Jay Dee 


Giza nene bado limetanda kwa wasanii kuhusu hakimiliki ya kazi zao kutokana na Chama  cha Hakimiliki Tanzania (Cosota), kukiri wazi kwamba wameshindwa kukusanya mirahaba ya wasanii kupitia vyombo vya matangazo, zikiwemo redio na televisheni, kutokana na kukosa mitambo ya kisasa ya kufuatilia kazi hizo.

Vyombo hivi vya matangazo vimeshindwa kuwalipa wasanii, lakini hivi sasa vimekuwa vikiongoza kuwatoza wasanii fedha ili kazi zao zipate kusikika redioni au video zao kuonekana hadharani. Hata hivyo, wasanii nao wamekuwa wakilipia fedha nyingi ili  nyimbo zao zipigwe na kufahamika kwa mashabiki, kwa lengo la kupata shoo ambazo ndiyo malipo ya kazi zao.

Kinachowaingizia fedha wasanii wa sasa ni kupitia shoo, mfumo ambao umekuwa ni ‘mama’ katika mataifa mengi duniani. Shoo ndiyo msingi pekee kwa msanii, hii inamaanisha nini?

Iwapo msanii atachuja na nyimbo zake kuendelea kupigwa redioni na hata video zake kuendelea kuchezwa kwenye vituo vya televisheni, inamaanisha kwamba hatakuwa na stahili yoyote anayoipata kupitia jasho lake, ilhali chombo cha habari husika kinaingia fedha kupitia matangazo mbalimbali.
Akizungumza na gazeti hili, Mwanasheria wa Cosota, Maureen Fondo Jandwa anasema mpaka sasa kuna kituo kimoja tu cha redio kilichopo mikoani, ndicho kinacholipa mirabaha kwa wasanii ambapo hata hivyo ni kiasi cha shilingi laki tano tu kwa mwaka.

“Licha ya kwamba Cosota hatuna mitambo ya kurekodi lakini sheria ya leseni kwa vyombo vya utangazaji wa kazi za wasanii ya mwaka 2003, imepitwa na wakati hivyo kwa sasa tunasubiri mchakato wa sheria mpya ili wasanii waweze kunufaika,” anasema Jandwa huku akifafanua kuwa wasanii wanalipwa mirabaha inayotokana na kazi mbalimbali zilizorekodiwa kupitia Juck Box na kwenye kumbi za starehe na bado kuna utata katika maonyesho ya umma na vyombo vya utangazaji.

Anasema kwa muda mrefu sasa kumekuwa na mazungumzo kati ya vyombo vya habari na Cosota ambapo wamiliki wamekuwa wakionyesha nia ya kulipa mirabaha.

“Bado vyombo vya habari havijaanza kulipa mirabaha, hivi sasa tupo kwenye mazungumzo na wamiliki wa vyombo hivi na wengine wameonyesha nia ya kufanya hivyo kwa kutoa mwongozo mbalimbali njia zipi zitumike katika kulipa mirabaha,” anasema Jandwa na kuongeza kuwa wameshakaa vikao mbalimbali kuhakikisha suala hilo linakamilika kwa uharaka zaidi.

Kauli ya Cosota inatofautiana na ile ya wasanii ambapo Rais wa Shirikisho la Muziki Tanzania, Ado Novemba, yeye anasema wasanii hasa wa muziki wanahitaji kuonana na Rais Jakaya Kikwete ili kuweza kukamilisha mchakato wa haki za wasanii hasa kuhusu mirabaha kabla hajaondoka madarakani mwaka 2015.
“Rais JK ndiye aliyetusaidia wasanii mpaka kufika hatua hii tuliyopo sasa, tunamwomba tena kwa mara nyingine akutane na sisi ili tuweze kumweleza mapungufu yaliyopo katika sanaa yetu, kwani kuna watu wanamzunguka, kwa kufanya hivyo ataweza kukamilisha kile alichokianzisha kabla hajaondoka madarakani mwaka 2015, kwani hatujui kama ajaye atakuwa na mapenzi na wasanii,” anasema Novemba. Anasema japokuwa wanapokea mirahaba lakini ni kwa kipindi cha miezi sita huku msanii mmoja akiambulia kiasi cha shilingi 60 elfu licha ya kwamba wimbo wake au filamu yake imeonyeshwa mara nyingi zaidi katika maonyesho ya wazi.

