NAMBIE mdau mambo vipi, wanasemaje waungwana hapo, mambo yanaenda au kila kukicha afadhali ya jana? Namshukuru Mungu kwa yote, sitachoka kuomba baraka zake sanjari na msamaha ninapotenda kinyume na anavyotaka yeye. Nimezungumzia msamaha kwa kuwa naamini si tu ni muhimu katika uhusiano wangu na yeye lakini pia, katika uhusiano wangu na wanadamu wengine.
Ni kwa kuzingatia hilo, nawapongeza wote wanaowasamehe kwa dhati waliowakosea. Ethel Ngwenya (50) wa Old Lobengula nchini Zimbabwe ni mfano wa hao, kamsamehe mumewe anayedaiwa kumuambukiza mama huyo virusi vinavyosababisha Ukimwi(VVU).
Awali, mwanamke huyo alimshitaki mumewe, Gilbert Mpofu, mahakamani kwa kumuambukiza kwa makusudi HIV, lakini sasa kaamua kufuta mashitaka hayo kwa kuwa, mwanamume huyo ameahidi kumtunza hadi atakapoaga dunia.
Septemba mwaka jana, Ngwenya alitoa taarifa Polisi kuhusu suala hilo baada ya kwenda kupima na kuonekana ana VVU na akaeleza kuwa, mwanamume huyo mkazi wa kitongoji cha Sikobokobo kilichopo Nkayi nchini humo kuwa kamuambukiza kwa makusudi walipofunga ndoa mwaka 2007 kwa kuwa hakumweleza kuwa ni muathirika na wakafanya tendo la ndoa bila kutumia kinga.
Mpofu katumia busara kukiri kosa kwa mkewe, na mwanamke huyo amekuwa mfano wa namna mtu anavyoweza kusamehe jambo kubwa kama hilo.
Nawapongeza hao lakini namlaumu Maxwell Jairos mkazi wa Harare, Zimbabwe, kwa kumlazimisha mkewe wafanye tendo la ndoa bila kutumia kinga wakati anafahamu kuwa wote wana VVU.
Tunapaswa kumtumia Jairos kuwa ni mfano hai wa watu wanaokiuka kwa makusudi masharti ya tiba hivyo kutoa fursa kwa VVU ama kuwa sugu au kupata maambukizi mengine na kuongeza kasi ya kupungua kwa kinga ya mwili.
Mwanamume huyo analazimisha kujamiiana bila kinga kwa madai kuwa na mzio (aleji) na kondom! Sababu anazotoa mwanamume huyo kuwa, kondom zinaathiri uume wake si za msingi kuliko kulinda afya yake na ya mkewe, Esther Chingondo.
Nampongeza mwanamke huyo kwa kuthamini afya yake, si tu kwa kukataa kujamiiana na mumewe bila kondom, lakini pia kwa kupeleka suala hilo mahakamani.
Kesi hiyo kwenye mahakama ya kiraia ina mafunzo mengi, wanaume wanapaswa kuwaheshimu wenzi wao, Jairos, hakuwa muungwana kwa kumtukana mkewe kwa sababu tu kanyimwa unyumba, na pia kitendo cha mwanamume huyo kutumia mkasi kuchana nguo ya ndani ya mkewe si cha kistaarabu na ni ukatili.
Tendo la ndoa ni la kistaarabu, ni la furaha, linahitaji ridhaa ya mume na mke kulifanya, na endapo litafanywa kwa kulazimisha, kwa kuchana nguo ya ndani ili ufanye wakati mwenzako hataki inakuwa ni sawa na kumbaka.
Si hivyo tu, mtu anayeishi na VVU anapaswa kutekeleza maelekezo ya daktari ikiwa ni pamoja na kutoacha kutumia dawa za kupunguza makali ya VVU, ARV’s, kuacha kutumia dawa hizo kwa madai kuwa, zinaathiri ngozi yako ni kuviwezesha virusi kuwa sugu na kuhatarisha maisha yako.
Niliwahi kusema na ninarudia, Mungu kampa mwanadamu zawadi ya uhai na uwezo wa kufahamu mema na mabaya, utashi wa kuamua afanye nini, wapi, wakati gani, tuna uhuru wa kujilinda au kujiangamiza, hapendi tuangamie lakini hapati hasara tukifa. Popote unapomuabudu, tambua thamani ya uhai wako, ukiupoteza haurudi tena.
Viongozi wa dini watusaidie kutuimarisha kiimani badala ya kutupotosha. Waumini pia wanapaswa kuwa makini, hivi sasa kuna makanisa mengi yanayotumia Biblia kupotosha.
Ipo mifano hai ya uovu huo, kuna taarifa zinazodai kwamba, Mchungaji Njohi wa Kanisa la Propeller Redemption nchini Kenya ameamuru waumini wanawake wasivae nguo za ndani na sidiria ili miili yao iwe huru kumruhusu Yesu aingie kwenye maisha yao.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, mchungaji huyo kawaeleza waumini hao kuwa, kuvaa nguo ya ndani kanisani ni kumkosea Mungu, imetungwa sheria inayozuia wanawake wanaosali kanisani hapo kuvaa nguo hizo kwa maelezo kwamba, unapoenda kanisani lazima mwili uwe huru ili kumpokea Kristo! Inasikitisha kwamba, waumini wanawake wanatekeleza amri hiyo, wanakwenda uchi kanisani.
Sioni uhusiano wa mtu kuwa uchi na utayari wa kumpokea Kristo, na nadiriki kusema kuwa, mchungaji huyo, analidhalilisha neno la Mungu, anawadhalilisha wanawake, ana mapepo, na aogopwe kama ukoma.
Siku njema. bmsongo(at)hotmail.com
src
Habari Leo
0 comments:
Post a Comment