KWANZA kabisa nimuombe Mungu azidi kuipa neema na amani Tanzania yetu, lakini pia tumshukuru kwa kutuweka hai tukiwa na afya njema.
Baada ya kusema hayo niseme kwamba nimeamua kuandika makala haya kutokana na kuona kwamba shinikizo la kutaka kusitishwa kwa Bunge Maalum la Katiba limezidi kuongezeka kutoka kada au taasisi mbalimbali hapa nchini.
Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba,Mh. Samuel Sitta
Mimi napendekeza kwamba mchakato huo usitishwe hadi Januari 2016 ili kupisha Uchaguzi Mkuu wa mwakani na kuokoa fedha za umma, hasa kama rasimu hiyo itakataliwa na wananchi au kukwama bungeni kutokana na sheria au kanuni.
Napendekeza hivyo kutokana na kukosekana kwa maridhiano baina ya pande mbili zinazovutana katika Bunge Maalum la Katiba, hali ambayo imesababisha mgawanyiko mkubwa katika nchi hivi sasa.
Hakuna siri, ni kwamba mgawanyiko huo ulianza pale yalipoibuka makundi kwa misingi ya kiitikadi za vyama vya siasa na kundi la wajumbe wanaotokana na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) waliposusia bunge hilo.
Hakika ukweli ni kwamba kitendo cha Ukawa kushindwa kurejea bungeni ni pigo na kinaunyima mchakato huo uhalali wa kisiasa na kisheria kwani kwa upande wa Zanzibar imegundulika kuwa wanapungua wajumbe 16 ili kuwezesha kupitisha Rasimu ya Katiba.
Binafsi sioni ulazima wa kuendelea na bunge hilo ilhali ikifahamika wazi kwamba Rasimu ya Katiba haitapata uungwaji mkono na wajumbe kutoka Zanzibar na kwamba kuendelea na mchakato huo ni hasara kwa taifa hasa kama rasimu itakataliwa na Watanzania.
Inashangaza kusikia kuwa Mwenyekiti wa Bunge Maalum, Samuel Sitta anasema eti anaamini kwamba bunge likikaribia mwisho watakuwa wamepata idadi ya kutosha, sasa kama muda wote hawakuwahi kufanikiwa kuwashawishi, ni kitu gani kitawawezesha kupata akidi katika muda huo? Je, wasipopatikana wajumbe wengine wa kuwezesha akidi kutimia itakuwaje? Jibu ni kwamba taifa litakuwa limeingia hasara kubwa kwa kupoteza fedha za umma.
Nashauri kwamba muda uliopo unapaswa kutumika kwa ajili ya maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa 2015, uchaguzi wa serikali za mitaa, uandikishaji wa wapiga kura katika mfumo mpya wa kielektroniki na utoaji wa Vitambulisho vya Taifa.
Katiba Mpya ya kidemokrasia na ya viwango vya kimataifa, haiwezi kukamilika na kutumika kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2015 na hakuna njia nyingine ya kunusuru mchakato wa Katiba Mpya zaidi ya kuusitisha.
Hakuna mtu anayeweza kubisha nikisema kwamba kwa hali ilivyo sasa huwezi kusema CCM ni wamoja, kwani kuna watu wana mitazamo tofauti, wengine wanataka bunge lisitishwe na wengine wanasema liendelee, lakini hata katika Kundi la Ukawa siyo wamoja maana wangekuwa wamoja tusingesikia kwamba wengine wapo Dodoma wakiendelea na mchakato.
Nilisikia kuwa wabunge wa CCM katika Bunge la Muungano walivutana kuhusu hoja ya kusimamishwa kwa mchakato wa Katiba Mpya kutokana na wajumbe wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kususia vikao.
Niliambiwa kuwa mvutano huo ulijitokeza katika semina ya wabunge wa kamati za Bunge hilo kuhusu Dhana ya Kusikiliza Maoni ya Wadau iliyoandaliwa na Bunge la Muungano kupitia mradi wake wa kuwawezesha wabunge (LSP), unaofadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP).
Nilihabarishwa kuwa mvutano huo ulianza wakati Mbunge wa Longido, Michael Lekule Laizer aliposema mchakato wa Katiba Mpya umekuwa ni jambo gumu na unaelekea kushindikana na hivyo kupendekeza usimamishwe hadi hapo kutakapokuwa na maridhiano.
Ndugu zangu, mchakato huu umekuwa ni vurugu na umekosa utashi mpaka wananchi wanashindwa kuelewa nini kinachoendelea na nashauri kwamba bila maridhiano tutakuwa tunatwanga maji kwenye kinu.
Tukirudisha mawazo yetu nyuma tutakumbuka kuwa ziliwahi kuundwa tume nyingi huko nyuma kama vile Tume ya Shelukindo (William), Tume ya Jaji Nyalali (Francis) na Tume ya Jaji Warioba (Joseph) iliyochambua tatizo la rushwa nchini, ambazo zilienda kwa wananchi kuchukuwa maoni ya wadau,  maoni hayo yako wapi na kwa nini yamefunikwa?
Wote tunajua kuwa tume hizo zimepoteza fedha nyingi za Watanzania lakini maoni ya wadau hayajulikani yamepelekwa wapi. Si vema hata kidogo kupuuza maoni ya wananchi na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kusema kwamba hata maoni ya wachache yasipuuzwe. Mwalimu alisema ni vema kuchukuwa maoni ya wachache kuliko kungoja wawe wengi na kusababisha vurugu nchini. Ushauri huu uzingatiwe.
Ukweli ni kwamba hapa nchini kuna tatizo la maoni ya wananchi kuingiliwa na wanasiasa na hii inatokana na kukosekana kwa uzalendo, uadilifu na ukweli kama ambavyo nimekuwa nikihimiza, hivyo basi naomba sana mchakato huu wa katiba yetu ya nchi usitishwe mara moja kwa sababu ambazo nimeziainisha hapa.
Jipu limepasuka, siwezi kuwa adui kwa kusema ukweli

0 comments:

Post a Comment

 
Top