Na Baraka Mpenja,
Dar es salaam
KUELEKEA katika
mechi ya keshokutwa ndani ya dimba la Taifa, jijini Dar es salaam baina ya
mabingwa watetezi wa ligi kuu soka Tanzania bara, Young Africans dhidi ya makamu
bingwa kwa misimu miwili mfululizo, Azam fc wana Lambalamba mashabiki, viongozi
na mabenchi ya ufundi yamepandwa na homa kali.
Azam fc waliopo
kileleni wakiwa na pointi 43 wapo katika mipango kabambe ya kuhakikisha wanapata
ushindi mbele ya Yanga inayotajwa kuwa na kikosi bora zaidi msimu
huu.
Ni kweli Yanga msimu
huu imesheheni majina ya wachezaji wenye mvuto zaidi nje ya uwanja, japokuwa
ndani ya uwanja bado kuna matatizo ndani ya kikosi chao.
Ukitaja majina kama
vile Emmanuel Anord Okwi, Hamis Friday Kiiza `Diego`, Didier Kavumbagu `Kavu`,
Mrisho Khalfan Ngasa `Anko`, Simon Msuva , Said Bahanuzi, Jeryson John Tegete
ambao huongoza safu ya ushambuliaji, hakika utahofia unapoingiza uwanjani kikosi
chako cha bei `chee` .
Pia ukija dimba la
kati, unakutana na mafundi, Haruna Niyonzima `Fabregas`, Frank Domayo `Chumvi`,
Athuman Idd `Chuji` , Hassan Dilunga na wengineo ambao hawana namba za kudumu
katika kikosi cha kwanza.
Nayo safu ya ulinzi
imesukwa kwa mabeki visiki wakiwemo Kelvin Patrick Yondan, Nadir Haroub
`Canavaro`, Mbuyu Twite, Oscar Samwel Joshua, David Luhende na
wengineo.
Ukiangalia tofauti
ya majina baina ya Yanga na Azam fc, Wanajangwani ni chama kubwa zaidi kwa maana
ya kuwa na mtaji mkubwa wa wanachama, mashabiki na hata ukongwe wa ligi kuu soka
Tanzania bara.
Ukija katika
mipango, uwekezaji, hapo unaleta habari nyingine. Azam fc wameipiga bao Yanga
kwa asilimia kubwa.
Wakati mashabiki
wakisubiri mechi hiyo kwa hamu kubwa, tayari kikosi cha Yanga kimeingia chimbo
maeneo ya Bagamoyo, Mkoani Pwani kujiwinda na mechi hiyo ya kesho
kutwa.
Taarifa za uhakika
kutoka ndani ya Yanga zinasema kuwa kipa namba moja wa klabu hiyo aliyekosa
mchezo wa jumamosi dhidi ya Mtibwa Sugar ulioishia kwa suluhu ya bila kufungana,
Deogratius Munich `Dida` anaweza kurejea uwanjani kufuatia kuendelea vizuri
baada ya kuumia katika mazoezi wiki iliyopita.
Naye Mrisho Ngasa
aliyeumia katika mchezo wa machi 9 mjini Alexndria dhidi ya Al Ahly ambapo
Yanga walitolewa kwa penati 4-3 anaendelea vizuri ingawa bado hakuna uhakika
kama anaweza kutumika mechi ijayo.
Hata kama `Dida`
hatakuwepo katika mchezo wa kesho kutwa, bado nafasi yake itaweza kuzibwa na
makipa waliopo, Juma Kaseja na Ally Mustapha `Bartez`.
Kaseja aliyesajiliwa
maalum kwa mechi za kimataifa, alikosa mechi tatu za ligi ya mabingwa barani
Afrika.
Alikosa mechi ya
marudiano dhidi ya Komorozine mjini Moroni, na akakosa mechi mbili dhidi ya Al
Ahly.
Lakini jumamosi
kwenye mchezo wa Mtibwa Sugar, Kaseja alitumika na alionesha umahiri langoni,
hivyo kama `Dida` hatocheza, lango la Yanga litakuwa katika mikono
salama.
Nao vinara Azam fc
wameshaingia kambini katika Hosteli zao zilizopo Azam Complex, Chamazi, nje
kidogo ya jiji la Dar es salaam.
Ni mandhari nzuri
kwao na masikani kwao, hivyo bila shaka wapo katika mipango madhubuti kuwaliza
Yanga kwa mara nyingine tena ligi kuu soka Tanzania bara.
Yanga wanahitaji
ushindi kwa nguvu zote ili wapunguze pengo la pointi dhidi ya Azam
fc.
Mpaka sasa Yanga
wapo nafasi ya pili kwa pointi 39 baada ya kucheza mechi 18.
Nyuma yao wapo Mbeya
City wenye pointi 39 sawa na Wanjangwani, lakini utofauti wa mabao ya kufunga na
kufungwa ndio unawafanya wagonga nyundo wa Mbeya kuwa nyuma.
