Mwenyekiti wa CCM, Jakaya Mrisho Kikwete
CHAMA cha Mapinduzi kinang’ang’ania muundo wa serikali mbili kwa hofu ya kuwa serikali tatu hazitohakikisha usalama imara na endelevu wa pande zote mbili za Jamhuri ya Muungano, imefahamika.
Tangu kuanza kwa mchakato wa kuandika Katiba mpya, CCM kimeweka msimamo mmoja kwa wanachama na viongozi wake, wa kuendelea kutetea sera yake ya kuwa na muundo wa Muungano wenye serikali mbili, kiasi cha kuwagharimu baadhi ya wanachama na watendaji wake wanaokwenda kinyume na msimamo huo.
Mansour Yusuf Himid, aliyekuwa kada wa CCM na Mwakilishi wa Jimbo la Kiembe Samaki, ni miongoni mwa mifano ya wanachama na watendaji wa chama hicho, ambao misimamo yao inayokwenda kinyume cha sera hiyo ya CCM ya kuwa na muundo wa Muungano wenye serikali mbili, iliwagharimu kwa kuvuliwa uanachama wake.
Taarifa kutoka vyanzo kadhaa vya habari ndani ya CCM, ambazo zimethibitishwa na baadhi ya viongozi wakuu waandamizi ndani ya chama hicho, zinasema kiini kikubwa kilichowasukuma waasisi wa taifa hili la Tanzania, Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume, ilikuwa ni usalama dhidi ya maadui wa aina yoyote kutoka nje kwa mataifa haya mawili na si suala la undugu wa kihistoria kama inavyoimbwa siku zote na baadhi ya wanasiasa.
Muungano wa mataifa mawili huru ya Tanganyika na Zanzibar ulifanyika Aprili 26, 1964, ikiwa ni takriban miezi mitatu tu baada ya kutokea Mapinduzi ya Zanzibar Januari 12, 1964, na ikiwa pia ni takriban miaka mitatu baada ya Uhuru wa Tanganyika.
Mara kadhaa, imekuwa ikielezwa na baadhi ya wanasiasa wa pande zote mbili hizo za Muungano kwamba chimbuko hasa la Muungano huo ni historia ya muda mrefu ya muingiliano wa wananchi wa nchi hizo uliowafanya kuishi kama ndugu hata kabla ya nchi hizi kuwa chini ya wakoloni.
Hata hivyo, suala hilo la undugu wa wananchi wa nchi hizo, limeelezwa na baadhi ya viongozi waandamizi wa CCM kwamba ni lugha ya kisiasa tu, lakini ukweli halisi ilikuwa ni kuimarisha usalama dhidi ya maadui wa nje.
“Neno undugu kati ya nchi mbili hizi, linatumiwa kisiasa tu. Chimbuko hasa la Muungano wetu huu ni usalama wa uhakika kwa pande zote mbili hizi. Nje ya Muungano, Zanzibar haiwezi kuwa salama na Zanzibar isipokuwa salama, basi na huku Bara hakuwezi kuwa salama,” anasema kiongozi mmoja mwandamizi wa CCM na kuongeza:
“Kama mnakumbuka, Mwalimu aliwahi kutamka kwamba kama angelikuwa na uwezo wa kuvisukumia mbali visiwa vya Zanzibar, angefanya hivyo na Muungano huu ukafa, lakini kwa kuwa hana uwezo huo, basi Muungano huu lazima udumishwe kwa kila jia.
“Kwa hiyo, wakati sisi (CCM) tunatetea muundo wa Muungano wenye serikali mbili kwa ajili ya usalama wa taifa letu hili na watu wake, wenzetu wanataka serikali tatu ili tu waweze kupata fursa ya kuingia Ikulu, lakini hawatuelezi ni kwa jinsi gani watahakikisha usalama wetu huu unakuwa endelevu.
“Wanapita wakisema wazi kwenye majukwaa yao ya kisiasa kwamba wanataka serikali tatu kwa sababu serikali hizo zikija tu, CHADEMA wataingia Ikulu ya Tanganyika na CUF watashika Ikulu ya Zanzibar, lakini hawazungumzii kabisa suala la usalama.
