Kulikuwa na sababu nyingi za kuisubiri hotuba hii ya ufunguzi wa Bunge Maalumu la Katiba, kitu cha kihistoria katika taifa letu.
Lakini kubwa zaidi tulisubiri kusikia maoni yake juu ya Rasimu ya Katiba iliyowasilishwa na Jaji mstaafu Joseph Warioba.
Wengine walitaka kufahamu kama angekwenda kinyume cha matakwa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) anachokiongoza kinachosimamia muundo wa serikali mbili.
Ni wazi sote tumechanganyikiwa na tunaendelea kuchanganyikiwa kila siku tunavyojongea kuanza mjadala wa Katiba mpya, kiasi cha kufikiri kwamba katiba inahusu tu muundo wa serikali zetu.
Yaani serikali mbili au serikali tatu. Mambo mengi yanayotajwa kwenye rasimu, tunayaweka pembeni na kushikia bango muundo wa Muungano.
Hata rais mwenyewe, ingawa alianza kuonya kwamba Katiba ina vitu vingi, aliishia kutumia muda mwingi kufafanua muundo wa Muungano.
Mbaya zaidi kutujaza hofu kubwa juu ya muundo wa serikali tatu. Kumbe waliokuwa wakisema, kanuni ya Bunge Maalumu ya Mwenyekiti wa Tume kuwasilisha rasimu, baada ya hotuba ya rais, ilivunjwa kwa makusudi, walikuwa sahihi.
Hotuba ya rais ilikuwa inamjibu Mwenyekiti wa Tume na kuhakikisha inafuta kwa nguvu zote ‘Upepo mbaya’ (unaokwenda kinyume cha mapenzi ya CCM) alioueneza ndani ya Bunge na Watanzania kwa ujumla.
Maana yake ni kwamba muundo wa muungano ndicho kitu cha msingi. Pamoja na rais mwenyewe kutoa takwimu kutoka kwenye taarifa ya tume ya Jaji Warioba, kwamba asilimia kubwa ya Watanzania hawakuwa na matatizo na muundo wa muungano; kwa maana kwamba hawakutaja wala kujadili muundo wa muungano.
Ukweli ulio mbele yetu kwenye Bunge la Katiba, vyombo vya habari, kwenye taasisi, vijiweni, kwenye daladala na hata rais wetu mwenyewe ni muundo wa muungano.
Yeye mwenye, ameonyesha hilo kwa kutumia muda mwingi kuongelea muungano.
Labda nikubaliane na rais wetu kwamba hakuna mtu anayependa muungano uvunjike, tatizo ni aina ya muungano tulionao.
Na tukilichezea hili, majibu yatakuwa kwenye kura ya maoni. Watanzania ni wavumilivu muda wote, lakini kuna dalili za kuwashangaza wengi. Waswahili wanasema kimya kingi kina mshindo!
Kwa kifupi hotuba ya Rais Kikwete haikuwa mbaya wala ya kiushabiki. Ilikuwa ya kizalendo na yenye umakini. Hatuwezi kumlaumu kwa kuegemea kwenye chama chake.
Yeye ni mwenyekiti na ule ugonjwa wa kufikiri kwamba CCM ndiyo Tanzania, unamkumba pia. Ni ugonjwa wa hatari kuliko hatari zote alizozieleza kwenye muundo wa serikali tatu.
Bila kupata dawa ya kutibu ugonjwa huu sugu wa kufikiri CCM ndiyo Tanzania, ni vigumu kupiga hatua ya kwenda mbele.
Ingawa sifahamu kama kazi ya rais ilikuwa ni kulizindua Bunge au kuichambua rasimu ya katiba. Wataalamu na wachambuzi wengine watatueleleza zaidi juu ya hili.
Kwa maoni yangu, rais alitumia muda kuichambua rasimu, badala ya kulifungua Bunge Maalumu la Katiba.
