BARAZA la Mitihani la Taifa (NECTA), limesema tangu kuanza mfumo wa kuweka picha kwenye vyeti vya kidato cha nne na sita kumepunguza kwa kiwango kikubwa vitendo vya kughushi.
Ofisa Habari wa NECTA, John Nchimbi alisema miaka iliyopita, kabla ya kuanza kwa mfumo huo, watu wengi walijihusisha katika kutumia vyeti bandia au vya kughushi.
Alisema kwa sasa ni rahisi kugundulika kwa mtu aliyegushi cheti chenye picha, kwani Baraza lina kumbukumbu ya picha halisi ya mwenye cheti.
“Kikiletwa kwetu cheti ambacho kimeghushiwa ambacho kina picha inakuwa rahisi kugundua kwa sababu picha halali ya mwenye cheti ipo kwenye kumbukumbu zetu,” alisema.
Nchimbi alisema kwa mwaka wa fedha 2012/13, vyeti 1, 891 ambavyo ni asilimia 3.7 ya vyeti vyote 50,497 vilivyowasilishwa kwa ajili ya uhakiki, vilibainika kuwa ni vya kughushi na ambavyo vimetolewa kabla ya mfumo mpya kuanza.
Kutokana na kukithiri kwa kughushi kwa vyeti vya elimu ya kidato cha nne, sita na ualimu, Baraza la Mitihani lilianza kutoa vyeti vyenye picha kwa Kidato cha Nne mwaka 2008 na mitihani mingine mwaka 2009.
Nchimbi alisema taasisi mbalimbali na wizara zimekuwa zikipeleka vyeti vya watumishi wao kwa ajili ya uhakiki. Taasisi hizo ni pamoja na Jeshi la Polisi, benki mbalimbali, Wizara ya Mambo ya Ndani na vyuo vya Ualimu.
src
habari leo

0 comments:

Post a Comment

 
Top