Kwa Waziri wa Mikiki na Makeke,
Uzitoni Street,
Bongo.
We Mpenzi wangu Frank,Uzitoni Street,
Bongo.
JAMANIEE, nikiwa mbali na wewe namna hii, unategemea nitajibu nini kama unaniuliza nina hali gani? Hali yangu ni nzuri kimwili.
Naamka, nafanya kazi, nalala vizuri lakini bila kuwa karibu na wewe, moyo una mpasuko mkali. Sina raha mwenzio, njoo unitibu basi angalau kidogo, nipooze, nikumbushe kwamba duniani kuna watu wasio na kichaa, kuna watu wenye akili timamu, maana nikiangalia magazeti na runinga najawa na wasiwasi.
Kweli mpenzi wangu. Iwapo watu ambao wanatakiwa kuwa mfano bora wanafanya wanavyofanya, sisi akina hohehahe tutafanya nini? Yaani sielewi kabisa. Watu wamekaa karibu mwezi kutengeneza kanuni kwa posho isiyohesabika, kisha siku ya kwanza wanataka kuvunja kanuni hizohizo. Ni akili kweli mpenzi?
Na wakati huohuo wanaendelea na unzige wao wa kumaliza chakula chote shambani. Ingekuwa mimi ningevunjilia mbali hili bangi la kutibua kama fyatu wako anavyoelezea maana wataendelea kukaa siku, wiki, miezi, lakini sidhani kama katiba tunayotaka sisi wananchi itapatikana. Kweli kabisa mpenzi.
Basi kutokana na zogo hilo, Bosi alirudi nyumbani mara moja na sisi tulikuwa na mjadala wa kanuni humuhumu ndani. Tena alianzisha Bosi mwenyewe ingawa binti yake alitia mafuta kwenye moto. Kisa, wauza mahaba huko.
‘Yaani siamini. Mji umefurika wadada hawa kuliko hata sisi wajumbe, utadhani kuna bunge mbadala.’
BB akacheka.
‘Bora ingekuwepo. Nadhani hawa dada wanaelewa hali halisi kuliko hata nyinyi mnaopigania maslahi ya vyama vyenu tu.’
‘Ohoo, Ernesta Guevara ameanza. Kweli unataka kusema kwamba hawa dada wanajua kuliko sisi ambao tumesoma, na tunahangaika kila siku kuleta maendeleo nchini.’
‘Kwani kusoma ni kuelewa baba? Mimi sidhani kwamba mtu yeyote ambaye amepitia hali halisi ya hawa madada ataweza kudai posho ya shilingi laki tatu, sembuse laki saba kwa siku.’
‘Mbona wao wanadai laki moja kwa kulala tu hadi asubuhi.’
Hapo Mama Bosi akashtuka.
‘He. Unajuaje? Una ….’
Bosi alipooza mambo harakaharaka.
‘Hapana mke wangu, wewe husomi magazeti? Imeandikwa humu.’
BB akaendelea.
‘Kwa hiyo maana yake ni kwamba waheshimiwa wanahitaji posho kubwa zaidi kwa sababu ya kupanda kwa gharama za huduma kama hizo.’
Bosi alimaliza hasira yake kwa mwanaye.
‘Acha upumbavu na uhuni wako. Nani kasema sisi sote tunatafuta huduma hizo?’
‘Lakini wengi wanatafuta. Vinginevyo wasichana wengi wasingehamia kule kwa wakati huu.’
‘Kwani tuliopo pale ni wabunge tu. Na madereva wetu, na wafanyakazi wengine.’
‘Lakini gazeti lilisema mashangingi nao wanaonekana kwenye hii mitaa maarufu.’
‘Mwanangu kweli huna adabu. Unataka kumhusisha baba yako na mambo hayo?’
‘Hapana baba, sikusemi wewe. Nasema tu kwa ujumla hawa wadada ni wajasiriamali, wanafuata soko lilipo. Wala hawaombi serikali iwatafutie soko, wanajua liko wapi.’
Nilifikiri Bosi atalipuka tena na kweli alilipuka, lakini kwa kicheko tu, si kwa hasira.
‘Duh, yaani huu ndio mfano bora wa ujasiriamali? Mbona hatari?’
MB akaingilia kati.
‘Mimi sioni kwamba haya mazungumzo yana faida yoyote. Wewe unaongea na mwanao kuhusu mambo ya ukahaba. Ama kweli dunia imekwisha.’
Baada ya hapa watu walikaa kimya kwa muda lakini niliona wazi kwamba anataka kuchokoza. Na mwisho alishindwa kuvumilia.
