KUNA neno jipya limeingia katika misamiati ya Kidiplomasia; Twiplomacy– likifupisha maneno mawili Twitter Diplomacy (Diplomasia ya Twitter). Viongozi wa dunia sasa wameamua, kwa dhati kabisa, kutumia mitandao ya kijamii, hususani ule wa twitter, kwa ajili ya kupasha habari zinazowahusu na wakati mwingine kuchangia katika mijadala. Miaka 10 iliyopita, ilikuwa vigumu kwa kijana wa kawaida kuweza kuwasiliana au kuonana na Rais wake. Leo hii, Rais Jakaya Kikwete, anaweza kuwasiliana kupitia mtandao huu na kijana wa miaka 17 aliyeko Kirando, Nkasi kwa kutumia mitandao hii. Kuna kitu katika mtandao huu kinaitwa Followers (yaani watu ambao wanafuatilia taarifa za kila siku zinazotolewa na mtu husika). Kikwete, kwa mfano, ni wa sita barani Afrika miongoni mwa viongozi wanaofuatiliwa zaidi na watu. Kwa mujibu wa utafiti wa Twiplomacy uliofanywa na taasisi ya Burson-Marsteller ya Marekani ambao matokeo yake yalitoka Juni mwaka huu, Rais Barack Obama wa Marekani anaongoza kwa kufuatiliwa na watu wengi miongoni mwa marais na wafalme hapa duniani kwa kuwa na watu zaidi ya milioni 43.7. Utafiti huo umeonyesha kwamba kufikia Juni mwaka huu, asilimia 83 ya wanachama 193 wa Umoja wa Mataifa (UN) wana anuania za twitter zilizo rasmi. Kuhusu viongozi, utafiti huo umeonyesha kuwa nusu ya mawaziri wa Nchi za Nje duniani wana anuani zao za twitter huku asilimia 68 ya wakuu wote wa nchi duniani wakiwa nazo pia. Afrika Barani Afrika, kinara wa kuwa na wafuasi wengi ni Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya ambaye ana wafuasi zaidi ya 457,000 mitandaoni. Anafuatiwa na Rais Paul Kagame wa Rwanda mwenye wafuasi 407,515 na watatu ni Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini mwenye wafuasi zaidi ya 325,876. Kufikia jana, anuani binafsi ya Kikwete ilikuwa ikionyesha kwamba ana wafuasi (followers) zaidi ya 171,500. Kimsingi, wengi wa viongozi vijana wameonekana kufuatilia sana mtandao huu kuliko wale wenye umri mkubwa pengine kutokana na mazoea ya teknolojia hii mpya. Ndiyo maana, si ajabu kwamba, Kenyatta, ambaye ni miongoni mwa viongozi vijana zaidi barani Afrika, ndiyo anaongoza kwa kuwa na wafuasi wengi. Namna pekee ya kuongeza wafuasi si kuwa na jina kubwa pekee. Inatakiwa mhusika awe na uwezo wa kuandika na kuweka mambo yake kwenye anuani yake hiyo mara kwa mara. Tangu afungue akaunti yake hiyo Machi 2011, Rais Kikwete ameandika mara 1,543 na pia amekuwa akituma pia kupitia anuani yake hiyohiyo baadhi ya meseji zilizomkuna kutoka kwa baadhi ya wafuasi wake. Gazeti la Red Pepper la Uganda limeeleza namna Rais Yoweri Museveni alivyokuwa mgumu awali kutumia njia hiyo ya mawasiliano lakini sasa ni miongoni mwa viongozi wanaotumia zaidi mtandao huo. Twitter sasa umekuwa uwanja wa viongozi kueleza hisia zao binafsi kuhusu baadhi ya mambo ambayo katika hali ya kawaida, usingetaraji Rais ayazungumze katika maeneo rasmi. Kwa mfano, Kagame amekuwa akiandika kuhusu maoni yake mara baada ya kumalizika kwa mechi za mchezo aupendao wa soka, masuala ya kisera ya Taifa lake pamoja na masuala mengine ya kimataifa yanayogusa nchi yake pamoja na Afrika kwa ujumla. Kagame pia anafahamika kuwa miongoni mwa viongozi wanaojihusisha moja kwa moja na mtandao huu –wakati mwingine akibishana moja kwa moja na watu ambao wametoa maelezo au maoni ambayo hakubaliani nayo. Hata hivyo, inafahamika kwamba viongozi wengi wa Afrika wana watu maalumu ambao wanawafanyia kazi ya kuweka taarifa kwenye anuani hizo na si wao binafsi. Rais Museveni, kwa mfano, anamtumia sana Sarah Kagingo, mhitimu wa miaka ya karibuni wa Chuo Kikuu cha Makerere nchini Uganda ambaye ameajiriwa kama Mshauri Msaidizi wa Masuala ya