumatatu nikaenda Kituo cha Afya cha Mtowisa, nilipofika
huko nilijitahidi sana kusukuma mtoto atoke, lakini nikashindwa.
Nikaletwa hapa hospitali ya mkoa,
baada ya kunifanyia upasuaji wakaniambia mtoto tayari amefariki. Hii ni mimba
yangu ya kwanza na ya pili nilijifungua kawaida kabisa bila kupata tatizo
lolote.
Mtoto wangu wa kwanza ana miaka
mitano, wa pili nilijifungua mwaka 2012, akafariki.
Dk Francis Mashi aliyekuwa
akimuhudumia Grace katika hospitali hiyo ya Mkoa wa Rukwa anasema kuwa mama
huyo alipata uchungu mkingamo na ilikuwa lazima afanyiwe upasuaji.
“Huyu alikuwa kwenye uchungu kwa muda mrefu, mtoto
alikuwa amekaa vibaya na asingeweza kujifungua kwa njia za kawaida. Ukiwa na
uchungu mkingamo, huwezi kujifungua kwa njia ya kawaida na inatakiwa uambiwe
mapema ili ujifungulie kwenye hospitali inayoweza kufanya upasuaji.”
Kituo cha Afya Mtowisha
kinatakiwa kifanye upasuaji lakini kuna wakati huwa
wanashindwa.
Anasema Dk Mashi kuwa mtoto aliyekaa vibaya,
ilitakiwa alipokuwa akihudhuria kiliniki suala hilo litambuliwe na atakiwe
kwenda kujifungulia kwenye hospitali kubwa inayoweza kufanya upasuaji.
Itaendelea
0 comments:
Post a Comment