Hotuba ile ililenga kufuta upepo wa muundo wa serikali tatu ulioonekana kuanza kujizolea mashabiki wengi ndani na nje ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambacho kinataka muundo wa serikali mbili.
Kimsingi nawashangaa sana waliodhani Rais Kikwete, angetoa hotuba ‘makini’ isiyokuwa na chembe za u-CCM. Hivi kiongozi aliyefanya uteuzi wa wajumbe wa mabadiliko ya katiba kwa kujali zaidi masilahi ya chama chake atawezaje kutoa hotuba isiyokibeba chama chake?
Nani anaweza kunionyesha kwenye ilani ya uchaguzi ya 2005 au 2010 ya CCM kuna eneo linataja uandikwaji wa Katiba mpya? Jambo hili lipo kwenye ilani za vyama vya upinzani.
CCM hawakujiandaa kwa hili, Rais Kikwete, aliwakurupusha ndiyo maana aliwaambia wajiandae kisaikolojia lakini kwa bahati mbaya hata yeye hajajiandaa kisaikolojia .
Wana CCM mpaka hivi sasa wanamshangaa Rais Kikwete, alikotoa uamuzi wa kuanzisha mchakato huo ilhali hakukuwa na kikao chochote cha kukubaliana juu ya mchakato ule.
Hawa ndiyo walioamua kutokubali mchakato huo, wanadhani Katiba mpya itakiua chama chao ndiyo maana wanadiriki kumwaga machozi vikaoni wakihofia kupoteza madaraka.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Frederick Werema, alishatuambia mapema kuwa hakuna haja ya kuandika Katiba mpya bali tuiwekee viraka hii tuliyonayo, huyu leo hii ni miongoni mwa wanaosimamia uandikwaji wa Katiba mpya, je, lini ameona kuna umuhimu wa kuwa na mpya?
Aliyekuwa Waziri wa Katiba na Sheria, Celina Kombani, alipinga mchakato kuandika Katiba mpya lakini hivi sasa naye yumo bungeni, anashiriki katika kile asichokiamini.
Makada wa CCM, chama ni muhimu zaidi kuliko masilahi ya taifa, wako tayari kuuhujumu mchakato wa katiba mpya ilmradi mazingira ya kufanya ujanja ujanja nyakati za uchaguzi yaendelee kuwepo.
Makada wa aina hii wako tayari kufumbia macho uvunjwaji wa Katiba ya Muungano uliofanywa na Katiba ya Zanzibar ya mwaka 2010 ilimradi chama chao kiwe salama.
Sikumsikia Rais Kikwete, akipinga kuwa Zanzibar si nchi kama Katiba yao inavyosema bali ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kama ilivyo kwenye Katiba ya mwaka 1977.
Nawahurumia waliotarajia hotuba ya Rais Kikwete ingekuwa kama ile aliyoitoa nchini Afrika Kusini wakati wa mazishi ya Nelson Mandela. Hana ubavu wa kwenda nje na matakwa ya chama chake.
Rais Kikwete anatilia shaka maoni yaliyotolewa na wananchi katika Tume ya Jaji Warioba kubeba mawazo ya wananchi milioni 45 lakini hatilii shaka wajumbe 629 wa Bunge Maalumu kugeuza, kuingiza mambo mapya wakiwa wamejifungia bungeni.
Nilichokisikia kwenye hotuba ya kiongozi wetu, kimenifanya nisikitikie mamilioni ya fedha yaliyotumiwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba pamoja na yanayotumiwa hivi sasa na Bunge Maalumu la Katiba.
Kumbe viongozi wa CCM wameshaandika rasimu yao ila wanachokisubiri hivi sasa ni kuihalalisha kwa kutumia Bunge Maalumu, huku ni kuwanyonya Watanzania pamoja na kumdhalilisha Warioba na wenzake.
Rais Kikwete na makada wenzake wa CCM, hawana dhamira njema ya kutupatia Katiba itakayobeba masilahi ya wananchi.
Siioni dhamira nje ya Rais Kikwete, ndiyo maana alipochagua wajumbe 201, wa kuingia katika Bunge hilo aliwajaza makada wenzake ili kusimamia masilahi ya chama.
Wamejazana bungeni kana kwamba wanatunga katiba ya chama chao, wanataka kuumeza mchakato huu. Sina shaka tuendako si kwema.
Najua wanasiasa wengi hivi sasa wanawaza madaraka tu ndiyo maana hata Rais Kikwete hataki wananchi wawe na nguvu ya kuwaondoa wabunge wao wanaovurunda.
Wanataka katiba itungwe kulinda masilahi yao na wala si ya nchi. Huu ni udhaifu mkubwa sana!
Nawasubiri hawa wajumbe wa Bunge maalumu la Katiba, wachanganye akili za kuambiwa na zao, nasubiri kuvunjika kwa Bunge hili wakati wowote kuanzia sasa.
Najua ni lazima litavunjika tu, ni suala la muda tu, litavunjika kwa sababu lilianza bila maridhiano, lilianza kwa mguu mbaya, ambapo wajumbe wengi wamebeba misimamo ya vyama na makundi yao badala ya masilahi ya taifa
src
Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment