MSHAMBULIAJI wa Yanga, Emmanuel Okwi, juzi Jumamosi alikuwa katika wakati mgumu baada ya kuvamiwa na mashabiki wa soka kwenye Uwanja wa Ally Hassan Mwinyi mjini hapa, hali iliyosababisha ashindwe kupumua vizuri.
Kitendo hicho kilitokea baada ya kumalizika kwa mechi kati ya timu yake na maafande wa Rhino ya mkoani hapa ambapo maafande hao walikula kichapo cha mabao 3-0.
Baada ya mwamuzi kupiga kipenga cha kumaliza pambano hilo, kundi la mashabiki lilimvaa mchezaji huyo na kumfanyia fujo.
Wengine walikuwa wakimkumbatia na wengine kumdandia na kutaka kumwangusha ndipo mchezaji huyo aliyeonekana kuchoshwa na dakika tisini za kusakata kabumbu, akaanza kunyoosha mikono kuomba msaada.
Askari ambao walikuwa nje ya eneo la kuchezea, baada ya kuona hali inakuwa mbaya kwa mchezaji huyo wa zamani wa Simba, walivamia uwanjani na kuwasambaratisha mashabiki hao kwa kutumia virungu na mbwa ili kumuokoa.
Baada ya kumuokoa, walimshika na kumpeleka walipokaa wachezaji wenzake ndipo alionekana kupumua kwa kasi kama mtu aliyetoka kwenye dhoruba.
Akizungumza na Championi Jumatatu, Okwi alisema huenda mashabiki hao hawakuwa na nia mbaya lakini hawakujua kama walikuwa wakihatarisha usalama wake baada ya kukosa hewa.
“Kwa kweli nilikosa hewa, ilikuwa hatari lakini siwalaumu mashabiki, hawakuwa na nia mbaya nami, walitaka kunisalimia, sema wingi wao ulinipa shida kidogo,” alisema Okwi.
Okwi ametokea kuwa gumzo kwa mashabiki wengi wa soka nchini tangu alipojiunga na Yanga akitokea SC Villa ya Uganda katika usajili uliokuwa na utata hadi Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) kulazimika kushirikishwa.
Utata ulitokana na kitendo cha Villa kumuuza wakati ikidaiwa timu iliyokuwa inammiliki ni Etoile du Sahel ya Tunisia ambayo bado mpaka leo haijailipa Simba fedha zake dola 300,000, zaidi ya Sh milioni 480 za usajili kutoka Msimbazi.
Mashabiki wa Yanga wamekuwa wakimfurahia kila wanapomuona baada ya kuruhusiwa kucheza, lakini wale wa Simba ni kama amegeuka kuwa adui kwao.
Mganda huyo aliichezea Simba kwa mafanikio na aliiwezesha kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu wa 2011/12 huku mwenyewe akitupia mabao 12 na alikuwemo kwenye kikosi kilichoifunga Yanga mabao 5-0 Mei 6, 2012 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar, akitupia bao moja dakika ya 62
0 comments:
Post a Comment