Dodoma. Mjumbe wa Bunge la Katiba, Kingunge Ngombale Mwiru, ameishambulia Rasimu ya Pili ya Katiba iliyowasilishwa na Jaji Joseph Warioba kwa kusema “imejaa maneno ya kugawana vyeo kwa watawala”.
Kingunge alitoa kauli hiyo mwishoni mwa wiki wakati akichangia katika mjadala wa masuala ya elimu ya historia ya Katiba ya nchi ya Kenya ambayo iliwasilishwa na Seneta Amos Wako.
“Kuna tofauti kubwa za kiuchumi kati yetu na wale waliotutawala. Tatizo letu sisi tunaandika Katiba ambazo hazina msingi wa kiuchumi ndani yake, badala yake zinakuwa na mwelekeo wa kugawana vyeo kama njugu,” alisema Kingunge huku akishangiliwa na umati wa wajumbe kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Alisema kuwa nchi nyingi za Kusini mwa Afrika bado ziko nyuma kiuchumi na maendeleo ya jamii na kwa sehemu kubwa bado ni tegemezi ya mataifa makubwa.
Kwa mujibu wa Kingunge, Katiba nyingi za Afrika alizokwishaziona zinazungumzia suala la kugawana madaraka na katiba hizo hazina tofauti na Rasimu ya Katiba inayopitiwa sasa na wajumbe wa Bunge la Katiba. Aliitaka Katiba Mpya ieleze namna ya kusukumu mbele masuala ya kimaendeleo na uchumi wa Watanzania pamoja na kuzungumzia maslahi ya wafugaji, wavuvi na wakulima, ikiwamo watumiaji wengine wa ardhi.
Akizungumza katika suala hilo, Wako alikiri kuwa Katiba ndiyo dira ya maendeleo katika nchi yoyote ambayo inaheshimu utawala wa kidemokrasia.
Hata hivyo, alipingana na mwanasiasa huyo kwa maelezo kuwa katiba ndiyo kila kitu hivyo suala la kueleza masuala ya utawala na jinsi ya kugawana vyeo sio tatizo, muhimu ni kuingiza vitu vitakavyoruhusu kuwepo na dira za kimaendeleo.
Alimtaka Kingunge kutumia nafasi aliyopewa na Rais kuingiza mambo ya uchumi na maendeleo katika rasimu ili yasaidie kuharakisha uchumi ingawa alisisitiza kuwa suala la kugawana vyeo haliwezi kukwepeka.
0 comments:
Post a Comment