GESI inatoka au haitoki? Swali maarufu sana lilizuka wakati ule wa vurugu kubwa zilizotikisa mkoani Mtwara. Wale wanaojiita wananchi wenye uzalendo na uchungu na maliasili yao katika mkoa huo wakawa wanatumia swali hilo kuwajua waliitwa wasaliti ambao wanataka maliasili yao itoke.
Mtu akienda kununua sigara, sukari au bidhaa nyingine katika duka, salamu atakayokutana nayo ni gesi inatoka au haitoki kujua msimamo wa mteja kama unaendana na mwenye duka.
Ikawa salamu ya kinafiki hata wale ambao hawakuamini katika uchoyo uleo wa wale waliojiita wazalendo na wachungu wa rasilimali yao, katika kuepuka wasiwaudhi wazawa au biashara yao isiharibiwe na hao waliojiita wazawa wanajikuta nao wanajibu haitoki.
Gesi haitoki ukawa wimbo ukaimbwa na idadi kubwa ya wana Mtwara, lakini baada ya kuelimishwa na Serikali yetu baada ya rabsha zile hatimaye walikubali na leo hii wimbo unaimbwa kule ni gesi inatoka.
Ni baada ya elimu wananchi wakaelewa faida za gesi hiyo kwa uchumi wa taifa, wamegundua kwamba walichokuwa wanakifanya hakikuwa na haki kwa Watanzania wenzao na leo hii taifa tunaimba wimbo mmoja kwamba gesi inatoka.
Ndivyo ilivyo leo hii katika wimbo wa Muungano, wimbo unaoimbwa na Watanzania wote ni serikali mbili au serikali tatu. Ni wimbo unaiombwa na vyama vya siasa na wimbo unaiombwa na wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba.
Wimbo huu umekuwa maarufu sana; lakini tupende tusipende kila mtu ana mtazamo tofauti lakini kuna watu wanataka tuimbe wimbo mmoja tu jambo ambalo halikubaliki.
Wale wanaotaka serikali tatu wanataka kuwalazimisha na wengine nao waimbe wimbo huo kwa sababu tu wao wanauimba. Wanao na kwamba wale ambao hawaimbi wimbo huo si wazalendo kwa taifa lao.
Wameanza kuwabatiza majina hao wasiokubaliana nao kuwa ni kasuku wanaofuata bendera fuata upepo. Wanashindwa kuja na hoja za kuwashawishi wasiokubaliana na mfumo huo ili wawaunge mkono. Vivyo hivyo wale wanaopigia upatu serikali mbili nao wanawaona wale ambao wanataka serikali tatu kuwa ni wasaliti na kwamba wanatumiwa na wapinzani. Kwao wao wale wanaotofauatiana nao kimtazamo wanawaita wapinzani na wanawachukulia kwamba sio Watanzania kwa vile mawazo yao mbadala ni ya usaliti na kwamba hayana chembe hata ya uzalendo kwa taifa lao.
Wanajiona wao ndio wana mawazo sahihi kwa mustakabali wa taifa leo. Waumini wa serikali mbili wanawasonda vidole wenzao kwamba wanataka kuvunja Muungano wetu uliodumu kwa miaka 50 sasa.
Lakini wote tumemsikia mzee Jaji Warioba kaja na malalamiko ya kila upande haya ndio tunatakiwa kujibiwa ili Muungano wetu uende mbele zaidi.
Kama tuna uchungu kama wangu ni heri twende kwenye serikali moja, Wazanzibari waonje uchungu walionja Watanganyika kuua utambulisho wao ili wote tuwe Watanzania. Hilo ugumu wake uko wapi?
Uzanzibari na Utanganyika utatusaidia nini wakati huu? Naamini tusipoenda katika serikali moja siku zote Muungano wetu utakuwa wa kusuasua tu.
Tuache unafiki na ubinafsi kila upande ukubali kupoteza tuunde katiba nzuri yenye nchi moja serikali moja na sio nchi mbili serikali mbili au serikali mbili nchi moja.
 
src
Habari Leo

0 comments:

Post a Comment

 
Top