“Kiasi tunacholipwa kama mirabaha ni kidogo bado kuna mabasi ambayo yanatumia kazi hizi za wasanii, lakini hayalipi yaani kuna utamaduni ambao ulianzishwa na bado unaendelezwa mpaka leo. Hata kwa watu wa vyombo vya habari Cosota wanasema hawana mitambo ya kurekodi lakini mbona TCRA waliwaambia warekodi uwezekano upo ila imefanywa kuwa mazoea,” alisema na kusisitiza kuwa bado wizi wa kazi za wasanii unaendelea kufanya na hata kampuni za simu kwani bado zimekuwa zikiwanyonya wasanii kwa kukata asilimia kubwa katika malipo ya miito ya simu.

“Kilio kikubwa zaidi ni kuhusu stika za TRA kwani mpaka sasa bado mchakato huu haueleweki, kazi zilizokuwepo awali walisema kwamba zingeondolewa lakini mpaka sasa bado hazijaondolewa na bado ulipaji wa stika hizi ni wa kiholela sana,” alisema Novemba
Rais wa Shirikisho la Filamu Tanzania (TAFF), Simon Mwakifamba anasema bado Cosota inahitaji mbinu za kisasa kukusanya mirabaha ya wasanii ili waweze kufikia hatua ile waliyostahili sambamba na kupata kiinua mgongo kupitia kazi zao walizozifanya kipindi wana nguvu.

Mwakifamba anasema Serikali inatakiwa kuwa ya kwanza kuonyesha mfano sasa na iwapo mwaka ujao 2015 utapita basi wasanii watakuwa katika nafasi ambayo si nzuri kwa wao wenyewe.

“Tunamwomba Rais akae na sisi wasanii ili tuweze kutoa madukuduku yetu hatumjui ajaye atakuwaje, Rais wetu Kikwete amekuwa na upendo mkubwa sana kwa wasanii mpaka hapa tulipofika ni kwa juhudi zake, bila shaka mwaka 2005 hatukua hapa tulipo tunashukuru kwa hilo lakini lazima ahakikishe ametuacha vizuri,” anasema Mwakifamba.

Anasema “Mirabaha ya wasanii iwe kama chachu ya wengi wetu kufanya kazi kwani iwapo itasimamiwa kwa umakini itageuka fursa na ajira kwetu kuliko ilivyo sasa. Wazee wengi wakiwamo kina Maalim Gurumo, kina mzee Bakari Mbelemba ‘Jangala’ na wengine wengi wamekuwa kwenye sanaa kwa kipindi kirefu lakini hakuna malipo yoyote wanayoyapata, lakini hata Gurumo hapati Mirabaha inayotokana na kazi zake zinazopigwa leo hii kutokana namfumo uliopo,” anasema.
Mkurugenzi wa Idara ya Utamaduni katika Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo, Profesa  Hermans Mwansoko, alisema suala la mirabaha ya wasanii  lipo chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara.

Naye Waziri wa Viwanda na Biashara Abdallah Kigoda alisema ameshatoa maagizo kwa Cosota, nini cha kufanya kuhusu suala la mirabaha kwa wasanii.

“Nilishatoa maagizo Cosota na mpaka sasa wameshafanya vikao kadhaa na wasanii pamoja na wanamuziki kutafakari. Nawahakikishia kwamba Wizara yangu kwa kushirikiana na Wizara ya Habari Utamaduni na Michezo na Cosota tutahakikisha wasanii wanalipwa mirahaba ya kazi zao,” alisema

src
mwananchi


0 comments:

Post a Comment

 
Top