- Asema lazima kutumia vema rasilimali watu, ardhi na muda
SHEIKH Nurdin Abdallah Mangochi, anaheshimika sana nchini, si tu kwa sababu yeye ni Sheikh wa Mkoa wa Mtwara, au tu kwa kuwa Shule ya Sekondari anayoiongoza, Ocean, safari hii imefanya vizuri sana kwenye matokeo ya kidato cha sita, lakini pia ni msomi mwenye shahada za juu kabisa kwenye elimu ya dini ya Kiislamu.
“ Unaiona shule hii. Nyasi zimejaa kila mahala. Kwa ujumla si safi sana. Lakini hakuna shule iliyofanya vizuri kutushinda mwaka huu Mkoa wa Mtwara kidato cha sita. Hapa hakuna division four, wala division zero.
“Tuna division one tano, divison two 19 na division three 14. Hakuna aliyetukaribia hapa,” anasema Sheikh Mangochi akiongeza kwamba ufaulu huo ni wa watahinwa 39 wa michepuo ya Historia, Kiswahili na Kingereza (HKL); Historia, Jiografia na Kingereza (HGL) na Historia, Jiografia na Kiswahili (HGK). Kwa jumla shule ya Sheikh Mangochi ina wanafunzi 705 kwa vidato vyote sita.
Sheikh Mangochi ni kati ya viongozi 19 wa dini wa Mikoa ya Lindi na Mtwara, ambao mwaka huu, chini ya udhamini wa Wizara ya Nishati na Madini, walipelekwa nchini Thailand kwa ziara ya mafunzo ya sekta ya uzalishaji gesi, yeye akiwa kati ya viongozi wakuu wa msafara.
Ni nini alichojifunza huko?” Nilichojifunza kwa wenzetu wale ni matumizi mazuri ya rasilimali tatu: Mtu; Ardhi na Muda.
“Wamewaelimisha sana watu wao. Masuala ya uchumi wa gesi wanayajua. Wengi wa wafanyakazi wa sehemu muhimu katika vinu na kampuni ya gesi ni raia wenyewe.
“Ardhini ndiko kuna gesi, madini na mafuta. Lakini ili uitumie vyema ardhi kwa maendeleo, yakubidi uwe umesoma vizuri namna ya kuzidua. Kila mahali tulipopita katika mfumo wa uzalishaji gesi tulikuta msimamizi alikuwa ni Mthailand. Sasa hapa kwetu hatujafika ngazi hiyo. Bado tunagombea mrabaha.
“Kuhusu muda, kule hakuna mtu anatembea bila shughuli. Kila mtu ana shughuli na muda wote unatumika kwa kazi. Vitu hivi vitatu, vikitumika vizuri ndipo tunapata maendeleo. Wenzetu wamevitumia vizuri sana na maendeleo yao ni makubwa sana.”
Lakini hali ya Mtwara, na hasa ukirejea zile vurugu za gesi inatoka au haitoki, inaruhusu wana Mtwara na Watanzania kwa jumla kupata ustawi utakaotokana na gesi?
Anasema Sheikh Mangochi: “Gesi si ya leo wala kesho. Gesi hii ni tunu ya Taifa, si tu ya Mtwara. Kwa yale yaliyotokea, Serikali ilikwishakuomba radhi kwenye vikao rasmi.
“Yale mliyosema kwenye vyombo vyenu (si Raia Mwema) kuhusu Mkuu wa Mkoa (Kanali mstaafu Dk. Joseph Simbakalia) wala hayakuwa ya kweli. Watu hamjui. Huyu ameshiriki katika kila hatua katika kuelekea kupata mafanikio ya gesi. Ameshiriki tangu mwanzo kabisa, na nadhani huko serikalini wanaolifahamu suala la gesi ya Mtwara na maendeleo yake wa kumshinda yeye ni wachache.
“Ni kweli wakati ule amani ilitoweka hapa. Sasa hali unayoiona ni ya kujenga na kurudisha amani. Bado haijakamilika, lakini inarudi. Wananchi wanangoja ahadi zao zitimizwe.
“Polepole wanaona kuwa zile ahadi ni za kweli. Viwanda vinajengwa, kikiwamo hicho cha Dangote (cha sementi), ukienda Madimba utashangaa kunavyojengwa. Sasa wanakuja wawekezaji wengi kuliko wakati ule. Mtwara yenyewe inajengeka sana. Na ujue kazi ya kurudisha amani huwa si rahisi, ni ngumu.
