Bunge la katiba likiendelea mjini Dodoma
Tunalazimika leo kutoa hadhari kwa wajumbe wa Bunge
Maalumu la Katiba kuwa, iwapo wataendelea kufanya vitimbi na vitendo vya
kulidhalilisha Bunge wakati wanapokuwa wakitoa hoja zao kama walivyofanya juzi
wakati Bunge hilo lilipokaa kumchagua mwenyekiti wake wa muda, taswira ya
chombo hicho kilichoundwa kutunga Katiba Mpya itaharibika na malengo yake
hayatafikiwa.
Wahenga waliposema siku njema huonekana asubuhi
walikuwa sahihi kabisa kwa sababu jambo lolote linaloanza vyema huwa na
uwezekano mkubwa wa kumalizika kwa mafanikio. Katika muktadha huo, Bunge
linapoanza shughuli zake kwa kutawaliwa na zogo na vituko kama ilivyotokea juzi
mjini Dodoma haliwezi kamwe kufikia malengo yaliyokusudiwa.
Inawezekana kabisa kwamba wapo watu wanaoweza kusema
kwamba matukio ya juzi bungeni yalikuwa madogo na kwamba yalitokea kutokana na
kutokuwapo kanuni au mwongozo wa kusimamia uchaguzi huo wa mwenyekiti wa muda. Tunaweza kukubaliana kiasi fulani na hoja ya pili ya kutokuwapo kanuni na
mwongozo, lakini hatuwezi kukubali hata kidogo hoja ya kwamba matukio hayo
yalikuwa madogo, kwani yalivuruga mwenendo wa kikao husika, ambapo baadhi ya
wajumbe walitoa kauli za kuudhi na kutumia lugha isiyo ya kibunge.
Vituko ndani ya Bunge hilo vilianza wakati wajumbe
walipoingia ukumbini juzi jioni kupiga kura kumpata mwenyekiti wa muda baada ya
wajumbe watatu waliogombea nafasi hiyo kujieleza na kujibu maswali ya wajumbe.
Baadhi yao waliuliza maswali yaliyoashiria shari na
yasiyokuwa na tija kwa ufanisi wa mchakato huo. Kwa mshangao mkubwa wa wajumbe,
mmoja wa wajumbe alimuuliza mmoja wa wagombea iwapo angefurahi kama angempigia
kura.
Hatua ya kupiga kura ilizua utata mkubwa kiasi cha
kusababisha uchaguzi kurudiwa. Hali hiyo ilisababishwa na tukio lililoonekana
kwa baadhi ya wajumbe kama uchakachuaji wa kura, kwani idadi ya wajumbe
waliopiga kura ilizidi idadi ya wajumbe waliopaswa kupiga kura.
Utata huo wa upigaji kura ulijenga hisia hasi kwamba
upigaji kura katika vikao vijavyo vya Bunge hilo, ambapo baadhi ya mambo
yataamuliwa kwa kupiga kura utachakachuliwa. Katika mazingira hayo, tutegemee
nini kama siyo vurugu zitakazosababishwa na uchakachuaji wa kura?
Sisi tunadhani kwamba kazi kubwa itakayoukabili
uongozi wa Bunge ni kutekeleza majukumu yake kwa uwazi, kutenda haki kwa
wajumbe wote ili kuweka mazingira ya kuaminiana.
Tumesisitiza mara nyingi kwamba Bunge hilo
litasambaratika iwapo litaendeshwa kwa ubabe na misingi ya itikadi za vyama
badala ya kusimamia matakwa na maoni ya wananchi waliyoyatoa kupitia Tume ya
Mabadiliko ya Katiba iliyokuwa chini ya Jaji Joseph Warioba.
Pamoja na baadhi ya vyama vya siasa, hasa CCM
kuwalazimisha wajumbe wake walio katika Bunge hilo kufuata msimamo wake kuhusu
vipengele mbalimbali vilivyo katika Rasimu ya Katiba, baadhi ya wajumbe hao
wamesema wataweka mbele masilahi ya wananchi badala ya misimamo ya vyama vyao.
Kinachoshangaza ni kwamba kila mtu anazungumzia utaifa. Lakini likija suala
hili la Katiba Mpya wengi wanajikita katika misimamo ya kisiasa.
Kikao cha Bunge hilo juzi
kimetufumbua macho na kutambua kwamba wajumbe wake wasipojitambua na
kujitayarisha kisaikolojia kuhusu uzito wa majukumu yao, upatikanaji wa
demokrasia kupitia Katiba Mpya utabakia kuwa ndoto ya mchana.
0 comments:
Post a Comment