Hata hivyo, hoja ninayoijenga kwenye makala hii, si juu ya kulifungua Bunge au kuichambua rasimu ya Katiba, wala sitapenda kujadili juu ya msimamo wa rais wetu wa serikali mbili, ambao anapenda kila mtu aukumbatie.
Na wala sijadili ushauri wa bure kwa Rais Kikwete, kwamba kazi kubwa aliyonayo ni kuwafunda wajumbe wa Bunge hilo la Katiba wanaotoka kwenye chama chake, waache tabia ya kukitanguliza chama.
Naandika kumshangaa rais wetu jinsi alivyotujengea hofu ya serikali tatu. Ametumia muda mwingi wa hotuba yake kuelezea changamoto za serikali tatu na hatari zake.
Tume ya Jaji Warioba, iliweka wazi changamoto za serikali mbili; mazuri ya serikali mbili na kuziweka wazi changamoto za serikali tatu na mazuri ya serikali tatu.
Lakini rais wetu, ameelezea kwa kina changamoto na hatari za serikali tatu, bila kugeuka upande mwingine.
Sikutegemea rais wa serikali ya muungano, aseme kwamba tukiwa na serikali tatu, serikali ya muungano haitakuwa na nguvu na itategemea hisani ya serikali washirika.
Kama angekuwa na nia ya serikali tatu, yeye mwenye angetuhakikishia mfumo wa kujenga serikali imara ya muungano.
Yeye amekuwa rais wa serikali ya muungano kwa kipindi cha miaka minane sasa, hivyo ana uzoefu wa kutosha kujenga serikali imara. Hata hivyo serikali ya muungano imekuwa ikisimama vipi miaka yote hiyo?
Wazanzibari wanalalamika kwamba Tanganyika imevaa koti la muungano. Je, si huu ndio wakati wa Tanganyika kulivua koti hilo kwa mpango maalumu wa kuhakikisha serikali ya muungano inakuwa imara?
Na wa kufanya kazi hiyo si ni rais huyu huyu aliye madarakani, ambaye ndiye alianzisha mchakato wa kuandika Katiba mpya?
Kwa nini alianzisha mchakato wa Katiba mpya akiwa na aina moja ya muungano? Au tuseme hakuwa na nia ya kuandika Katiba mpya?
Maana kama unaandika katiba mpya ni lazima utegemee mengi na ni lazima pia kujiandaa kwa lolote lijalo. Kukalia mawazo mgando ya serikali mbili ni kuonyesha kutojali mawazo ya wengine.
Kwamba kuifufua Tanganyika ni kuanzisha utaifa, ambao mwisho wake ni hatari? Mbona leo hii Wanzibari huko nje wanajitambulisha kwamba wao ni Wazanzibari na Watanzania wengine ni wa Tanzania Bara?
Muungano ulioimeza Tanganyika na kuicha Zanzibar, hauwezi kuufuta utaifa wa Tanganyika. Watoto watauliza kwa nini kuna Zanzibari na Tanzania Bara? Lazima watachimba na kutafuta chanzo.
Hivyo katiba hii mpya lazima ijibu yote haya. Ni lazima iweke wazi sababu za kumezwa Tanganyika na kuicha Zanzibar. Au Tanganyika ndio Muungano?
Tatizo la sasa hivi ni kubwa zaidi ya muundo wa serikali tatu unaoendekezwa na tume ya Jaji Warioba.
Kama tuna nia ya kweli ya kuhakikisha Muungano unadumu miaka mingi zaidi, tungefanya kila jitihada kuhakikisha tunatengeneza muundo wa serikali tatu ulio imara.
Hii ndiyo ingekuwa kazi kubwa ya Bunge maalumu la Katiba. Lakini kwa vile Bunge hili limejazwa woga na rais, itakuwa vigumu kulishughulikia hili kwa umakini.
