
KUNA taarifa za shughuli za uchimbaji wa makaa ya mawe zinazofanywa na kampuni ya Tancoal Energy jirani na bandari ya Ndumbi kule Ruvuma. Inasemekana tayari athari za uchimbaji huo wa makaa zimeanza kuonekana kwa samaki wa ziwa Nyasa kuathirika. Kama ilivyokuwa kwa wananchi wa maeneo yaliyozunguka mradi wa makaa ya mawe Kiwira, wananchi walio kando kando ya mradi huo kule Nyasa, Ruvuma, nao bado hawajaelimishwa vya kutosha juu ya faida na hasara za umeme unaozalishwa kutokana na makaa ya mawe. Katika hilo wasisubiri Bunge kupinga mradi wenye madhara ya kimazingira na kiafya kwao, wanaweza kwenda Mahakamani kudai kusimamishwa kwa mradi huu. Kuna mfano hai wa nguvu za wananchi kushinda kwenye vyombo vya haki katika shauri lenye kufanana na hilo. Na kuna mfano hai wa wananchi waliosimamia haki yao na wakaipata. Kwenye miaka ya tisini alitokea bwana mmoja pale Kunduchi Mtongani, aliitwa Festo Balegele. Festo na wenzake elfu saba walikubaliana wapeleke Mahakama Kuu shauri la kupinga uamuzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar Es Salaam kutenga jalala la takataka eneo wanaloishi wao. Sababu kubwa za kufungua shauri mahakamani zilikuwa mbili; mazingira na afya za watu wa eneo lile. Vyote vilikuwa hatarini. Uamuzi wa Halmashauri ya Jiji kuweka jalala katika eneo hilo ulihatarisha afya za watu wa eneo husika na hivyo kwenda kinyume na kifungu cha 14 cha Katiba. Kifungu hicho kinalinda haki ya mtu kuishi na kulindwa katika jamii. Festo na wenzake waliiomba Mahakama Kuu kwa mamlaka iliyonayo kisheria, kifungu 108(2) cha Katiba ya Tanzania, kufuta (to quash) uamuzi wa Halmashauri ya Jiji kufanya eneo hilo kuwa jalala. Aidha, waliiomba Mahakama hiyo itoe amri ya kuzuia (prohibition) Halmashauri hiyo kutoendelea na kazi ya kutupa takataka. Na mwisho waliiomba Mahakama hiyo kuiamrisha (mandamus) Halmashauri ya Jiji ikatafute eneo jingine la kutupa takataka zao. ( Festo Belegele na wenzake 7094, Vs DCC- High Court, Dar Es Salaam, Case No 90,1991) Mahakama Kuu ilipitisha hukumu kwa kutoa amri zote tatu kulingana na maombi ya walalamikaji. Ilikuwa ni hukumu ya kihistoria; ni aghalabu amri hizo tatu kutolewa kwa mpigo. Huenda shauri hili si geni kwa wanazuoni wanaosomea sheria. Na bila shaka limeingizwa kwenye vitabu vya sheria. Kwa bahati mbaya kabisa, katika kupanga na kutekeleza miradi mikubwa kama hii ya Kiwira, wananchi wanaweza kushirikishwa, lakini wananchi hawapewi nafasi ya kuelimishwa juu ya faida na hasara itakayowagusa wao juu ya kile kinachopangwa kufanyika. Hutokea kwa wawekezaji kuwapa wananchi mifuko ya sementi, mabati. Wanaweza pia kuwachimbia visima vya maji na kukarabati barabara zao. Itasemwa kuwa wameshirikishwa, wametaja matatizo yao, wamepewa misaada ya kijamii. Lakini, wananchi hawa hawajaelimishwa juu ya faida na hasara za mradi husika ili nao waone kama jambo hili lina maslahi kwao au la. Wanasheria na wanaharakati za kimazingira wana wajibu wa kutumia maarifa yao kuangalia kwa undani miradi kama hii, kisha wauelimishe umma. Hata kama kuna madhara makubwa kiafya na kimazingira yatokanayo na nishati ya makaa ya mawe, wananchi wa kawaida wa Kiwira hawawezi kulibaini hilo. Watafurahia tu kupewa mabati na mifuko ya sementi. Ni historia itakayowahukumu wanaharakati na wanasheria wa mazingira watakaoshindwa kutimiza wajibu wao wa kizalendo kuelimisha umma juu ya jambo hili, na kama kuna madhara makubwa yatakayowaathiri watu wa maeneo husika, basi, historia itawahukumu wasomi wetu kwa kushindwa kuzuia jambo hilo lisitokee ilihali walijua kabla. Mathalan, kitaalamu tunaambiwa uzalishaji wa megawati 200 za umeme wa makaa ya mawe ina maana pia ya kuzalisha kwa wingi hewa chafu ya ukaa (carbon dioxide) yenye madhara kwa afya ya binadamu na mazingira. Kwamba ili kupata umeme, makaa yanachomwa na kutoa hewa hiyo chafu ya ukaa. Ikumbukwe, nishati itokanayo na makaa ya mawe humu duniani ni rahisi sana na hupatikana kwa wingi, lakini ni nishati chafu sana kupindukia. Ni teknolojia ya kizamani ya kuzalisha umeme. Wanasayansi wanatwambia; kama kuna teknolojia nyingine mbadala ya kupata umeme, basi, makaa ya mawe yasitumike kuzalisha umeme. Katika nchi yetu mbali ya umeme utokanao na maji, tuna nafasi ya kutumia umeme wa jua. Umeme utokanao na gesi nao pia ni nishati safi. Wanaotetea kutumia makaa ya mawe kuzalisha umeme watadai kuna mitambo ya kusafisha hewa ya ukaa. Lakini, wataalamu wanatamwambia, kuwa hata kama kutakuwa na teknolojia ya hali ya juu katika kuzalisha umeme huo wa makaa ya mawe, lakini kamwe haiwezi kumudu kuzalisha umeme huo bila kuzalisha pia hewa ya ukaa. Asilimia 70 ya nishati iliyomo kwenye makaa ya mawe ni hewa ya ukaa. Kutokana na athari hizo mbaya za kimazingira, ni dhahiri, kaa la mawe si mgeni wa kumkaribisha tunapotafakari nishati mbadala. Kulichoma kaa la mawe kwa minajili ya kuzalisha umeme wa majumbani na viwandani ni sawa na kukichoma kizazi kijacho. Leo, tunafahamu, kuwa ulimwenguni kote, uchafuzi wa hali ya hewa unaotokana na kuchoma makaa ya mawe ni moja ya sababu za kuuongezeka kwa joto la ozoni, hali inayosababisha mabadiliko ya hali ya hewa duniani. Mathalan, mvua ya tindikali nayo husababishwa na uchomaji wa makaa ya mawe. Tunajifunza, kuwa mchakato mzima, kuanzia kuchimba makaa ya mawe, kuyasafirisha, kuyachoma na kutupa uchafu unaobakia una athari mbaya zaidi kimazingira kuliko uzalishaji wa nishati nyingine yeyote. Kwa mfano, katika hatua za kuzalisha umeme utokanao na makaa ya mawe, yanapochomwa makaa yanasababisha kuwepo kwa joto kubwa. Katika hali hiyo, hewa na maji vinapata joto kali kiasi cha maji kuchemka. Na mara maji hayo yanaporudi mtoni au ziwani yanabadili mfumo asilia wa kimazingira katika mito na maziwa hayo. Hali hii huathiri viumbe hai vya majini kama vile samaki lakini pia mimea. Kuyatayarisha makaa ya mawe pia kuna maana ya kuzalisha changarawe, vumbi na moshi. Vyote hivi vinaweza kumsababishia binadamu hali ya mwasho mwilini na hata vikohozi. Tuangalie mfano hai kutoka Zimbabwe. Miaka ile kabla ya uhuru wa Zimbabwe, nchi hiyo iliyoitwa Rhodesia ilikumbwa na vikwazo vya kiuchumi kimataifa. Haikuweza kutegemea umeme wa kutoka bwawa la Cabora Bassa kule Msumbiji. Wakaamua kuzalisha umeme kutoka kinu cha Wankie. Kinu hicho kwa sasa kimesimamisha uzalishaji wa umeme. Uzoefu wa Wankie unatuonyesha athari za kiafya na kimazingira; "Chembechembe za makaa ya mawe Wankie kimsingi ni mlundikano wa vumbi la makaa ya mawe. Na yakikaa kwa muda mrefu, milipuko ya ghafla na ya mara kwa mara hutokea. Moshi mweusi umeweza kuonekana hapa na pale. Hali hii imepelekea kuchafua hali ya hewa katika maeneo yote yenye kuzunguka kinu hicho." (D. O Hall na Y.S Mao; Biomass Energy and Coal in Africa, Uk.168) Naam, tuna lazima ya kuichunguza miradi ya umeme wa makaa ya mawe hapa nchini. Tufanye hivyo ili tuupate ukweli mzima. Huenda huko nako kuna watendaji wetu wa ngazi za juu wanaopotoshwa katika kufikia maamuzi makubwa kama haya ya kutumia makaa ya mawe kuzalisha umeme. Kama ikibidi, tunapaswa tuachane nayo, tuondoke huko kabla hatujaiingiza nchi yetu kwenye hasara kubwa. Tukumbuke, kuwa hakuna kitu kinachoitwa bahati mbaya katika matendo tunayoyafanya huku tukifahamu madhara yake. Tumesimama mbele ya historia, historia itawahukumu wote mnaonyamaza na mliofungwa midomo huku mkijua madhara yatakayosababishwa na baadhi ya maamuzi -
See more at: http://www.raiamwema.co.tz/makosa-ya-kiwira-tunayarudia-nyasa#sthash.nhwq4N0I.dpuf
0 comments:
Post a Comment