Uwazi ilipata fursa ya kuwasiliana na wananchi wa wilaya hiyo ambayo pia ni jimbo la uchaguzi linaloongozwa na Mheshimiwa Hamis Kigwangala kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ambao walieleza matatizo mbalimbali yanayowakabili, ikiwemo ufukara wa kupindukia wakati kuna migodi kadhaa ya dhahabu kwenye jimbo hilo.
MATATIZO YA WANANCHI
Wananchi Waliozungumza na Gazeti la Uwazi, walieleza kwamba matatizo yanayowakabili ni pamoja na ukosefu wa huduma bora za kijamii kama maji safi na salama, huduma bora za afya, uhaba wa walimu, madarasa na vifaa vya kujifunzia kwenye shule.
Kuzorota kwa kilimo cha pamba, kutonufaishwa na madini yanayochimbwa kwenye ardhi yao katika Migodi ya Resolute na Golden Pride, ukosefu wa ajira, ufukara na matatizo mengine kedekede.
MAELEZO YA MBUNGE
Uwazi lilifanikiwa kuzungumza na mbunge wa jimbo hilo, Mheshimiwa Kigwangala ambaye alikuwa na haya ya kueleza: “Ni kweli kuna matatizo mengi jimboni kwangu na mimi kama mbunge, nakoseshwa usingizi na matatizo hayo.
“Nimeshafanya mambo mengi kuhakikisha naboresha maisha ya wakazi wa Nzega ambao wamenipa dhamana ya kuwaongoza. Tayari nimeyashughulikia matatizo mawili makubwa ya kuzorota kwa zao la pamba ambapo nimeanzisha mradi wa kuhimiza kilimo cha mazao ya biashara ikiwepo pamba.
“Zamani wananchi walikuwa wakilima pamba lakini baadaye mfumo huo ulikufa kwa sababu nyingi. Mpaka sasa tayari nimehamasisha kilimo cha pamba na zaidi ya wakulima 50,000 wamejiingiza katika zao hilo la kibiashara.
“Tumefufua zao hilo hadi kufikia uzalishaji wa tani milioni 8 msimu uliopita. Licha ya zao la pamba, nimehamasisha kilimo cha alizeti ambalo nalo ni zao la biashara.”
Kuhusu suala la madini kutowanufaisha wakazi wa Nzega, Kigwangala alisema: “Tangu nimeingia bungeni nahakikisha tunapata faida katika mradi wa dhahabu na faida tunazipeleka katika miradi mbalimbali ya wananchi.
“Lakini pia tunajenga stendi mpya ya kisasa na soko, pia SACCOS zaidi ya kumi zimeanzishwa.
Tumejenga zahanati zaidi ya 20, shule za sekondari zaidi ya 20, ‘high school’ nne, mbili tayari zimekamilika. Haya yote nayafanya kwa juhudi zangu binafsi kama mbunge,” alisema Kigwangala na kuongeza kuwa: “Hata hivyo, siyo wananchi wote wanaoziona juhudi ninazozifanya kwani kuna kundi la wapinzani ambalo kazi yake ni kunichafua.
“Siku zote nimekuwa sijibu hoja wala mashambulizi navumilia ninaposhambuliwa kwa sababu kazi yangu ni kuwatumikia wananchi. “Ikitokea nikagombea tena ubunge nitashinda kwa urahisi sana kwa sababu nimejikita katika kazi nilizofanya na wananchi wengi wanaona juhudi zangu.
“Kipaumbele changu ni kuhakikisha zao la pamba linawanufaisha wakulima wote, nahangaika usiku na mchana kuhakikisha kunakuwa na masoko ya uhakika na bei ya pamba inaongezeka. Najua zao hili likiwanufaisha wananchi matatizo mengine yatapungua sana.
“Pia naelekeza nguvu kuhakikisha wawekezaji wanaokuja kuchimba dhahabu, wanachangia maendeleo ya kijamii na siyo kutuachia mashimo tu baada ya kumaliza dhahabu zetu, msimamo wangu umesababisha niwe na maadui wengi lakini nasisitiza kwamba lazima watu wa Nzega wanufaike na dhahabu yao na nitapambana usiku na mchana,” alisema Kigwangala.
Aliongeza kuwa, hadi sasa tayari amefanikisha kusambaza umeme kwenye vijiji vingi, shule na zahanati jimboni mwake.
0 comments:
Post a Comment