Rais amesema kwamba baada ya Bunge kupitisha rasimu ya Katiba, kampeni za kuinadi na kuipigia debe ili ipitishwe na wananchi zitaanza.
Lakini yeye ameanza kampeni hizo mapema hata kabla Bunge halijaanza mjadala. Hotuba yake ilikuwa ni kampeni tupu.
Kule kuhubiri hofu juu ya serikali tatu, inaonyesha wazi kwamba alikuwa anapiga kampeni ya waziwazi. Wakati wanatengeneza Kanuni za Bunge, hawakufahamu kama rais atakuja kupiga kampeni, hivyo hakukuwa na kanuni ya kumbana. Kanuni hiyo itabaki kwenye kura ya maoni.
Binafsi, ni muumini wa muundo wa serikali moja. Lakini kutokana na maelezo ya tume ya Jaji Warioba, nitakuwa mwendawazimu kufikiria serikali moja.
Kama Zanzibar imejitangaza kuwa nchi, haiwezekani tena tukazungumza mfumo wa serikali moja. Nchi mbili, serikali mbili, haiwezekani kuunda serikali moja! Ndoto za mchana na mimi sitaki kuota mchana!
Rais, ametujaza hofu ya serikali tatu kwamba yawezekana majeshi yakakwama, kama serikali washirika watashindwa kuichangia serikali ya muungano, matokeo yake, wanaweza kufanya mapinduzi.
Ingawa hili linaweza kutokea pia hata kama hatuna muundo wa serikali tatu. Hata hivyo tulimtegemea rais wetu ajibu swali muhimu la Jaji Warioba.
Jaji Warioba, ametuambia kwamba waasisi wa taifa letu, Nyerere na Karume, walituwachia muundo wa nchi moja serikali mbili. Lakini leo hii tuna nchi mbili serikali mbili.
Kwa maoni ya tume ya Jaji Warioba, huwezi kuwa na nchi mbili, serikali mbili. Ukiwa na nchi mbili ni lazima uwe na serikali ya tatu.
Rais wetu amelikwepa hili na wala hakuligusia! Hivyo ametuacha njia panda. Na kusema ukweli kero za muungano zitaendelea na kushika kasi endapo tutaamua muundo wa serikali mbili.
Amesema tunaweza kumaliza kero zote za muungano. Lakini je, kero hii ya nchi mbili serikali mbili tunaweza kuimaliza vipi? Je, tunatunga katiba ya nchi mbili au katiba ya nchi mmoja?
Kama picha ya sasa ni kwamba Tanganyika inavaa koti la Muungano na Zanzibar wana katiba yao ambayo inapingana na Katiba ya muungano, kuna haja gani kuwashirikisha Wazanzibari kutengeneza katiba ambayo haiwahusu?
Rais Kikwete amesema kwamba mabadiliko yote yaliyotokea Zanzibar, yalifanyika kwa makubaliano ya pande zote mbili! Ina maana, hata Zanzibar, walipovunja katiba na kujitangaza wao ni nchi na kuandika katiba inayokinzana na katiba mama, alikuwa na habari?
Tuseme na yeye alishiriki kuivunja Katiba ya Muungano? Tunaweza kuwa na imani na rais anayekubali mchana kweupe ni uvunjaji wa Katiba?
Ninachokubaliana na rais ni kwamba tunatengeneza Katiba ya Watanzania. Na kwamba wajumbe wa Bunge Maalumu washikamane na kuacha tofauti zao.
Wajenge madaraja ya kwenda pande zote. Hili ni jambo zuri, lakini madaraja yajengwe kwa pande zote. Ile tabia kwamba CCM ndio wenye kufahamu vizuri njia ya kupitia taifa letu, ikome!
Maoni yote yasikilizwe na kila mjumbe apate muda wa kujieleza na kutoa maoni yake. Ule msemo wa kuwashughulikia wale wanaoupinga muungano, upigwe vita na usipate nafasi kwenye Bunge hili.
src
Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment