Dar es Salaam. Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), imetangaza
uamuzi mzito dhidi ya wanachama wake sita ambao hivi karibuni waliitwa na
Kamati Ndogo ya Maadili na kuwahoji kutokana na tuhuma za kuanza kabla ya
wakati kampeni za Uchaguzi Mkuu wa urais wa mwaka 2015.
CCM imewatia hatiani vigogo wote sita kwa makosa ya
kujihusisha na kampeni za uchaguzi kabla ya wakati, hivyo kuwafungia kugombea
nafasi za uongozi ndani ya chama hicho kwa miezi 12, pia wakiwa chini ya
uangalizi.
Waliokumbwa na adhabu hiyo ni Waziri Mkuu wa zamani,
Edward Lowassa, Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye na Waziri wa Mambo ya Nje
na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe.
Wengine ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na
Uratibu), Stephen Wassira, Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia,
January Makamba na aliyewahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye
akizungumza na waandishi wa habari jana alisema wanachama hao wote sita
walitiwa hatiani kwa makosa ya kuanza kampeni za kuusaka urais wa 2015 kabla ya
wakati jambo ambalo ni kinyume na taratibu za chama hicho, hivyo kutoa onyo
kali. Adhabu ya onyo kali kwa mujibu wa taratibu za chama hicho inamaanisha
kuwaweka chini ya uangalizi kwa miezi 12 ili kuhakikisha hawajihusishi na
vitendo vyovyote vinavyokwenda kinyume na misingi ya chama hicho, vinginevyo
hatua kali zitachukuliwa dhidi yao.
“Mwanachama aliyepewa onyo kali atakuwa katika hali ya
kuchunguzwa kwa muda usiopungua miezi 12 ili kumsaidia katika jitihada zake za
kujirekebisha,” alisema Nnauye.
Hatua hiyo ya CCM imezitia doa harakati za vigogo hao,
kwani watatumikia adhabu yao hadi Februari 2015 na wakati wote watakuwa
wakichunguzwa mienendo yao.
Nnauye alisema makada hao kwa kuanza kwao kampeni za
kutafuta kuteuliwa kuwania urais kabla ya wakati ni kinyume na kanuni za
uongozi na maadili za CCM, toleo la Februari 2010, Ibara 6 (7)(i).
“Wamethibitika kufanya vitendo vinavyokiuka maadili
ndani ya chama na baadhi yao kufanya vitendo vinavyokiuka maadili ndani ya
jamii. “Vitendo vya namna hii ni kosa kwa mujibu wa kanuni za uongozi na
maadili za CCM toleo la Februari 2010, Ibara kadhaa za kanuni hizo,” alisema
Nnauye.
Alisema: “Kamati Kuu baada ya kuthibitisha makosa hayo, imewapa watu wote
sita waliohojiwa adhabu ya onyo kali na kuwataka wajiepushe na vitendo
vinavyokiuka maadili na iwapo wataendelea na vitendo hivyo chama kitawachukulia
hatua kali.”
Alisema Kamati Kuu imeiagiza kamati ya maadili
kuwachunguza mawakala na watendaji wa wanachama hao waliokuwa wakiratibu
shughuli mbalimbali ili waweze kuchukuliwa hatua kali za kinidhamu hatua
inayolenga kuhakikisha chama hakigawanyiki.
Nnauye alisema Ibara 6 (2) (1-5) ya maadili ya viongozi wa chama hicho
inawazuia kutoa michango, misaada, zawadi za aina yoyote, kukusanya michango na
kufanya kampeni bila ya kupata kibali kutoka kamati ya siasa ya halmashauri ya
eneo husika.Sumaye, Membe wanena
Akizungumza jana, Sumaye alisema: “Siwezi kuzungumza
chochote kwa kuwa sijapata taarifa rasmi kutoka ndani ya chama.
“Mimi sijapata taarifa yoyote, nitakapopata barua
ndipo nitakaposema, kwa sasa ndiyo kwanza ninakusikia wewe ukinipa hizi
taarifa,” alisema Sumaye.
Kwa upande wake, Membe naye alisema hajapa taarifa
kutoka ndani ya chama na hivyo hawezi kuzungumzia taarifa za kusikia.
“Sina habari hadi sasa! Utaratibu wa Kamati ya Maadili
ni kupeleka taarifa Kamati Kuu….Kamati Kuu inajadili na barua huandikwa kwa
kila aliyehojiwa na kupatikana na hatia. Mimi sijapata hiyo barua na siwezi
kukujibu au kutoa maoni ‘based on hearsay!’ vuta subira” alisema Membe.
Mnyukano CCM,Katika siku za karibuni kumekuwa na vita
ya maneno baina ya makada wa chama hicho, wakituhumiana kwa rushwa na kutangaza
mapema kugombea urais kabla ya ruhusa rasmi
ya chama. Malumbano ya sasa yalishika kasi Januari
Mosi mwaka huu wakati Lowassa, alipotangaza kuanza rasmi kwa safari aliyoiita
ya matumaini ya ndoto zake, ambayo alisema itatimiza ndoto za Watanzania za
kupata elimu bure, maji safi na maendeleo ya uhakika.
Lowassa alitoa kauli hiyo wakati wa hafla ya mwaka mpya aliyowaandalia
rafiki na jamaa zake, Januari Mosi, mwaka huu huko Monduli mkoani Arusha.
Source
mwananchi
0 comments:
Post a Comment