Tangu gazeti dada la The Citizen lichapishe mwishoni
mwa wiki habari za upotevu wa Sh480 bilioni katika Wizara ya Fedha, Serikali
imekaa kimya kama vile wizi huo ni tukio la kawaida, hivyo halihitaji maelezo
ya kina wala ya haraka. Wananchi walitegemea kwamba Serikali ingetoa kauli haraka
iwezekanavyo kuhusu mazingira ya upotevu huo na hatua inazochukua kuwawajibisha
wahusika.
Tunasema kiasi hicho cha fedha zilizoibwa ni kikubwa
kwa sababu ni zaidi ya bajeti ya mwaka kwa baadhi ya wizara, zikiwamo wizara
kubwa kama ya Uchukuzi ambayo katika mwaka wa fedha wa 2013/14, kwa mfano
ilitengewa Sh491 bilioni.
Tunaambiwa Sh480 bilioni zilizopotea katika Wizara ya Fedha zinaweza
kujenga kilomita 375 za barabara kwa kiwango cha lami ikiwa ni urefu wa kutoka
Dar es Salaam hadi Gairo, kilomita chache kutoka Dodoma. Tujiulize kiasi hicho
cha fedha kingeweza kugharamia madawati, zahanati na madarasa mangapi kwa ajili
ya wagonjwa na wanafunzi wetu.
Pamoja na ukimya wa Serikali kuhusu wizi huo, tumetiwa
moyo na hatua ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Fedha za Serikali (PAC), ambayo
imemtaka Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Fedha za Serikali (CAG), Ludovick Utouh
kuchunguza upotevu huo wa kiasi hicho kikubwa cha fedha ambacho kilitumika
pasipo maelezo katika kipindi cha miaka miwili ya fedha cha 2012/13 na 2013/14.
Wasiwasi wa kamati hiyo ni kwamba kuna uwezekano
mkubwa wa kuwapo kwa mtandao mkubwa wa wizi wa fedha za Serikali katika Wizara
ya Fedha. Jambo hilo limethibitishwa na vitendo vya wizi wa kimtandao ambavyo
vimekuwa vikifanywa na baadhi ya watumishi wake wakishirikiana na baadhi ya
watendaji wa Tamisemi.
Ugumu uliopo hapa ni kwamba haijulikani kama fedha
hizo zilizopotea zilitokana na kodi za wananchi au wafadhili ambao walichangia
Sh842 bilioni katika bajeti ya mwaka wa fedha wa 2012/13. Ni sahihi kabisa kwa
Kamati hiyo ya Bunge kushangazwa na kuendelea kuwapo kwa vitendo vya ufisadi
serikalini, hasa kwa kuzingatia ukweli kwamba ripoti za CAG kila mwaka zimekuwa
zikifichua wizi wa mabilioni ya fedha katika Serikali Kuu na Serikali za Mitaa.
Kujirudia kwa vitendo hivyo kila mwaka ni ishara kwamba Serikali haina dhamira
ya kupambana na vitendo hivyo.
Mwenendo huo wa Serikali unashangaza, hasa kutokana na
ukweli kwamba mwaka 2013/14 ilikuwa na nakisi ya Sh847 bilioni katika bajeti
yake. Hivyo, utekelezaji wa mipango yake ya maendeleo ingekwama kama siyo
kukopa mabilioni ya fedha kutoka vyanzo vya nje na ndani ya nchi.
Matokeo yake ni kuzidi kuongeza mzigo wa Deni la Taifa ambalo limefikia
Sh27 trilioni sasa, huku ikishindwa kukusanya kodi na kupanua wigo wa vyanzo
vya kodi. Ndiyo maana iko hoi kifedha na
karibu shughuli zake zote zimesimama, huku ikisuasua
kulipa mishahara ya watumishi wake.
Pamoja na hali hiyo mbaya kifedha, bado vitendo vya wizi na ufisadi
serikalini vinaendelea kama tunavyoshuhudia vikishamiri katika Wizara ya Fedha.
Ni jukumu la Serikali kudhibiti ubadhirifu na ufisadi miongoni mwa watumishi
wake, vinginevyo uchumi wetu utazidi kudidimia. Kwa kuanzia iwasake na
kuwawajibisha wote walioiba Sh480 bilioni kutoka Hazina
Source
mwananchi
0 comments:
Post a Comment