
Mgombea ubunge Jimbo la Kalenga kwa tiketi ya CCM, Godfrey Mgimwa akibebwa na wananchi wa Kijiji cha Ilala Simba baada ya kuwasili kijijini hapo kabla ya kufanya mkutano wa kampeni za uchaguzi mdogo wa jimbo hilo mkoani Iringa, jana. Picha na Edwin Mjwahuzi.
Iringa. Chama cha Mapinduzi (CCM), kimeanza kutumia mbinu mpya ya kuwaomba wananchi wa Jimbo la Kelanga kwa makada wake kupiga magoti.
Mwenyekiti wa CCM wilayani hapa, Delfina Mtavilalo na Naibu Mstahiki Meya wa Manispaa,Gervas Ndaki kwa nyakati tofauti kwenye maeneo tofauti wameonekana wakiwaomba kura wananchi wa Kijiji cha Kibebe Kata ya Mlanda kwa kupiga magoti.
Mtavilalo alisema, CCM inaomba ridhaa ya wananchi hao kumchagua Godfrey Mgimwa ili afanye kazi ya kuendeleza miradi na mipango yote iliyoachwa na aliyekuwa Mbunge wa Jimbo hilo, Dk William Mgimwa.
Aliongeza kuwa miradi na mipango ya maendeleo iliyopo imeanzishwa na CCM na ni chama hicho pekee ndicho chenye uwezo wa kuendeleza ili kuwapelekea wananchi maendeleo ya kweli na haraka.
Ndaki alisema, anayeweza kutatua kero za wananchi ni Godfrey Mgimwa kwa kuwa ana wabunge wengi wanaoweza kumuunga mkono katika jitihada za kufanikisha maendeleo.
Alisema pia chama alichopitia Godfrey kinaunda,Serikali hivyo ni rahisi kumsikiliza wakati wa kutatua changamoto zinazowakabili wananchi wa Jimbo la Kalenga.
Naye Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa, Jesca Msambatavangu alisema, umefika wakati vijana wakabadilika na kuanza kukiunga mkono Chama Cha Mapinduzi badala ya kuendelea kupotea kwa kuwaamini wapinzani.
“Vijana badilikeni, mtukubali na mtuamini na kutuunga mkono badala ya kuendelea kupoteza muda kwa kuwaunga mkono wapinzani”, alisema.
Naye Naibu Katibu Mkuu wa CCM ambaye pia ni Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba alisema, mtu anayejua muda uliobaki kufikia uchaguzi mkuu na jinsi miradi ya maendeleo inavyotekelezwa ataichagua CCM na mgombea wake.
“Kuna vijiji vinataka minara ya simu, madarasa na zahanati, ili vipatikane vitu hivyo kwa haraka,havina budi kuchagua CCM na mgombea wake. Kuchagua CCM na kwenda mbele hatua nyingi katika kujiletea maendeleo”, alisema.
Godfrey Mgimwa alisema, ameweza kujitoa na taaluma yake kwa ajili ya kuwatumia wananchi wa Jimbo la Kalenga kama alivyokuwa akifanya baba yake hivyo wamchague ili wapate maendeleo ya haraka.
src
mwananchi
src
mwananchi
0 comments:
Post a Comment