Katiba Mpya ya Kenya imeanzisha
mambo mengi mapya. Imeshusha madaraka kwa wananchi na kuwapa madaraka makubwa
magavana ya kuamua mambo mbalimbali.
Kenya ilizindua Katiba mpya Agosti 27 mwaka 2010
kwenye sherehe iliyojaa mbwembwe katika bustani ya Uhuru, Nairobi.
Hiyo ilikuwa baada ya Wakenya kupiga kura kwa wingi
wakiunga mkono Katiba Mpya. Badala yake katiba imekuwa chungu kwa Wakenya kwa
magavana kuaanzisha ushuru wa aina mbalimbali ikiwemo ushuru wa kuaga maiti.Inatafsiriwa
kuwa, magavana wametumia mamlaka yao kunyanyasa wananchi katika kaunti.
Katika Kaunti ya Kiambu, inayoongozwa na Gavana
William Kabogo, kuna ushuru mpya unaotozwa kwa familia iliyopoteza
mpendwa ama wapendwa wao, Hakuna anayekubaliwa kumzika mfu
wao bila kulipa ushuru huo. Pia, huwezi kuchinja mfugo wako nyumbani bila
kulipa ushuru!
Katika Kaunti ya Kakamega, Gavana amebuni ushuru wa
kuku ambapo kila mfugaji atalipa Sh20 kwa kila kuku anayemfuga.
Pia, watu wanapoomboleza, lazima walipe ushuru wa
kuomboleza haswa wanapotazama mwili wa marehemu. Ukiutazama zaidi ya mara
mbili, utalipa ushuru zaidi ya mara moja!
Watu hawajui la kufanya na wana majuto makuu kwa
kukaribisha Katiba mpya 2010. Walipokuwa wanaipitisha walikuwa na matumaini
kwamba ingebadilisha maisha yao kwa kuleta utawala na huduma za Serikali Kuu
karibu yao. Wakati huo wa mchakato wa Katiba mpya, Makamu wa Rais William Ruto
alikuwa katika upande uliokuwa ukipinga Katiba hiyo.
Kutetea Katiba
Hata hivyo, Muungano wa Jubilee ulipochukua hatamu ya
uongozi, Ruto na Uhuru Kenyatta waliapa kuilinda na kuitetea Katiba hiyo. Katiba
ikawa mwanzo wa Serikali mpya iliyoshusha zaidi madaraka kwa wananchi hadi
ngazi ya Kunti, kwa lugha ya Kenya inaitwa Serikali ya Ugatuzi, ambapo
mipaka ya nchi iliyowekwa wakati wa ukoloni, iligawanywa upya ili mipaka
mipya ya Kaunti 47 iundwe.
Machi 4 mwaka 2013, uchaguzi mkuu ukafanyika na
viongozi mbalimbali wakiwamo magavana wakachaguliwa, ikiwa ni mara ya kwanza
kwa Kenya kuwa na viongozi wa aina hii.
Sasa Kenya ina magavana 47, baadhi ya watu wanaona
kuwa viongozi hawa wanakuwa kama miungu watu ambao Wakenya hawana budi
kumshukuru Mola kwa sababu yao.
Hali hiyo inatokana na tuhuma za ufisadi
zinazowakabili baadhi magavana, hali iliyowakasirisha Wakenya walio wengi.
Mmoja wa anayekabiliwa na tuhuma hizi ni Martin Wambora wa Kaunti ya Embu
Kiongozi huyu alipoteza wadhifa wake wiki iliyopita,
baada ya Bunge la Kaunti kupiga kura ya kumwondoa katika wadhifa wa Ugavana.
Wambora alituhumiwa kujihusisha na ufisadi wa hali ya
juu, ambapo Kaunti ilipoteza mamilioni ya fedha baada ya zabuni ya
kununua mbolea na mbegu za mahindi kwenda mrama.
Mbegu za mahindi hazikumea na mbolea haikuwa nzuri,
huo ulikuwa mwanzo wa masahibu ya Wambora yaliyomfikisha mbele ya Kamati ya Seneti
iliyosikiliza kesi yake na kuamua kumfuta kazi. Naibu wake sasa amechukua
nafasi yake na kufanya Kenya kupata gavana wa kwanza mwanamke.
Kufutwa kazi kwa Wambora kulifungua mlango wa Bunge la
Seneti kuonyesha kati ya seneta na gavana, ni nani mkubwa.
Wakati Seneti ilikuwa ikitoa uamuzi wake
kuhusu hatma ya Wambora, maseneta wawili walisema hawatashiriki kwenye zoezi
hilo kwa sababu mchakato mzima haukufuata haki.
Seneta mmoja aliyeunga mkono kufutwa kazi kwa Wambora,
aliiambia Seneti kuwa, kuanzia sasa magavana watajua ‘ nani kati yao na sisi
ndiye ana uwezo wa kumtimua na kumwadhibu’.
