WALIOSEMA, maisha ni safari ndefu, sina budi kuwapongeza kwa maana katika hali ya kawaida ya maisha yetu na hususan kwa watu wa kipato cha chini na kati, kwa kweli kila kukicha tunakumbana na mikiki mikiki kibao ambayo kwa njia moja au nyingine inazidi kutuongezea ugumu wa safari ya maisha yetu ya kila siku.
Ukigeuka huku bei ya mafuta juu, nauli za daladala ndio hizo tena, ukienda hospitali ndio kabisaa, kama huna cha juu ujue matibabu hupati, ukipigwa mapanga na kukikimbilia Polisi, huko tena na wao watataka wakuongezee machungu mengine kwa kukutoa kidogodogo ndio waanze kupanga mipango ya kukuhudumia, ukirudi nyumbani, mwenye nyumba anasubiri kodi yake ya pango, watoto wetu huko shule ndio balaa zaidi; vyumba vya madara havitoshi, vilivyopo havina madawati na matundu ya choo ni kichefuchefu kitupu, n.k. Kwa ujumla kila upande unaomzunguka Mtanzania wa kada hizi ni matatizo matupu!
Kutokana na ugumu wa maisha uliopo katika kundi hili, kwa kawaida kama siku inatokea kukuanzia vizuri, bila shaka siku hiyo huonekana ni fupi sana kwa jinsi ambavyo saa zinavyokatika kwa ulaini, lakini kama mambo yanakuwa hayajakaa mkao wa kula kwa upande wako, hapo ni dhahiri hata dakika moja kati ya zile sitini za saa, utaiona ni ndefu sana kukatika.
Hebu jaribu kufikiria mwenyewe, ni jinsi gani wale waliopo gerezani, hospitalini, vitani n.k., wanavyopata tabu kuivuka dakika moja ya saa wakati wewe mwenzangu na mimi ukiendelea kuyanyonya maji ya rangi ya mende kiulani kwa kuagiza moja moto na moja baridi.
Ni dhahiri hamuwezi kuwa katika hali moja, wewe utaendelea kupeta wakati wenzako wakiwa katika machungu makali ya kuivuka kila dakika ya saa iliyopo mbele yao.
Hivyo hivyo ndivyo ilivyo kwa Watanzania wengi wa kipato cha chini au kwa jina lililowahi kupata umaarufu sana miaka kadhaa ya nyuma yaani ‘walalahoi’ tunavyoendelea kugombana huku Uswahilini kwa kunyang’anyana makopo ya kuendea msalani wakati wale wenye nyadhifa zao za maana na vipato vya kushiba vyema wakiendelea kupeta katika mahekalu yao huko maeneo yenye sifa zote za miundo mbinu mizuri na iliyo bora kwa maisha stahiki ya bianadamu.
Walionena huko nyuma kuwa aliyenacho huongezewa, kwa kweli wangekuwa hai ningejikakamua kwa kila hali ili niwatafutie tuzo yoyote ile hata kama ni ya kilalahoi kwa jinsi ambavyo ukweli wa usemi huo unavyojidhihirisha waziwazi katika jamii yetu ya Kibongo.
Wewe mwenzangu na mimi mshahara wako haukufikishi hata mwisho wa wiki ya kwanza ya mwezi, hapo hapo ukitaka kwenda kuoga ni lazima upange foleni, haya tumbo nalo likikukusumbua lazima ukutane na foleni nyingine ya msalani, ukiumwa ndio kabisaa shida tupu huko kwenye hospitali zetu sisi tusioweza kupelekwa India wala Afrika Kusini,.
LUKU nayo inapokwisha ndio balaa–hailipwi hadi mkunjane mashati na wapangaji wenzako na ukigeuka nyuma mzee mwenye nyumba huyu hapa anadai kodi ya nyumba yake ambayo wakati huo huna!
Lakini cha kushangaza huyu huyu mlalahoi anayelala nyumba isiyokuwa na miundombinu stahiki kwa maisha ya binadamu ndiye anayelipa kodi kubwa ya pango kuliko hao wanaoishi nyumba nzuri na zilizopo sehemu nzuri kimiundombinu na zinazomilikiwa na shirika la nyumba ambalo ni la umma.
Kwao foleni wanayoijua ni ya magari tu barabarani na jinsi ya kuyaegesha majumbani mwao, kamwe siyo ya chooni, kwa kuwa kila mtu ana chumba chake cha choo na baadhi yao hata mbwa wana vyoo vyao tena vya ku-flashi!
Ukijaribu kupiga hesabu zako za mwezi mzima, utagundua kuwa mshahara wako hauwezi kukuwezesha kufanya jambo lolote lile la ziada zaidi ya pesa yako kuishia katika mzunguko huo wa kutatua matatizo ya kila siku ya nyumba unayoishi.
Kwa ujumla mambo haya ya utofauti mkubwa wa kiuchumi na huduma muhimu za jamii kati ya aliyenacho na asiyenacho, kama yatazidi kuongezeka kwa kasi hii iliyopo hivi sasa, ni dhahiri huko mbele lazima mwisho wake hautakuwa mzuri.
Kuna kila dalili kuwa chuki kubwa itajengeka miongoni mwetu, kwa asiyenacho kumchukia zaidi aliyenacho na hatimaye kundi la wasionacho ambalo ndilo kubwa, litakuwa tayari kwa lolote kutokana na kukata kwao tamaa ya kupata maisha bora.
Inaonekana kama vile wenye mamlaka hawalioni kabisa jambo hili, kwa kuwa hawajui kama kuna watu ambao kila kitu kwao ni foleni, kuanzia jikoni hadi chooni, lazima na wao kuna siku watataka waondokane na hizi foleni na kwa gharama yoyote ile ili wapate usalama wa matumbo yao.
Ni wazi serikali na mamlaka zake haziwezi kukomesha foleni zote, lakini kama wakidhamiria kama walivyodhamiria kutoa pesa za Bunge la Katiba, baadhi yao zinaweza kupunguzwa ama kumalizwa kabisa, kama vile foleni za watoto wetu mashuleni kukaa chini pamoja na kugombania matundu ya choo, vile vile dawa mahospitalini na vituo vya afya.
Hayo siyo mambo kabisa lazima yapigiwe kelele za kimatendo siyo kama za vita ya ufisadi za kung’ta na kupuliza


src
Tanzania Daima

0 comments:

Post a Comment

 
Top