Muundo wa muungano ni moja ya mambo ambayo yamevuta zaidi hisia za wananchi wengi na hiyo inatokana na mjadala uliopo hivi sasa ambapo Bunge maalumu la Katiba limekaa kujadili rasimu ya katiba mpya na iwapo wataafikiana Katiba mpya ya Tanzania itapatikana baada ya kupigiwa kura na wananchi.
Watanzania waliamua kuandika katiba mpya ili iendane na hali ya sasa ikiwa ni pamoja na kuangalia mapungufu katika muungano ambayo yamekuwa yakilalamikiwa na kila upande wa muungano. Wakati Jaji Warioba akiwasilisha maoni hayo bungeni alisema asilimia 60, ya wananchi wa Zanzibar waliotoa maoni yao walitaka muungano wa mkataba huku asilimia 61 ya wananchi wa Bara waliotoa maoni yao wakipendekeza muundo wa serikali tatu.
Lakini pamoja na maoni hayo, kuhusu aina ya muungano wautakao wananchi ni wazi kwamba kwa kipindi cha miaka takribani 50, faida za muungano ni kubwa na mojawapo ni wananchi kuungana na kuwa wamoja bila kujali wametoka maeneo gani ya muungano.
“Wananchi wameungana wameimarisha undugu, umoja na mshikamano, na pia nchi ina taasisi zinazofanya kazi kwa pamoja. Haya ni mafanikio makubwa ya muungano,” anasema Jaji Warioba.
Hiyo ndiyo sababu mojawapo ya rasimu ya Katiba mpya kupendekeza suala la uraia uwe ni mmoja na haki za binadamu zimeorodheshwa ili kulinda haki na misingi ya utu, lengo likiwa ni kuwaendeleza wananchi na kuendeleza umoja na mshikamano wao.
Akitoa maoni na mtazamo wake kuhusu muungano wa Tanzania, mjasiriamali kutoka Zanzibar, Zuhura Issa Salum, anasema yeye anapenda muungano wa Tanzania uendelee kudumu milele na pia anapenda muundo wa serikali mbili, kwani muundo huo ndio uliomfikisha hapo leo kimaendeleo.
“Sioni kama kuna tatizo kubwa la muungano, kasoro ndogondogo ni za kutafutia ufumbuzi ila sio kuvunja muungano wote, hata kwenye familia kuna matatizo madogomadogo ambayo mnayatafutia suluhu lakini sio kuvunja undugu,” anasema Zuhura. Anasema pamoja na kuwepo kwa kasoro za muungano, lakini kwa umri wake unaolingana na muungano huo, amekuwa huru kuishi upande wowote wa muungano na kwamba hata wazazi wake kwa upande wa baba yake asili yao ni kutoka bara.
“Kwao baba yangu walizaliwa wengi, wako ndugu waishio Kondoa, Dodoma wengine wanaishi Tanga lakini baba yeye alihamia Zanzibar miaka hiyo kabla hata ya uhuru. Sasa si rahisi kututenga. Bara nina ndugu na visiwani ndo nilikozaliwa,” anasema Zuhura.
Zuhura anasema Wazanzibari wengi ambao wanaangalia mbele akiwemo yeye hawawezi kukubali muungano uvunjike kutokana na faida zake nyingi, lakini anasema kuna wachache ambao wana uchu wa madaraka na wengine, hususan baadhi ya vijana, wameingia kwenye ushabiki wa kuchukia muungano kwa sababu za makundi bila ya wao wenyewe kufahamu uzuri wa muungano.
“Mimi naona tatizo kubwa la wananchi wa Zanzibar sio wote wanaouchukia muungano, ila tatizo ni siasa kuingizwa kwenye jambo hili na pia dini kupenyezwa na hivyo kuwachanganya baadhi ya watu. Ila tunahitaji vijana wetu waelimishwe, wengi wameshaabikia kuona muungano sio mzuri bila wao wenyewe kuufahamu muungano asili yake,” anasema Zuhura.
Akizitaja faida za muungano kutokana na mtazamo wake, Zuhura anasema, moja na kubwa ni uhuru alionao wa kwenda kokote na hiyo ni kutokana na muungano uliopo. Kwani yeye ni mjasiriamali mdogo na amekuwa akifanya kazi zake Tanzania yote bila kubughudhiwa wapi ametoka na hiyo imemfanya aendelee kibiashara.
“Katika biashara yangu ya viungo nimezunguka maeneo mbalimbali ya nchi, sijawahi kubughudhiwa wala kuulizwa mimi nimetokea wapi. Niko huru hata kuwaelezea wageni wanaokuja nchini kwenye maonesho mbalimbali ya kibiashara, kuwaambia uzuri wa vivutio vya nchi yangu ya Tanzania,” anasema.
Jambo jingine ni utambulisho ambao ni faida nyingine ya muungano kwani kujitambulisha yeye ni mtanzania kunampa amani na kumfanya awe na uhuru wa kuielezea nchi yake popote na hiyo ni kutokana na muungano uliopo. Akizungumzia hasara za kuuvunja, Zuhura anasema kwa wale wasioufahamu na kujua umuhimu wake, watafurahi ukivunjika, ila hasara ni nyingi na mojawapo ni Zanzibar haitakuwa salama kutokana na historia ya visiwa vingi duniani.
“Zanzibar ni kisiwa ambacho kwanza ni kidogo, na suala la usalama ni jambo zito. Muungano wetu umefanya usalama uwe imara na hivyo ikitokana na muungano kuvunjika tutapata shida na hatutakuwa salama. Hata mimi nitafadhaika sana kwani sitakuwa tena huru,” anasema Zuhura.
Zuhura hakusita kuzungumzia suala la utandawazi kama sababu nyingine ya kuharibu vijana ambao nao ndiyo wamejikuta wakiingia kwenye mkumbo wa ushabiki, bila woga wala kuonesha nidhamu.
“Utandawazi ni mzuri lakini, kwa upande mwingine umeharibu vijana wetu, wamejiona wao ndio wajanja kuliko hata wazazi wao. Wamewaona wazazi wao ni washamba na hawajasoma, hivyo ni rahisi kudanganywa na kushawishiwa kufuata mkumbo ambao hata hawaufahamu, “ anasema Zuhura.
Maoni yake kwa wananchi wa Tanzania anashauri vyombo vya habari na hata shule kuwaelimisha zaidi wananchi kuhusu historia ya muungano kwani wapo wasioufahamu na wamekuwa wa kwanza kuutaka uvunjike kwa kufuata ushabiki au mkumbo wa baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa au vikundi vya dini vyenye nia na maslahi binafsi.
“Muungano huu ndio umetufanya sote tufike hapa tulipo. Tuko huru na tuna maendeleo. Tusiwe wajinga kutaka ujuvunjike, tuendelee nao ila kero zilizopo ziendelee kutafutiwa suluhu, kwani ni bora kurekebisha kasoro kuliko kuanza jambo moja ambalo hulijui litakuwaje, ili hali hili la kwanza halina tatizo kubwa,” anasema Zuhura
src
Habari Leo
0 comments:
Post a Comment