Taarifa iliyotolewa hivi karibuni inayoonyesha kuwa deni la Taifa linakua kwa wastani wa Sh2 trilioni kila mwaka, imepokewa tofauti, huku wengi wakilalamikia hali hiyo.

Kulingana na taarifa hizo za Serikali ya Tanzania ni kwamba mwaka 2005 Taifa lilikuwa na deni la Sh10 trilioni, ambalo limekua hadi kufikia Sh27 trilioni mwishoni mwa mwaka jana.

Kulingana na hali ilivyo sasa, Tanzania inaelekea kupoteza sifa za kukopesheka; bado asilimia 22 ya kufikia kikwazo cha kutopata mikopo.

Mikopo inatumikaje
Mbaya zaidi hata mikopo hiyo imeonekana kutotumika kama ilivyotarajiwa.Katika kudhihilisha hilo inaelezwa miaka ya 70, Serikali ilikopa Sh96 bilioni kwa lengo la kuanzisha Kiwanda cha Viatu Morogoro, lakini kilifilisika.

Baada ya kufilisika, kilibinafsishwa miaka ya 90, deni la fedha zilizotumika likawa bado mzigo kwa wananchi wa Tanzania.
Waziri wa Fedha, Saada Mkuya hata hivyo anajipa matumaini kuwa licha ya kuwa na deni hilo, Serikali bado inayo nafasi ya kukopa fedha.

Kauli hiyo inatokana na hatua ya Serikali kwa kushirikiana na taasisi za kimataifa kufanya thathmini iliyokuwa na lengo la kuangalia uhimilivu wa deni hilo katika kupata mikopo.

Tathmini hiyo ya Septemba mwaka jana ilionyesha deni hilo linaweza kuhimili kwa sababu viashiria vyote bado viko chini ya ukomo unaotakiwa.

Wachumi wanasema kutokana na mazingira hayo, makadirio ya miaka kadhaa ijayo Serikali inaweza kuingia kwenye kikwazo cha kupata mikopo endapo haitakuwa na mkakati wa kulipa deni na kupunguza mikopo hiyo.

Profesa Humphrey Mushi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) anasema kukopa siyo dhambi lakini ni muhimu kuzingatia mikopo hiyo inatumikaje.

“Lazima kujiuliza je, uwezo wa kulipa upo au la, siyo vizuri kukopa tu ili mradi; siyo kukopa tu kwa sababu eti bado tunayo nafasi ya kuendelea kukopa,hiyo siyo sahihi,” anasema Profesa Mushi na kuongeza;

Serikali isijisahau katika mikopo hiyo kwa sababu eti tumepata ugunduzi wa gesi asilia, ikumbukwe inaweza kukopa na gesi ikakosekana inakuwa ni hasara kubwa kwa taifa, kwa hivyo ni muhimu kuwa makini na maeneo ya kuwekeza mikopo hiyo.

Tahadhari kwa Serikali

Akitoa mifano, Profesa Mushi anasema kwa sasa Serikali inatakiwa kuhakikisha inatumia fedha za mikopo katika miradi yenye tija katika uchumi wa Taifa.

“Serikali ikope pale inapowezekana, siyo kukopa na kuwekeza katika mambo mengine yasiyo ya maendeleo,” anasema.

Mbali na hilo, Profesa Mushi anasema Serikali inatakiwa kuwa makini na taarifa za wahisani juu ya mikopo.

“Wakisema eti bado tuna vigezo vya kukopa tu haitasaidia, hao siyo wa kusikiliza sana, badala yake iwe na utaratibu wa kutumia mawazo ya Watalaam wa ndani,” anasema

Wizara ya Fedha imejipangaje?

Mwandishi wa makala haya alifanikiwa kufanya mahojiano na Waziri wa Fedha Saada Mkuya ili kujua mikakati na tahadhali zilizopo katika wizara yake juu ya deni la Taifa.

Kwanza kabisa Waziri Mkuya anasema mpaka sasa Serikali haijafikia uwezo wa kusitisha ukopaji.

“Kulipunguza deni hilo maana yake tusiendelee kukopa lakini sisi hatujafikia uwezo wa kuacha kukopa kwa sababu mapato yetu ya ndani hayajitoshi,” anasema na kuongeza;

Tunachokifanya kwa sasa ni kuhakikisha tunakuwa na utaratibu wa kupata mikopo itakayokuwa na riba ndogo, yenye masharti nafuu.

Waziri Mkuya anasema pamoja na kuendelea na ukopaji, wizara yake itakuwa makini na mikopo hiyo katika mpangilio wa bajeti yake ikiwemo kupeleka fedha hizo katika miradi ya maendeleo mbalimbali ya uchumi nchini.

Kila mkopo tutakaochukua kwa sasa utaelekezwa katika miradi ya maendeleo hasa ile inayochochea ukuaji wa uchumi na mapato ya ndani, kwa mfano miundombinu. Ni kwamba siyo kila mradi utaombewa mkopo,” anasema Waziri Mkuya.

Pia Serikali inaangalia njia nyingine za kukopa hapa nchini kupitia ushirikiano wa pamoja kati ya sekta binafsi na umma (PPP).

“Zote hizo ni jitihada za kuhakikisha tunapata mikopo inayokuwa na mabadiliko makubwa ya uchumi wa taifa, pia itatusaidia kutofikia kwenye vikwazo vya kupata mikopo kwa sababu uchumi unapokua hata kasi ya kufikia vikwazo inapungua,” anasema waziri huyo.

Mazingira ya deni lenyewe

Mnamo mwaka 2006, deni la Taifa lilikuwa asilimia 70 ya Pato la Taifa, ingawa msamaha wa madeni ulipunguza kiwango hicho hadi asilimia 21 mwaka uliofuata.

Kwa sasa deni hilo ni sawa na bajeti ya Serikali ya mwaka mmoja na nusu kwa mujibu wa bajeti ya mwaka 2013/14 ya Sh17.7 trilioni. Kati fedha hizo, Sh20.23 trilioni zinatajwa kuwa ni deni la nje huku Sh6.81 trilioni deni la ndani Waziri Mkuya anasema sababu za kuongezeka deni hilo ni pamoja na mikopo iliyopokelewa na Serikali ambayo muda wake wa kulipa haujafika.

Aidha malimbikizo ya deni la nje yanayofikia Dola 801.7 milioni kutoka kwa nchi zisizo wanachama wa jumuiya ya wahisani, ni baadhi ya mambo yanayochangia kukua kwa deni la Taifa.

Sourece mwananchi

0 comments:

Post a Comment

 
Top