Dodoma. Mjumbe wa Bunge Maalumu la Katiba,
John Chiligati amesema mabadiliko ya Katiba yatakayofuta haki ya mbunge
kuwa Waziri, yataongeza uwajibikaji kwa umma.
Chiligati aliwahi kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya
Ndani (2000-2005), Waziri wa Mambo ya Ndani (2006), Waziri wa Kazi,
Ajira na Maendeleo ya Vijana (2006-2008 na Waziri wa Ardhi mwaka 2008.
“Mhimili wa Bunge ufanye kazi za Bunge na ule wa
Serikali ufanye kazi za Serikali na Mahakama ifanye kazi zake. Siyo mtu
mmoja kutumikia mihimili zaidi ya mmoja,” alisema.
Kwa mujibu wa Chiligati, kama mapendekezo hayo
yatapitishwa na wajumbe wa Bunge la Katiba ina maana kuwa Mbunge hawezi
tena kuwa Waziri, Mkuu wa Mkoa au Mkuu wa Wilaya.
“Sasa hivi tuna wabunge ambao ni wakuu wa mikoa
au mkuu wa wilaya na mbunge mwingine ni waziri. Tukipitisha hili kwenye
Katiba ni kwamba sasa mbunge atabaki kuwa wa kuwatumikia wapigakura wake basi,” alisema.
Chiligati alisema ingawa pendekezo hilo
linaonekana kuwa ni jipya miongoni mwa Watanzania, mgawanyo huo wa
madaraka upo pia katika nchi za Kenya na Rwanda na kwamba umeongeza
uwajibikaji kwa umma.
“Unajua unapokuwa waziri halafu unakuwa mbunge
jambo likija pale bungeni kwa hali ya kibinadamu, unaona haya kumbana
unasema ‘aah, huyu ni mwenzetu’,” alisema Chiligati.
“Lakini akishakuwa huyo mnayembana siyo mbunge
mwenzenu, kibano kinakuwa kikali na ni kwa manufaa ya umma. Binafsi
sioni kama kuna tatizo japo mazoea nayo yana matatizo yake,” alisema.
Chiligati alisema mapendekezo hayo yanaelekeza wabunge wa Bunge la
Jamhuri ya Muungano na mawaziri kukutana kwenye Kamati za Kudumu za
Bunge.
0 comments:
Post a Comment