Mapato na mgawanyo wa Mapato ya Muungano katika Serikali Tatu
Rasimu ya Katiba imependekeza kuwa ushuru wa forodha na mapato kutoka Mashirika ya Muungano ndiwe fedha za muungano. Ninaamini kabisa kwamba Tume ya Katiba haikupata ushauri mzuri kuhusu suala hili. Kwa uzoefu wangu kama Waziri Kivuli wa Fedha, vyanzo hivyo havitoshi kuendesha DOLA. Dola inapasa kuwa na rasilimali za kutosha na ziada inaweza kugawa kwa washirika na mikoa katika wajibu wa kuhakikisha maendeleo yanawiana. Dola pia inaweza kuwa na miradi ya Muungano. Vile vile, hayo Mashirika ambayo Tume inasema ni yepi maana muungano umependekezewa masuala saba tu. Kuna haja ya kuangalia kwa umakini mkubwa suala hili kama kweli kuna nia ya dhati ya kuendelea kuwa na Muungano. Mapendekezo yangu ili yafanyiwe kazi ni haya.
Mapato ya Muungano
1. Ushuru wa Forodha
2. Mrahaba wa uvunaji wa Rasilimali ambapo 25% itabaki kwenye mkoa wenye rasilimali na 75% itatumika na Serikali ya Muungano kugawa kwenye mikoa kwa mujibu wa ‘formulae’ itakayokubaliwa kwa kuzingatia idadi ya watu, kiwango cha umasikini na ukubwa wa kijiografia.
3. Ushuru wa Bidhaa ambapo 60% itagawiwa kwa nchi washirika kwa ajili ya miradi maalumu.
4. Mapato kutoka kwenye kampuni za kibiashara za Serikali ya Muungano na gawio la Benki Kuu ya Tanzania.
Mapato ya Serikali za Washirika
1. Kodi ya Mapato ya watu binafsi na Makampuni
2. Kodi ya Ongezeko la Thamani au kodi kama hiyo
3. Tozo mbalimbali zitakazotungwa kwa mujibu wa sharia
4. Mapato yasiyo ya kikodi kutoka idara na Wizara za Serikali.
Mapato ya Mikoa
1. 25% ya Mrahaba kutokana na uvunaji wa Rasilimali/maliasili inayopatikana katika mkoa husika
2. 10% ya makusanyo ya kodi ya mapato ya watu binafsi na makampuni kutoka katika mkoa husika
3. Mgawo kutoka Serikali ya Muungano
4. Mgawo kutoka Serikali ya Washirika
5. Tozo mbalimbali zitakazoanzishwa kwa mujibu wa sheria ndogo ndogo zitakazopitishwa na Mabaraza ya Mikoa

0 comments:

Post a Comment

 
Top