‘Unajua baba, mimi ningetaka kubadilisha hiyo rasimu ya katiba, ningeongea na hao wadada. Tena ningewaita kwenye semina mchana, baada ya wao kulala kulingana na shifti zao za usiku. Ningewaeleza yote ninayotaka kubadilisha kisha kuwaambia waseme kwa wateja wao.’
MB alikunja uso lakini Bosi alicheka tena.
‘We mwanangu, mara nyingine najiuliza hii akili yako ya ovyoovyo unaipata wapi? Kwani watu wanaenda kwa hawa wadada kupewa semina za kisiasa?’
‘Nasikia ndipo hapo mwanamume anakuwa dhaifu kabisa. Anaweza kuahidi chochote.’
‘Kwa hiyo unataka wapiganie haki zao kwa ajili hiyo?’
‘Si wazo baya. Wao wanatoa huduma kila siku kisha wanapigwa na kuswekwa ndani na haohao waliowahudumia, kwa amri ya haohao waliowahudumia. Bora watambulike kama wafanyakazi wa mahaba tu. Na kukatwa kodi kwenye malipo yao. Wapewe hizi mashine za Mamlaka ya Mapato.’
Bosi alizidi kucheka.
‘Mmmh! Wewe unatafuta matatizo kweli wewe. Watu wa dini zote wataamka vikali sana.’
‘Kwani na wao hawapokei hizi huduma?’
MB alilipuka tena.
‘Funga mdomo wako mchafu wewe. Unafikiri watu wote wameharibika?’
‘Mimi sisemi watu wote mama. Nasema tu kwamba wanaowalaani wengine ni haohao wanaowafuata usiku. Maneno ya laana mchana, vitendo vya laana usiku.’
‘Na bora utambue kwamba ni laana.’
‘Ndiyo mama. Lakini ukiangalia katika historia, hata katika biblia, watu kama hawa wamekuwa na nguvu sana. Ndiyo maana nasema badala ya kukaa pale kwenye viwanja vya bunge siku nzima na kujaribu kuwashawishi wasioshawishika kutokana na msimamo wa chama chao, bora upitie kwa hawa. Nadhani ushawishi utakuwa na nguvu zaidi.’
Bosi akaingilia tena.
‘Ni kweli mwanangu. Kama kawaida umetia chumvi hadi pilipili kichaa lakini nao wana mawazo yao. Mmoja alikuwa anajaribu kunielezea jinsi vijana walivyosahaulika na rasimu …’
Bosi hakuweza kuendelea maana alikuta sahani inamwelekea juu kwa juu.
‘Na huyu hayawani ulikuwa unaongea naye wapi?’
Bosi aliweza kukwepa sahani ambayo ilitua na kuvunjika nyuma yake lakini sasa ikabidi ajihami haraka sana. Na kama kawaida ya madume (sijui wewe mpenzi), alijihami kwa kushambulia.
‘Unafanya nini? Yaani kutaja nimeongea naye maana yake nimefanya uhuni! Miaka yote hii ndiyo leo natangaza uhuni!’
Lakini mke wake hakuwa tayari kusikiliza. Alikuwa ameshaamka na kutaka kumvaa mume wake.
‘Leo umejileta mwenyewe. Utanieleza huyu hayawani ulikuwa unaongea naye wapi.’
‘Bosi alijaribu kushika mikono yake.
‘Kwani hatukutani kwenye baa. Wakati tunakula nyama choma ….’
‘Usinidanganye. Mpaka apate wasaa wa kuelezea mafungu ya katiba. Utanikoma leo.’
Basi mpenzi ikawa kukurukakara hadi hata BB aliamua kwenda kujificha, sembuse Hidaya wako. Hatimaye Bosi alimfokea mke wake kwamba hii fujo mbele ya watoto haina maana. Wakapanda juu na sijui mambo yaliishaje ingawa MB alidai kesho yake kwamba amejigonga kwenye mlango wa bafuni, na Bosi mwenyewe akawa anachechemea.
Hakuna aliyekuwa tayari kumwangalia mtoto wao usoni na mimi nilijitahidi kuangalia chini tu wakati naleta supu zao maana mfanyakazi hatakiwi kuona udhaifu wa mabosi, wanaweza kumwondoa kwa kuficha aibu zao.
Kwa hiyo mimi kimya tu mpenzi, ingawa hata wakinifukuza tu, maana yake ni kwamba nitaachana na uMirembe huo na kurudi kwako.
Lakini nilipenda wazo la BB. Hawa dada zetu wangepewa semina kidogo, naamini katiba ingebadilika kweli na labda hata sisi vijana tungeacha kubaguliwa hata na katiba. Au vijana tufanye nini?
Akupendaye daima kijana mwenzangu
Hidaya.
src
raia mwema
0 comments:
Post a Comment