ZAMANI nilipokuwa nikiishi katika kijiji nilichozaliwa kabla ya kuja katika Jiji la Dar es Salaam, mabibi na mabwana Afya walikuwa ni muhimu sana katika jamii yetu. Watu hawa walikuwa maarufu na muhimu.
Umuhimu wao ulikuwa ukionekana pindi wafanyapo operesheni za usafi katika mazingira yetu, kila mtu alikuwa akijua ujio wao, watu walikuwa na hekaheka za kuhakikisha mazingira yao yanakuwa safi ili kukwepa mkono wa watu hawa.
Ukaguzi wao waliokuwa wakiufanya mara kwa mara, na wakati mwingine kwa kushtukiza.
Ulikuwa umelenga kuhakikisha wananchi wanakuwa na tabia ya kuweka mazingira yao safi, kwa kuangalia mashimo ya taka kama yamejaa au umechimba, kukagua usafi wa vyoo, na walifika mbali kwa kuhakikisha maji ambayo watu wanatumia kunywa yanachemshwa.
Na hawakuwa na mzaha na hili. Nakumbuka, walikuwa wakifika kwenye nyumba yako, wataomba maji ya kunywa kwenye glasi au kikombe, na wakiangalia tu bila hata kunywa wanaweza kubaini kama maji haya yamechemshwa au la.
Kazi yao haikuishia kwenye nyumba za makazi pekee, bali hata kwenye maeneo ya biashara, kama sokoni kuhakikisha mabucha, wauza unga, vitafunwa watoa huduma za chakula lazima wawe na aproni nyeupe na kofia kichwani.
Mfumo huu bado unaendelea katika wilaya kadhaa nchini na watu wanatozwa faini kubwa, ikiwemo hata kama watakuta shimo la taka limejaa na hujachimba jingine.
Mfumo huu mzuri ambao ni kampeni nzuri ya kupambana na uchafu na kuweka mazingira safi, nimeuacha huko nilikotoka. Na hata kazi nzuri ya mabwana na mabibi Afya, pia nimeiacha huko huko, huku Dar es Salaam watu hawa ni lulu.
Hawaonekani kabisa na sina uhakika kama katika Jiji hili, wapo au hawatakiwi kuwapo? Wakazi wa Jiji la Dar es Salaam, watakubaliana na mimi kuwa mabwana na mabibi Afya ambao ni muhimu katika jamii zetu hawapo, na kama wapo basi wamekwenda likizo ya milele.
Wengi watakuwa shahidi, kwani kuna mambo yanaendeshwa kiholela, na ni ushahidi tosha kuwa watu hao hawapo, kwani wangekuwapo nina hakika kabisa, kampeni ya usafi na kuwa na mazingira safi, ingekuwa endelevu.
Ukienda kwenye masoko au magenge yetu, utakuta uchafu umelundikana, na kwa vile wafanyabiashara wanalipa ushuru, kazi hii inaachwa kwa mkandarasi wa kuzoa taka.
Lakini hili lingefanyika kwa umakini, kama kungekuwa na nyongeza ya nguvu ya bibi au bwana Afya, ambaye angefanya kazi yake vizuri katika eneo lake.
Pia, hata ukienda kwenye mabucha ya samaki au nyama au migahawa, hali ya usafi katika maeneo hayo inatisha. Watu wanapata huduma hiyo wakiwa na shaka na usalama wa kile wanachokinunua.
Watoa huduma katika maeneo hayo, hawazingatii usafi na ni kawaida kuwakuta wakitoa huduma bila kuvaa kofia, vizibao vyeupe huku wengine wakiwa na makubazi.
Kusema ukweli usafi wa maeneo hayo ni kizungumkuti. Huko ni moja, tisa ni kwenye baa. Usafi wa baadhi ya baa ni wa kutisha, ukienda maliwatoni hali ni mbaya zaidi, kwani idadi ya matundu haiwiani na idadi ya watu wanaopata huduma hapo.
Pia, usafi na usafishaji wa vyoo hivyo ni hatari tupu. Naamini kuwa mabwana na mabibi Afya ni watu muhimu katika kampeni za kuhakikisha wananchi wanashiriki katika kuweka mazingira yao safi. Naamini watu hawa wakiwajibika na kutoza faini wakosaji, kila mtu atafanya shughuli zake kwa kuzingatia kauli ya ‘Mtu ni Afya’.
Kwa hali iliyopo sasa, hasa kwa kuangalia uchafu uliokithiri katika mitaa, mifereji, kukosekana kwa vyoo na usafi wa vyoo vyenyewe, nabaki kujiuliza hivi, mabwana na mabibi afya, wapo katika Jiji la Dar es Salaam?

src
Habari Leo

0 comments:

Post a Comment

 
Top