Katika kutambua ukweli kuhusu lugha kama chombo muhimu cha kuunda fikra miongoni mwa wanajamii, lugha ya taifa ilitumika kupiga vita ukabila.
Zamani mataifa mengi ya Afrika yalikuwa yakitumia lugha za asili (makabila) sambamba na lugha za kikoloni, mfano Kifaransa, Kiingereza na Kireno.
Mtihani kwa wapigania uhuru ukawa ni juu ya lugha gani hasa itumike kama lugha rasmi ya mataifa yao.
Tofauti na mataifa mengine ya Afrika, Tanzania tulikuwa na lugha yetu adhimu ya kiasili ambayo haikuwa na mfungamano na kabila lolote katika nchi yetu.
Ni kwa sababu hizi ndiyo maana waasisi wa taifa letu kwa busara na hekima wakaamua kuifanya lugha hii kuwa lugha ya taifa na ya kufundishia elimu ya awali, msingi, mafunzo ya cheti cha elimu ya ualimu na elimu ya watu wazima.
Sambamba na Kiswahili, Kiingereza kikapitishwa kuwa lugha rasmi ya shughuli zote za kiserikali na kufundishia kwa ngazi ya elimu ya sekondari na vyuo vikuu vyote nchini.
Matumizi ya Kiingereza serikalini na katika elimu ya juu nchini yalichangiwa na uchache wa wataalamu wazalendo, hivyo kulazimika kutumia wataalamu wengi wa kigeni.
Lakini kwa utashi wa viongozi wetu wa Serikali ya Awamu ya Kwanza, juhudi na mipango madhubuti ikawekwa ili kuikuza na kuistawisha lugha ya Kiswahili ndipo taasisi mbalimbali kama vile BAKITA, UKUTA na Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (TUKI hivi sasa TATAKI) zilianzishwa ili kulifikia lengo hilo.
Na hivi sasa ukweli unadhihirika kuwa Kiswahili ni lugha inayojitosheleza kimisamiati na imeendelea kukua na kukubalika kimataifa.
Hili linathibitishwa na namna vyuo vikuu mbalimbali duniani vimekuwa vikifanya jitihada za kufundisha lugha hii.
Kiswahili kinafundishwa katika vyuo vikuu kama Havard, Yale, Stanford, Princeton, Chuo Kikuu cha Pennsylvania na vinginenyo.
Inakadiriwa nchini Marekani peke yake kuna taasisi karibu 100 zinazojihusisha na ufundishaji wa Kiswahili. Pia vituo mbalimbali vya redio duniani vinarusha matangazo yake kwa Kiswahili kupitia idhaa za Kiswahili za BBC, DW, RFI na VOA.
Hadi sasa ukweli uko wazi hususan kwa Watanzania kuwa Kiswahili si lugha muhimu kwetu bali ni lulu ambayo hatuna budi kuikuza, kuiendeleza, kuilinda, kuisambaza na kuipigania kwa hali na mali katika nyakati hizi ambazo kila taifa hususan mataifa tajiri yakiendelea kuzisambaza lugha zao.
Kwa Watanzania, Kiswahili kina umuhimu mkubwa sana si tu kwa mwananchi mmoja mmoja bali hata kwa taifa kwa ujumla.
Kiswahili ni silaha ya ukombozi wa kijamii, katika uwezo huu tu ndipo mtu anakuwa na uwezo wa kutoa mchango wake katika ujenzi wa taifa lake.
Mwanazuoni nguli wa Afrika, Profesa Ngungi wa Thiong’o, akizungumza katika Mhadhara wa Kitaaluma katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kabla ya chuo hicho kumtunuku shahada ya heshima ya udaktari katika fasihi mwishoni mwa mwaka 2013, alisema: “Lugha ni silaha ya kivita baina ya mtumwa na mtawala; ni silaha ya kutamalaki kama ilivyo upanga, lakini Waafrika wengi kwa kulowea upumbavu wa usasa, tumeziweka lugha zetu za asili kwenye uduni na kutukuza za kigeni kana kwamba ni kinyaa kuzungumza za kwetu, huku ni kumezwa na hakuna wa kukwepa kwamba tuko mateka.
“Kuna wasomi wajinga, wanaodhani kuzungumza lugha zao mfano Kiswahili ni kujidhalilisha, hivi ni nani alikufa kwa kuzungumza Kiswahili na nani akahesabiwa haki ya kuishi kwa kuzungumza Kiingereza?
Si viongozi wa serikali za Afrika pekee waliotekwa na fikra za kigeni, bali hata wasomi wa karne ya sasa ni majemedari wanaopigana vita upande wa adui.
Majemedari hao tena wakiwa na majina ya Kizungu na kuweka kando ya asili.
“Wanaona fahari kutumia lugha za kigeni kama silaha ya maendeleo, bila kujua kuwa wanaangamizwa wao na vizazi vyao na kuendelea kujenga matabaka makubwa.”
Anasema Tanzania ndiyo nchi pekee inayotumia Kiswahili kama lugha yake ya taifa. Hivyo kwa kuikuza na kuiboresha kwa kuitumia katika shughuli zote za kiserikali na kielimu itakuwa njia nzuri ya kuendelea kulitangaza taifa letu kimataifa.
Ukweli ni kwamba Kiingereza kinachangia kudorora kwa elimu nchini. Kwa shule chache nilizopita na kufundisha katika mikoa ya Lindi, Dar es Salaam, Iringa, Mbeya na Kigoma kilichopo kinatisha.
Si zaidi ya asilimia kumi ya wanafunzi darasani utakuta ndio wana uwezo wa kuandika sentensi ya Kiingereza iliyonyooka na yenye maana. Katika hali kama hii inakuwa kazi kufanya vema katika masomo yao, wanaishia kusoma kwa kukariri na wakati mwingine hata wasiweze kuvioanisha vitu wanavyojifunza na mazingira yao halisi ya kimaisha.
Mwanafunzi anayejifunza elimu ya awali (mwaka mmoja au miwili) na elimu ya msingi (miaka saba) kwa Kiswahili, kumfundisha kwa Kiingereza tupu katika elimu ya sekondari ni kumpa mtihani wa kuanza kujifunza lugha mpya na kuishia kukariri bila kuelewa kwa mapana yale anayojifunza darasani.
Ni katika mfumo huu ndio tunazalisha mawaziri wa elimu wasioweza kujieleza kwa Kiingereza, madaktari wanaofanya upasuaji na kuacha mikasi tumboni mwa wagonjwa, madaktari wanaotakiwa kupasua mguu wanapasua kichwa na kuleta maafa na kupunguza nguvu kazi ya taifa. Haya yote ni matokeo ya kuipuuza lugha yetu ya thamani.
Umoja na amani tunayoishuhudia nchini mwetu pamoja na sababu nyingine ni kutokana na lugha hii kuweza kutuunganisha watu wa makabila tofauti, hali inayochangia kuendeleza utengamano wa kitaifa na hii inatoa hamasa na chachu katika harakati za kulinganisha Bara la Afrika na kuunda taifa moja la Afrika.
Kiswahili pia kina uwezo wa kulinda afya ya Watanzania kwa sababu vipodozi vingi kutoka nje, maji na vyakula vya viwandani huwekwa vibandiko vya maelekezo kwa watumiaji vilivyoandikwa kwa Kiingereza.
Katika muktadha wa sasa si zaidi ya asilimia 10 ya Watanzania ndio wanaojua kuongea Kiingereza kwa ufasaha.
Matumizi ya vyakula, maji na vipodozi vilivyoandikwa maelekezo ya matumizi yake kwa lugha za kigeni ni hatari kwa afya za wananchi. Hivyo matumizi ya Kiswahili ni njia pekee ya kukabiliana na tatizo hili.
Kuna tatizo gani kwa wazalishaji wa viwandani hususan wa vile viwanda vya ndani kushinikizwa kuweka maelekezo ya matumizi ya bidhaa kwa lugha ya Kiswahili?
Matumizi ya Kiswahili yanaweza kulinda masilahi ya taifa katika mikataba ya kimataifa hususan ile inayohusiana na rasilimali za nchi na mambo ya usalama.
Mikataba mingi ya kimataifa inaandikwa katika lugha ngumu za kisheria, hivyo wakati fulani inaweza kuwayumbisha wataalamu wanaohusika na kusaini mkataba husika.
Historia inatufunza na kutukumbusha kuwa moja ya sababu iliyosababisha sehemu kubwa ya Bara la Afrika kutawaliwa na ukoloni kwa karibu karne nzima ilitokana na viongozi wa jamii za Kiafrika kusaini mikataba wasiyoijua.
Pamoja na hilo, umma wa Watanzania ambao hawajui lugha za kigeni unanyimwa fursa ya kuijua mikataba hiyo na namna inavyoweza kuwanufaisha.
Miongoni mwa vitu vinavyodhalilisha utu wa mtu ni pamoja na kukumbatia tamaduni za kigeni, mfano kuchapa viboko na kuwapa vijana wetu waliopo mashuleni adhabu nzito kwa sababu tu wameongea Kiswahili. Huu ni utumwa mamboleo.
Ni vema tukaukomesha. Ni aibu kuendelea kuchapana wenyewe kwa wenyewe kwa sababu ya lugha za kigeni kama Wazungu na Waarabu walivyowachapa babu na bibi zetu enzi za utumwa.
Umewaona Wazungu wakichapa vijana wao kisa hawaongei lugha za Kiafrika? Mbona Wachina, Waarabu, Wajapani, Warusi na wengine hawawachapi vijana wao kwa sababu ya kutojua kuongea Kiingereza au Kifaransa? Hii ni aibu tunayowajibika kuifuta mara moja.
Isitoshe viboko na adhabu nyingi zinawajengea hofu wanafunzi hatimaye kufanya vibaya katika masomo yao.
Sheria na miswada mingi ya sheria serikalini inaandaliwa na kuhifadhiwa kwa Kiingereza. Watawala wanalifanya hili huku wakijua kuwa zaidi ya asilimia 80 ya Watanzania hawajui Kiingereza.
Kama ilivyotokea wakati wa kuandaa muswada wa sheria ya mabadiliko ya katiba mwaka 2011; hadi pale wananchi kupitia vyama vya upinzani na taasisi za kiraia kutoa shinikizo, ndipo watawala wakakubali kuubadili muswada ule na kuuandika kwa Kiswahili.
Hapa lengo ni kuwanyima fursa Watanzania kujua taarifa za msingi zinazohusiana na taifa lao. Tunaomba Katiba Mpya itamke kuwa Kiswahili ni lugha ya taifa itakayotumika katika mawasiliano yote serikalini na kufundishia shule za awali hadi vyuo vikuu.
Kwa kuidhinisha Kiswahili kutumika katika ngazi zote za elimu kuna fursa za ajira kupatikana kwa Watanzania kupitia kampuni za vitabu za ndani ya nchi kwa kuongeza wigo wa soko, hivyo mapato yao yataongezeka na kupanua fursa za ajira kwa kampuni zao na wataalamu wa kutafsiri vitabu vya kigeni watahitajika kwa wingi zaidi.
Pamoja na umuhimu wa lugha hii kwa upande wa mwananchi mmoja mmoja bado kuna watu wenye hoja za kupinga, baadhi wanasema Kiswahili hakina misamiati ya kutosha hivyo hakifai kufundishia elimu ya sekondari na vyuo vikuu.
Wenye mawazo haya wanachoshindwa kufahamu ni kuwa kadiri lugha inavyotumika ndivyo inavyoendelea kukua na misamiati yake kuongezeka na kadiri lugha isiyotumika ndivyo inavyoendelea kudumaa na hatimaye kutoweka kabisa.
Na katika kudhihirisha kuwa misamiati si tatizo katika Kiswahili; kampuni ya kuchapa vitabu ya Mkuki na Nyoka kwa kushirikiana na Haki Elimu wamezindua kitabu cha kemia kwa elimu ya sekondari kilichoandikwa kwa Kiswahili kinaitwa ‘Furahia Kemia’ ambacho kimeandikwa na jopo la walimu wa Tanzania.
Taasisi na wataalamu mbalimbali wamesema masomo yote yakiwemo ya sayansi yanaweza kuandikwa kwa Kiswahili.
Wengine wanasema mbona hata somo la Kiswahili wanafunzi wanafeli, sasa kama hoja ni kuboresha elimu hata tukitumia Kiswahili wanafunzi wataendelea kufeli tu, wanafunzi wanafeli Kiswahili kutokana na kutokuwa na mipango madhubuti ya kuongeza hamasa kwa wanafunzi kupenda na kusoma kwa bidii lugha yao ya taifa.
Wapo wanaosema kuwa Kiingereza ni Kiswahili cha dunia hivyo katika nyakati hizi za utandawazi ni sharti tuijue lugha hiyo inayozungumzwa na watu wengi duniani.
Wabebaji wa hoja hii wanapaswa kufahamu jambo moja kuwa utandawazi si lugha bali utandawazi ni ujuzi na maarifa.
Hivyo ili kuwa na jamii yenye uwezo wa kushindana katika zama hizi za utandawazi ni sharti kuwa na jamii yenye ujuzi na maarifa ya hali ya juu yanayopatikana kwa vijana kufundishwa kwa lugha inayoeleweka vema kwa mfundishaji na mfundishwaji.
Tuelewe kwamba Kiingereza na lugha zingine za kigeni zinazofundishwa shuleni na vyuoni zitaendelea kufundishwa kama somo huku masomo yote mengine yakifundishwa kwa lugha ya Kiswahili.
Mfano nchi ya Italia pamoja na kufundisha kwa lugha yao ya asili lakini zaidi ya asilimia 34 ya wananchi wake wanaweza kuongea Kiingereza, kwa Israel wao ni asilimia 84, Ujerumani 56, Ufaransa 39, Hispania 22 na Uholanzi asilimia 90.
Tanzania pamoja na kufundisha kwa Kiingereza masomo yote kwa zaidi ya nusu karne tokea tupate uhuru idadi ya wazungumzaji wa lugha hiyo hawazidi asilimia 10 (wanaojua kuongea na kuandika Kiingereza fasaha si kiswanglishi).
Ni kwa kutumia lugha zao ndiko kulikoifanya China, Japan, Ujerumani, Urusi na mataifa yote makubwa duniani kuboresha elimu zao na hatimaye kuweza kutoa wasomi waliobobea na kupiga hatua kubwa kiteknolojia na kiuchumi
src
Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment