
NDANI ya daladala kutoka Posta kwenda Ubungo jijini Dar es Salaam, watu wazima wawili na kijana mmoja walikuwa wakijadiliana, hivi karibuni, masuala mbalimbali kuhusu mustakabali wa taifa letu na kurushiana wenyewe maswali.
Mmoja akamrushia mwenzake swali hili: “Kwani hata kufungua kitu kidogo tu kama soko la kata au kijiji, Kikwete (Rais Kikwete) lazima afanye yeye? Si kuna makatibu tarafa huko”?
Chanzo cha swali hilo ni redio iliyofunguliwa na daladala hilo kutangaza habari kwa ufupi za kituo kimoja che redio kwamba Rais Kikwete jana yake alikuwa amefungua soko huko Matombo alipokuwa katika ziara ya mkoa wa Morogoro.
Baada ya swali hilo kuulizwa, abiria mmoja alidakia kwa kusema: “Si Rais bwana anaweza kufanya lolote atakalo”?, na mwingine naye akakoleza: “Anataka sifa tu huyu Rais wetu”.
Maswali ya abiria hao yalinifikirisha kidogo na kunifariji ya kuwa, kumbe bado kuna Watanzania wanayaona baadhi ya mambo yanayotendwa na watawala wetu yana mushkeli, na hawasiti kueleza hisia zao hata ndani ya basi lenye abiria wengi.
Niweke wazi hapa kuwa walichokijadili abiria wale kuhusu Rais Kikwete kufungua soko pale Matombo na kusema kuwa ilikuwa ni kukamilisha alichoahidi kwenye Ilani ya chama chake CCM, ni jambo lililonikera hata mimi.
Ni uamuzi wake kufanya lolote (ili mradi havunji sheria au Katiba aliyoapa kuilinda) lakini pia ni wajibu wake na busara zake na za washauri wake kujua kuwa, kwa hadhi ya urais wananchi wanapenda asifanya baadhi ya mambo.
Kama Rais anafungua bomba la maji, darasa, kituo cha mafuta, shamba darasa, uzio wa shamba la mwekezaji, kituo cha afya, tenki la kuvuna maji na soko dogo kama ilivyokuwa Matombo, basi kuna maswali wananchi kama wale wa kwenye daladala watajiuliza.
Hivi kweli washauri wake au yeye mwenye Kikwete anapoamua kufungua soko ambalo nina uhakika sio kipaumbele cha watu wa eneo hilo la Matombo, anaitendea haki ofisi tukufu hiyo? Na anawatendea haki wale aliowateua au wanaoiwakilisha serikali yake kuanzia mwenyekiti wa mtaa, kijiji, afisa mtendaji kata, tarafa, mkuu wa wilaya, mkurugenzi mtendaji wa wilaya, afisa tawala wa wilaya na mkoa na mkuu wa mkoa; achilia mbali wakuu wa idara husika ambao humshuhudia akifanya hivyo?
Nina hakika kuwa wanapomwona Rais Kikwete anafungua soko dogo, Afisa Biashara wa wilaya na maofisa wengine wa mkoa husika hujisemea kimoyomoyo:“Hata mimi ningeweza kumwakilisha na kufungua kisoko hiki.”
Rais Kikwete asipokuwa nje ya nchi mara nyingi hufanya ziara za kukagua maendeleo mikoani. Hilo ni jambo jema. Na akiwa Dar es Salaam, hufungua makongamano na mikutano ya kitaifa na kimataifa. Hilo pia ni jambo jema, lakini hata hiyo mikutano ya ndani na nje, kuna wakati wananchi wangependa asifanye yeye kazi hiyo bali wasaidizi wake.
Ana hiari kufanya yeye au wawakilishi wake. Nani atamlazimisha Rais afanye hili au lile? Lakini kama abiria wale ndani ya daladala walivyozungumza, kuna uzinduzi ambao ukifanywa na Afisa Mtendaji wa Kata au Katibu Tawala au hata DC, inaleta mantiki zaidi kuliko uzinduzi huo ukifanywa na Rais. Isitoshe, wao wana muda zaidi wa kufuatilia miradi hiyo kwa kuwa iko maeneo yao ya kazi kuliko ilivyo kwa Rais.
Labda niseme hivi: Baada ya kuizunguka Tanzania nimebakiza wilaya mbili tu nchini kuzifikia, Ileje na Pangani. Wilaya zote zaidi ya 133 nimeshafika kikazi. Na jambo moja ninaloweza kuthibitisha ni kuwa katika vijiji vingi hapa Tanzania, kuna miradi ya masoko ya kuuza bidhaa yaliyojengwa ama kwa fedha za ufadhili au kwa kulazimisha wananchi husika kunakofanywa na watendaji wa halmashauri za wilaya.
Ndiyo maana naweza kusema kuwa, zaidi ya asilimia 80 ya masoko hayo hayatumiwi na wananchi wa eneo husika. Wao huendelea kuuza bidhaa zao kwa staili na maeneo waliyoyazoa na yanayofikiwa na wateja wengi.
Kwa maneno mengine, soko sio kipaumbele cha wananchi wa vijijini. Ni kipaumbele cha Halmashauri za Wilaya kwa sababu ya urahisi wa kukusanya kodi; huku nyingine zikiwa ni za dhuluma kwa wananchi.
Msomaji unaweza kufanya uchunguzi kidogo tu unapokuwa likizo kijijini kwako ambapo soko kama hilo alilofungua Kikwete Matombo limejengwa. Waulize wananchi nini vipaumbele vyao. Soko litakuwa namba 10 au zaidi katika vipaumbele vyao likitanguliwa na maji, kituo cha afya kuwa karibu nao, pembejeo na mbegu bora kwa wakati, dawa na majosho ya mifugo yao na barabara, kero za ardhi au usafiri. ‘Kubwa lao’ ni rushwa na ufisadi katika maeneo yao.
Watakuambia wangetamani kila darasa katika shule yao ya msingi liwe na madawati ya kutosha watoto wote ili pasiwepo na mtoto anayekaa vumbini; huku mwalimu akipinda mgongo kumsaidia kuandika.
Soko la nini hasa unaposikia kuwa nchi inahitaji madawati milioni 1, 147,471 na wakati huo huo shule ya Msingi ya Chemchem, Tabora mjini, mwalimu mmoja anafundisha wastani wa watoto 204?!
Hebu chukulia mfano wa Tarime. Taarifa za hivi karibuni za vyombo vya habari zinasema kuwa shule za msingi za Kegonga (wanafunzi 512) na Nyantage (Watoto 684) zimelazimika kufungwa kutokana na kukosa vyoo hata vya mashimo.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, jamii zimo katika pilikapilika za kujenga vyoo vya mashimo ili shule zifunguliwe katikati ya Septemba. Cha ajabu, watu watakwenda Tarime kufungua tamasha la fiesta au la miziki ya bongo fleva wakati vipaumbele vya wilaya ni watoto kwenda shule!
Tuulizane: Soko la nini hasa wakati zahanati tu pale Matombo haina dawa kwa wazee, na hata Bima ya Afya haikusaidii kuokoa pesa maana unaambiwa ukanunue kwenye maduka ya dawa!
Ninaandika haya nikijua fika kuwa hata ule mpango wa maboresho ya serikali za mitaa uliofadhiliwa kwa mapesa mengi na nchi za Uingereza (kupitia shirika lake la maendeleo la DfID) na zile za Scandinavia wa kuwezesha wananchi kupanga mipango yao badala ya kupangiwa kutoka juu, sasa hivi haina tija tena.
Hivi sasa mipango hiyo imo kwenye makaratasi na kompyuta tu. Zi wapi enzi za Upangaji Mipango kwa Kuangalia Wananchi Wanasemaje Kuhusu Fursa na Vikwazo (Opportunities and Obstacles for Development - O &OD)?
Huwezi kusema wananchi wa Matombo au Ruvu Darajani mkoa wa Pwani au wa kijiji cha Mngeta wilayani Kilombero wangetamani soko kwanza kabla ya kuwepo kwa dawa katika zahanati yao au kujengwa barabara ya kokoto au daraja la mto Kilombero ambalo juzi Rais Kikwete alisema litakamilika kujengwa ikiwa ni mara ya kumi kutamkwa hivyo tangu kupata Uhuru .
Hata Wasukuma na Wamasai walioingia kwa wingi wilayani Ulanga na Kilombero wasingeweza kutaja soko kuwa ni kipaumbele chao, na badala yake wangetaja majosho na maeneo ya malisho ya mifugo yao.
Hata huko walikotoka kabla ya kuingia wilaya hizo mbili hawakuwa na masoko yaliyojengwa bali walikuwa na maeneo ya gulio mara moja au mbili kwa wiki kunadi mifugo na mazao mbalimbali.
Kama wananchi wanakutana mara moja kwa wiki kununua na kuuza mazao na mifugo yao, nani anawalazimisha wajenge masoko kama kipaumbele chao?
Ndiyo maana mengi ya masoko hayo kama lile la kijiji cha Mngeta au Ruvu Darajani ambako viongozi wengi hupita wanapokwenda Morogoro, sasa ni sawa na kile Waingereza wanachopenda kukiita ‘white elephant’; yaani majengo makubwa kama tembo lakini yasiyo na tija kwao!
Nijuavyo, Watanzania wengi wameshaandika na kutoa shauri wao kwa Rais Kikwete na wasaidizi wake kuhusu mazoea ya viongozi wakuu kuzindua au kushikia bango mambo ambayo kwa hakika yangetosha sana kufanywa na walio chini yao - tena kwa ufanisi sana, lakini ushauri huo hauthaminiwi, na ndiyo maana tabia hiyo inaendelea kama ilivyotokea majuzi huko Matombo.
Ingawa hakuna takwimu sahihi kujua ni kwa kiwango kipi marais wanne tuliokuwa nao tangu kupata uhuru wamefungua majengo mangapi ya vimiradi vidogo badala ya uzinduzi huo kufanywa na wasaidizi wao, lakini nina hakika idadi itakuwa kubwa.
Tuambizane ukweli. Kote duniani Rais ni mtu bize sana katika kufikiria, kubungua bongo kuhusu nini atawafanyia wananchi wake kutokana na kupewa uwezo na nguvu kikatiba ili kuwatoa hapo walipo na kuwasogeza mbele.
Kijisoko kidogo ambacho wala si kipaumbele cha wananchi hakiwezi kuwasogeza mbele kimaendeleo. Kama nakosea, nakupa changamoto uwaulize wananchi wa Matombo, Kibaigwa, Ruvu Darajani, Mngeta na kwingineko, kama soko lililozinduliwa maeneo hayo limesaidia kupunguza umasikini wao.
Nihitimishe kwa kusema kwamba, Watanzania wanahitaji na wanapenda kumwona Rais Kikwete akiwa bize kutafuta ufumbuzi wa matatizo yanayofukarisha wananchi na kufanya maamuzi magumu yenye maslahi kwao, na sio kuzindua vijimiradi vidogo vinavyoweza kuzinduliwa hata na DC tu!
Kikwete anayoa orodha ndefu ya maamuzi maguu anayopaswa kufikiria kuyachukua kama vile kupunguza bei ya pembejeo kwa serikali kutoa ruzuku au kufidia kiasi fulani cha gharama, kupunguza bei ya saruji na mabati, kuondoa michango ya lazima ya Sh. 20,000 kwa watoto wa shule za msingi nk.
Hayo ni baadhi tu ya mambo mengi ambayo wananchi wangependa kuyaona Rais akishughulika nayo , na si kufungua miradi hii midogo ambayo wala si kipaumbele cha wananchi.
Hatumpangiii wala kumfundisha Rais cha kufanya; maana ana wasaidizi wake, lakini tunaposikia malalamiko ya wananchi kwenye daladala au majumba ya ibada au vijiweni, tunalazimika kupaza sauti ili wenye masikio makubwa na mdomo mdogo wasikie!
Ni matumaini yangu kuwa wanaomshauri Rais Kikwete wataupata ujumbe huu na kumshauri ipasavyo; maana hatumtarajii rais wa nchi kupigana vibega na wasanii katika misiba ya kawaida au sherehe na wala hatumtarajii siku moja kuzindua albamu za wanamuziki wa bongofleva!
Hata enzi za Mwalmu Nyerere walikuwepo wasanii nyota kama vile mzee Makongoro, Mwinamila au waimbaji nyota wa taarab kama Shakila au wanamuziki waliobobea wa kipaji cha Mbaraka Mwinshehe (soloist nationale), lakini hatukupata kuona wakiitwa Ikulu na kuandaliwa karamu huku wakipiga picha na Rais.
Hatukuona hayo, kwa sababu Nyerere alikuwa mtu bize akiyashughulikia matatizo ya kimsingi ya Watanzania wengi; hususan wafanyakazi na wakulima masikini.
-
See more at: http://www.raiamwema.co.tz/wameshindwa-kumshauri-kikwete-vipaumbele-uzinduzi-wa-miradi#sthash.EkaqDLvM.dpuf
0 comments:
Post a Comment