“Elimu ya gesi inatolewa. Makongamano yanafanyika , na safari kama hizi za kwetu ni kwa ajili ya kuvuta amani. Tuliporudi tumeandika serikali ni mambo gani yafanyike.”
Safari ya kwenda Thailand ya Sheikh Mangochi na viongozi wenzake wa dini ilikuwa ni hatua ya tatu ya jitihada za Serikali, kupitia Wizara ya Nishati na Madini, za kutafuta muafaka na uelewa na kujiweka tayari kwa ajili ya uchumi mpana wa gesi.
Januari 19 na 20 mwaka huu, viongozi hao wa dini wa Mikoa ya Lindi na Mtwara walikutana na uongozi wa Wizara ya Nishati na Madini, katika Hoteli ya Whitesands kupata uelewa mpana na stadi juu ya rasilimali gesi na mafuta kwa amani na maendeleo endelevu. Kongamano la pili la pande hizo lilifanyika VETA, Mtwara, kati ya Februari 25 na Februari 26, mwaka huu.
Ripoti ya msafara wa Sheikh Mangochi tayari imefikishwa serikalini ikibeba mambo mengi: Mfumo uliotumika katika Mafunzo; Maeneo yaliyofikiwa na Wajumbe; Mambo ya Msingi/Muhimu Waliyojifunza; Changamoto na Matarajio.
“Elimu iliyopatikana nchini Thailand itumike vyema kuhabarisha na kuwafahamisha Watanzania kuwa na subira katika matarajio ya haraka waliyonayo wananchi juu ya gesi asili,” inasema sehemu ya Ripoti hiyo katika eneo la Changamoto.
Inazitaja changamoto nyingine kuwa ni kusambaza umeme vijijini; kutoa huduma za maji kwa jamii, hususan, za vijijini; kutoa elimu stahiki kwa maeneo ya vijijini; kuwa tayari kubadilika na kuwa na mawazo mbadala; ubinafsi ni sumu katika suala zima la kuleta maendeleo katika nchi yoyote na kuwaanda vijana kushika uchumi wa gesi kwa maendeleo endelevu kwa kuwapa elimu, hasa ya masomo ya sayansi.
Changamoto nyingine ni vijana kubadili mtazamo wa kuyakimbia au kuyaogopa masomo ya sayansi kwa kuwa huo ndio ukombozi kwa Wazalendo kushika uchumi wa gesi; kujitolea (kwa vile) uzalendo umekuwa ni tatizo katika maeneo mengi nchini, na, uhusiano kati ya Serikali, sekta binafsi, asasi za kiraia na wananchi yanapaswa yaboreshwe kupitia viongozi wa dini mbalimbali.
Inasema pia Ripoti hiyo katika eneo la Matarajio: “kutoa elimu sahihi kwa jamii tunazoziongoza namna wenzetu wa Thailand walivyofanikiwa kupitia sekta ya gesi; kuwa na mikutano ya kupeana tathmini kati ya viongozi wa dini na kutoa taarifa na ushauri kwa Serikali kila baada ya miezi mitatu; kuchochea vijana, hasa wa Mikoa ya Lindi na Mtwara, kuwa na hamasa ya kusoma masomo ya sayansi, ujasiriamali, utalii, ukarimu kuanzia shule za awali mpaka elimu ya juu, na, wananchi hasa wa Mikoa ya Lindi na Mtwara, kubadilika kimtazamo na fikra katika masuala mengi ya kimaendeleo, ikiwamo gesi asilia.”
Gesi inayotajwa kupatikana nchini ni nyingi mara nne ya ile ya Thailand. Kwa mujibu wa takwimu, miaka 30 iliyopita, uchumi wa Thailand na Tanzania ulikuwa katika ngazi sawa.
Gesi imechangia sana maendeleo ya Thailand kiasi kwamba sasa ni kati ya nchi 20 duniani zinazovutia sana uwekezaji kwa mujibu wa takwimu za Benki ya Dunia (WB).
Ili Tanzania ifike ilikofika Thailand, baada ya kuanza kuvuna gesi, anasema Sheikh Mangochi, itahitaji uongozi bora, si bora uongozi; itahitaji mipango makini si mipango ya kulipua; itahitaji maono, si kufikiria tu leo na kesho, bali fikra pana; usimamizi na nidhamu ya hali ya juu.
0 comments:
Post a Comment