Mawasiliano wa Rais. Kazi yake aliyopewa, limeandika gazeti hilo la Red Pepper ni kuhakikisha kwamba Rais Museveni anakubalika kwa vijana na kutoa ujumbe ambao unaeleweka kwa urahisi na haraka. Sarah, inaonekana ameifanya kazi hiyo vizuri. Tanzania na Jakaya Kikwete Kikwete alianzisha anuani yake ya twitter@jmkikwete, miaka mitatu iliyopita. Yeye alikuwa miongoni mwa viongozi wa mwanzo kabisa kujiunga na mtandao huo hapa nchini. Inasaidia pia kwamba Kikwete ana watoto ambao wanajihusisha vizuri kwenye mitandao hiyo na pengine labda aliambukizwa na vijana wake hao. Kikwete hutumia mitandao ya kijamii kwa mambo mengi. Anaitumia kwa ajili ya kusalimu watu katika matukio mbalimbali kama sherehe za mwaka mpya na zile za kidini. Wakati wa kuanza kwa Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, Rais Kikwete alitumia anuani yake hiyo kuwatakia kheri Waislamu waliokuwa wakianza kutimiza jukumu lao hilo la kidini. Mara ya mwisho kwa Kikwete kuweka kitu kwenye akaunti yake ilikuwa ni Agosti 6 mwaka huu, wakati alipoweka mazungumzo yake na Watanzania waishio nchini Marekani ambapo, pamoja na mambo mengine, alizungumzia kuhusu tuhuma za mmoja wa wanawe kuhusishwa na biashara ya dawa za kulevya. Kuna picha nyingine za kibinafsi sana ambazo watumiaji wa mitandao ya kijamii, na haswa wale wanaofuatilia anuani ya jmkikwete wanaweza kuzipata ambazo magazeti hayawezi kuwa nazo. Kwa mfano, April inane mwaka jana, Kikwete aliweka picha katika mtandao wake wa twitter akiwa kwenye kivuko cha Magogoni, Dar es Salaam, na akaeleza kwamba anakwenda kumjulia hali Rais mstaafu wa Zanzibar, Aboud Jumbe. Kuna picha nyingine ya Aprili mwaka huohuo ambayo inamuonyesha akiwa katika mbuga ya Seronera hapa nchini pamoja na familia ya Makamu wa Rais Mteule wa Kenya, William Ruto. Picha hiyo ilipigwa Aprili 4 mwaka jana, siku chache baada ya Ruto kushinda nafasi hiyo akiwa mgombea mwenza wa Kenyatta. Uzuri wa picha hizi za kwenye mitandao ya kijamii ni kwamba, wananchi sasa wanaweza kupata picha nzuri kwa wakati uleule wakati tukio linatokea; tofauti na picha za zamani ambazo zinaonekana magazetini siku moja baada ya tukio kuonekana. Utafiti huo wa akina Burson-Marsteller unaeleza kwamba mitandao ya kijamii inasaidia kumfanya kiongozi aonekane kama raia wa kawaida na hivyo inakuwa rahisi kwa wananchi kujihusisha naye. Juhudi za Raia Mwema kuzungumza na mtu anayeshughulikia anuani za Rais katika mitandao ya kijamii ili kuelewa uzoefu na changamoto za kazi yake hiyo hazikufanikiwa hadi tunakwenda mitamboni, ingawa mmoja wa wanafamilia ya Kikwete alilithibitishia gazeti hili kwamba yuko mtu maalumu anayeshughulikia suala hilo. Wana Twitter wanasemaje kuhusu anuani ya Rais Mmoja wa wanasiasa wanaotumia sana mitandao ya kijamii hapa nchini Zitto Kabwe, anasema ni jambo zuri kwa Kikwete kuwa na anuani yake binafsi kwani huo ndiyo mtazamo wa kisasa duniani. Alisema Kikwete alikuwa miongoni mwa viongozi wa mwanzo kabisa kuwa na anuani yake binafsi na viongozi wengine wamefuata nyayo zake, jambo alilosema ni zuri. Hata hivyo, anasema ingawa Kikwete alianza vizuri, spidi yake ya kuweka masuala imepungua kuliko wakati anaanza mwaka 2011, na kwamba hilo limesababisha anuani ipoe na matokeo yake anazidiwa wafuasi na viongozi wa nchi ndogo kama Rwanda. “Kuna kitu kingine pia nimekiona katika akaunti ya Kikwete. Anafuatilia watu wanane tu ambapo ninaowakumbuka ni Umoja wa Vijana wa CCM, Peter Kallaghe, Dk. Faustine Ndugulile, Benard Membe, Mohamed Dewji na January Makamba. “Hakuna Rais yoyote duniani ambaye Kikwete anafuatilia taarifa zake kwenye mitandao hii ya kijamii. Hakuna mwanasiasa yeyote wa upinzani hapa nchini ambaye Kikwete anafuatilia masuala yake. “Hakuna msanii yeyote hapa nchini ambaye Rais anafuatilia habari zake. Tuna wasanii wakubwa tu hapa nchini kama vile Diamond, Ali Kiba, Profesa Jay na Ambwene Yesaya (AY). Wote hakuna Kikwete anayemfuatilia ingawa anajulikana anapenda muziki na wasanii. “Kuna watu wanaitwa opinion makers kama akina Rakesh Rajan ambao huwa wanaposti vitu vyenye kufikirisha sana kila wakati. Anuani hii ya Rais inamuonyesha kama mtu ambaye anataka kusikiliza watu anaojua hawatamshughulisha na hiki si kitu kizuri,” alisema Zitto ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini. Kwa kufuatilia anuani binafsi ya Zitto, yeye anafuatilia watu 1, 298 akiwamo Kikwete, Raila Odinga, Narendra Modi, Rajani, Global Witness, Museveni na wengine. Kwenye anuani yake ya twitter ya @UKenyatta, Uhuru anaonyesha kuwafuatilia watu 98 (90 zaidi ya Kikwete) wakiwamo marais Kagame na Museveni, Bill Gates, Obama na wafanyabiashara wengine wakubwa na taasisi za kimataifa. Diplomasia ya # na Selfie Takwimu zilizotolewa na utafiti wa akina Burson zinatoa picha ya kusisimua kidogo kuhusu twitter na athari zake katika siasa za kimataifa. Ingawa Modi aliukwaa Uwaziri Mkuu wa India miezi michache tu iliyopita, tayari amekuwa kiongozi wa nne kuwa na wafuasi wengi kwenye mtandao huo. Picha yake ya kwanza kuvuta hisia za watu ilikuwa ni ile aliyojipiga mara baada ya kumaliza kupiga kura katika uchaguzi huo wa Aprili mwaka huu. Katika mazungumzo yake na waandishi wa habari, Modi amepata kusema yafuatayo; Mtu anayedharau nguvu ya mitandao ya kijamii katika dunia ya sasa hajui analolifanya. Nitatumia mitandao ya kijamii kwa kadri nafasi inavyoruhusu.” Wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanaeleza kwamba mojawapo ya masuala yaliyompa Modi nafasi kubwa ya kushinda ni namna alivyokuwa akitumia vema mitandao ya kijamii. “Kwa urahisi kabisa, hakuna mwanasiasa nchini India aliyewekeza na kuamini katika mitandao hii kuliko Modi na ushindi wake huo umesimika dhamira yake aliyokuwa nayo,” anasema mwandishi wa kitabu cha Narendra Modi: The Man of the Moment, M.V Kamath katika mojawapo ya kurasa ndani ya kitabu hicho. Twitter pia imekuja na mambo yake mengine. Kwa mfano sasa kuna kitu kinaitwa Hashtag Diplomacy (#) ambapo kama watu wanataka kufanya kampeni kuhusu jambo lolote, basi hutumia alama ya # (hashtag) na kuweka ujumbe mbele yake. Mfano mzuri wa diplomasia ya aina hii ni lile tukio la kutekwa kwa wanafunzi zaidi ya 200 na kundi la kigaidi la Boko Haram ambapo mara moja jamii ya kimataifa iliibuka na ujumbe uliokuwa na maneno #BringBackOurGirls, ukitaka kundi hilo liwaachie wasichana hao. Wasichana hao hawajaachiwa bado lakini harakati bado zinaendelea. Selfie nalo ni jina jipya lililoibuka katika mitandao ya kijamii. Ni kawaida sasa kuona wanasiasa na viongozi wakubwa kabisa wakijipiga picha wenyewe na kuzisambaza katika mitandao ya kijamii. Zamani, wanamuziki na wasanii wa aina nyingine ndiyo waliokuwa wakitumia sana mitandao hii lakini sasa wanasiasa nao wameingia. Katika ripoti ya mwaka huu ya Twiplomacy, picha ya mfano iliyotumika ni ile waliyojipiga Rais wa Singapore, Lee Hsie Lo, akiwa na mwenzake wa Indonesia, Susilo Bambang Yudhoyono, wakati wakiwa kwenye kigari cha mchezo wa gofu. Na kama kama unakumbuka, Obama alipiga pia selfie wakati wa msiba wa aliyekuwa Rais mstaafu wa Afrika Kusini, Nelson Mandela, akiwa na Waziri Mkuu wa Denmark, Helle Thorning Schimidt. Nenda muziki usiku hapa Dar es Salaam na utaona namna watoto wa mjini walivyocharuka kwa Selfies siku hizi. Kila mahali panafaa kwa Selfie -

src
Raia mwema
Ezekiel Kamwaga

0 comments:

Post a Comment

 
Top