“Na kwa sababu hiyo hiyo, wenzetu kule Zanzibar (wana CCM-Zanzibar), wametwambia wazi wazi kwamba Katiba mpya ikija na serikali tatu, wao watafufua ASP yao ili waweze kuwashikisha adabu ma-CUF…hali hii ikitokea, tutakuwa tumeirejesha Zanzibar enzi zile za siasa za ASP na ZPP.”
Kiongozi mmoja mwandamizi wa CCM, ameliambia Raia Mwema kwamba sehemu kubwa ya Wazanzibari ni waumini wa dhati wa Mapinduzi ya Zanzibar na Muungano, hawako tayari kuona Zanzibar ikitengwa ndani ya Muungano, kwani kufanya hivyo, kutairejesha nchi hiyo nyuma kama ilivyokuwa miaka ya mwishoni mwa 1950 na mwanzoni mwa miaka ya 1960. 
Kwa mujibu wa kiongozi huyo, kundi hilo la Wazanzibari waumini wa Mapinduzi na Muungano, kwa sasa wanasubiri tu Katiba mpya itamke muundo wa Muungano wenye serikali tatu, nao watangaze kurejeshwa kwa Afro-Shiraz (ASP) ili kukabiliana na chama kikuu cha upinzani Visiwani humo, Chama cha Wananchi (CUF) kama ilivyokuwa kabla ya Mapinduzi.
Mbali na kiongozi huyo mwandamizi wa CCM kuweka wazi suala hilo la kwanini CCM imeng’ang’ania serikali mbili tofauti na mapendekezo ya Rasimu ya Pili ya Katiba yanayotaka muundo wa Muungano wenye serikali tatu, kiongozi mwingine amezungumzia dhana inayojengwa ndani na nje ya Bunge la Katiba kwamba CCM pekee ndiyo yenye msimamo ndani ya Bunge hilo, na pia kwamba CCM imeandaa rasimu yake mbadala.
“Kuna dhana inajengwa ndani na nje ya Bunge la Katiba ili kuwaaminisha wananchi kwamba CCM inawashinikiza wabunge wake kuwa na msimamo wa serikali mbili, na lakini pia kwamba CCM imeandaa rasimu yake mbadala, nasema sawa tumefanya hivyo, lakini ni chama gani cha siasa ambacho hakina msimamo wake kinaoutetea na kuusimamia ndani ya Bunge?” anahoji kiongozi huyo.
Aliongeza: “Wabunge na viongozi wa CHADEMA, CUF na NCCR-Mageuzi wanakutana kila mara na kila siku kupanga mikakati kuhakikisha serikali tatu zinakuwapo, kwanini wao hawaambiwi wala kuandikwa kwamba wameng’ang’ania serikali tatu?
“Kama unafuatilia hotuba za Rais Jakaya Kikwete, kuna siku moja alisema moja ya sababu iliyomfanya amteue Dk. Sengondo Mvungi (marehemu) kuwa mmoja wa makamishina wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, ni kwamba waliwahi kukutana Bagamoyo, kabla hata ya mchakato huu wa Katiba mpya kuanza, akiwa amejifungia hotelini akiandika Katiba ya Tanzania, ambayo chama chake kinataka iwe…mmeuliza rasimu hiyo iko wapi?
“Je; rasimu hiyo ya NCCR-Mageuzi haikuwasilishwa kwenye Tume ya Jaji Warioba? Haya; mmsahau pia kwamba hata kabla ya Tume ya Jaji Warioba kuanza kusikiliza maoni ya makundi yanayofanana, CHADEMA walimpelekea rasimu yao lakini akakataa kuipokea, akawambia wasubiri hadi utakapofika wakati wa kuchukua maoni ya makundi yanayofanana?
“Je; ulipofika muda, CHADEMA hawakupeleka rasimu yao kwa Warioba? Hawakubaki na nakala za rasimu hiyo? Kwa nini vyombo vya habari, haviandiki kuhusu rasimu hizi mbadala za vyama hivi, lakini vinaandika rasimu ya CCM tu?
Tayari Jaji Warioba amewasilisha rasmi bungeni rasimu ya Pili ya Katiba mpya ili sasa ianze kujadiliwa na kupitishwa na Bunge hilo, ambalo pia linatarajiwa kuzinduliwa rasmi na Rais Jakaya Kikwete leo, Jumatano, kabla ya Katiba hiyo kurudi tena kwa wananchi kwa ajili ya kupiga kura ya kuikubali au la

src
raia mwema
Mayage S. Mayage
 

0 comments:

Post a Comment

 
Top