Kwa wadadisi wa kisiasa, hatua ya Seneti kumng’oa
mamlakani gavana huyo, ni jaribio la maseneta kutoa ujumbe kwa magavana
wanaotuhumiwa kuwapuuza viongozi hao haswa katika suala la kupeleka madaraka
kwenye kaunti. Sasa, Wambora ameenda nyumbani kutafuta kingine cha
kufanya na Seneti inapanua upeo wake ili inase magavana zaidi wanaoshukiwa
kufuja pesa za umma na kubuni sera potofu za kunyonya jasho la wananchi wa
kawaida kwa kuwatoza ushuru.
Kusambaza ufisadi
Ufisadi sasa umesambazwa kutoka Serikali Kuu hadi
Serikali za Mashinani na kufanya maisha kuingia kwenye mkondo mbaya zaidi.
Fedha zilizopaswa kutumwa kutoka kwenye Serikali Kuu kwenda kwenye
kaunti, hazitumiwi ipasavyo.
Badala yake, pesa hizo za maendeleo ya kikaunti
zinafujwa na kuelekezwa kwenye miradi bifasi ya magavana na vibaraka wao.
Ajira katika kaunti ni kama sarakasi kwa sababu
magavana hawazingatii sheria na kanuni zinaoongoza uajiri wa wafanyakazi wa
umma.
Magavana wanaajiri jamaa zao wasio na ujuzi au elimu
na kuwaacha wataalamu waliosomea nafasi husika, Uchunguzi uliofanywa miezi mitatu iliyopita, unaonyesha kuwa
magavana wametenga mamilioni ya fedha kugharimia safari zao za nchi za nje
haswa Uingereza, Amerika na Ufaransa.
Seneta inanuia sasa kukata ‘pembe’ za magavana wote
na kuna orodha ya majina tisa ya wale wanaotakiwa kufika mbele ya Kamati
ya Seneti kujibu maswali kuhusu matumizi ya fedha za umma.
Majibu yatakiwa
Magavana hao tisa wanatakiwa pia kujibu maswali
kuhusu ushuru tata walioanzisha katika kaunti zao.Anayelengwa zaidi ni Gavana
wa Kaunti ya Bomet, Isaac Ruto aliyekuwa amezoea kumzomea na kumkosoa Makamu wa
Rais kwa hili na lile. Majibizano kati ya hao wawili yalikuwa yakitawala vyombo
vya habari.
Gavana Rutto anaonekana kama ‘mwenye kichwa kikubwa’
na anafaa ‘kurekebishwa’ na Seneti ili afuate mkondo unaotakikana. Lakini Seneti ina haki ya kuwaadhibu magavana wanavyopenda? Nguvu hizi za
Seneti kuwaadhibu magavana zimetoka wapi?
Kwa muda mrefu, mashindano katika ya maseneta na
magavana kuhusu ‘ukubwa’ yamekuwa yakitawala vyombo vya habari.
Magavana walioandikiwa barua kufika mbele ya Seneti
wanasema maseneta wamekosea kisheria kuwataka wafike mbele yao.
Hatua ya kwanza wanayochukua magavana kujaribu
kuwazuia maseneta kuwaadhibu ni kutuma maombi ya kesi kwa kwa mahakama ya
kisheria ili iamue nani kati yao ni ‘ndume’ ya mwengine.
Mwaka mmoja umeisha tangu Uchaguzi Mkuu
umefanyike, lakini kilichodhairi shahiri ni kwamba maendeleo ya kipekee
wanayoyazingatia viongozi waliochaguliwa ni kujipiga kifua kuonyesha nani ni
mkubwa zaidi ya mwenzake. Hayo yakiendelea, barabara
zimezorota, sekta ya afya imesambaratika na wananchi wamepoteza matumaini, ya
kuona siku moja wataishi maisha yanayofaa na kuachana na ufukura wao wa miaka
mingi.
Ufisadi umeota mizizi nchini na ni mzigo kwa maisha ya
wananchi, hawaoni tofauti kati ya vitendo vya maseneta na magavana.
Hii ni kwa kuwa wengi wao wanashiriki ufisadi.
Ni kweli kwamba kama maseneta wangekuwa na nafasi ambayo magavana wanazo,
baadhi yao wangefanya kama vile magavana walivyofanya kwa kufuja mali za umma
na kuendeleza ukabila.
Katiba Mpya ilikuwa inaonekana kama baraka kwa
Wakenya, lakini kwa hakika imeleta shida nyingi na kufanya maisha kuwa magumu
zaidi.Wanaoumia ni wananchi wa kawaida, huku viongozi wakiendelea
kujilimbikizia mali bila kutoa jasho.Wanaendelea kutajirika huku wananchi
wakihangaishwa na maisha. Mwokozi wao ni nani?
Source
mwananchi
0 comments:
Post a Comment