Endapo Yanga
watashinda mchezo wa jumatano, watafikisha pointi 42 nyuma ya Azam fc wenye
pointi 43, hivyo pengo la pointi moja litawapa unafuu mkubwa.
Kama Azam fc
watashinda, basi Yanga watazidi kuisoma namba. Endapo watatoka sare, basi Azam
fc wataendelea kubarizi kileleni kwa raha zao.
Matokeo yoyote
katika mchezo huo, hayatabadili nafasi mbili za juu. Azam fc watabaki wa kwanza
na Yanga watabaki wa pili, huku mechi za wikiendi zikisubiriwa ambapo Mbeya City
watakupambana na JKT Ruvu, uwanja wa Chamazi.
Ugumu wa mchezo wa
keshokutwa unachangiwa na mazingira mengi;
Moja; ubora wa Azam
fc ambao mpaka sasa chini ya kocha wake Joseph Marius Omog hawajafungwa katika
mechi 19 walizocheza.
Kutofungwa kwa mechi
19, kunakupa picha kuwa Azam fc wapo katika mikakati mizito ya kuchukua
ubingwa.
Hawakufanya vizuri
kombe la shirikisho mwaka huu, lakini mechi za mwisho za ligi kuu wamepata
ushindi mkubwa sana katika uwanja wa Chamazi.
Wikiendi iliyopita
waliwafunga Coastal Union 4-0, lakini kabla ya hapo nao Ashanti walikula
4-0.
Pia urejeo wa
nahodha wao na mwenye bahati ya kuwatungua Yanga, John Bocco `Adebayor`
kumewaongezea nguvu zaidi Azam fc katika safu ya ushambuliaji ambayo kwa muda
mrefu imekuwa ikiongozwa na Kipre Herman Tchetche na Mganda Brian
Umony.
Siku za karibuni,
Azam fc walionekana kuwa na tatizo nafasi ya beki wa kushoto kufuatia nyota
wake, Samih Hajji Nuhu na Waziri Salum kuwa majeruhi kwa muda mrefu, lakini
kwasasa pengo hilo linaonekana kuzibwa vyema na beki aliyepandishwa kutoka
kikosi cha pili, Gadiel Michael.
Mechi ya mzunguko wa
kwanza Azam fc iliifunga Yanga SC mabao 3-2 uwanja wa Taifa jijini Dar es
salaam.
Kabla ya mechi hiyo,
timu hizo zilikutana katika mechi ya Ngao ya jamii ambapo Yanga waliilaza Azam
fc bao 1-0.
Timu hizo zimekutana
mara mbili msimu huu na kila moja kushinda na kufungwa, hivyo kwa haraka hakuna
mbabe msimu huu, na Jumatano kila klabu itataka kuonesha kuwa ni bora
zaidi.
Pili; Azam fc
wanataka ubingwa wao wa kwanza msimu huu, huku Yanga wakihitaji pointi muhimu
ili kupunguza pengo. Hivyo kutakuwa na upinzani mkubwa zaidi.
Tatu; ubora wa
vikosi vyote. Yanga wana wachezaji wa gharama kubwa zaidi, lakini hawajafanikiwa
kucheza kwa mafanikio ligi kuu soka Tanzania bara kama Azam fc.
Wao waliwahi
kufungwa, Azam fc hawajafungwa mpaka sasa. Hivyo utagundua kuwa timu hizi ni
bora.
Kufungwa kwa Yanga
hakumaanisha hawana timu bora, bado kikosi chao kinaonekana kuwa na makali.
Mechi itakuwa ngumu zaidi.
Joto la mechi hii
linazidi kupanda na ukipita mitaani unawasikia mashabiki wakizungumzia kipute
hiki.
Nao viongozi
wamesikika wakisema wapo katika mikakati mizito ya kuibuka na
ushindi.
Sina shaka kuwa
mikakati hiyo inalenga kuziandaa timu zao kucheza mpira
uwanjani.
Kama mikakati
inayosemwa ni nje ya uwanja, sasa hapo kunakuwa na shaka juu ya ubora wa mechi
yenyewe.
Makocha wa timu
zote, Joseph Marius Omog wa Azam fc na Hans Van Der Pluijm wa Yanga wanaonekana
kutuliza akili zao kuhakikisha wanawapa raha mashabiki wao.
Pluijm ana kazi
kubwa ya kuhakikisha anapata ushindi ili kuwapa raha mashabiki wa Yanga ambao
walifurika uwanja wa Jamhuri Morogoro, lakini waliambulia kuona timu yao inatoka
suluhu.
Inafurahisha sana
kuona mechi ya Azam fc dhidi ya Yanga inagusa hisia za mashabiki kwa kiasi
kikubwa.
Miaka ya nyuma,
mechi ya watani wa jadi pekee ndio ilionekana kuwa na mvuto kwa
mashabiki.
Kila mtaa ukipita
unasikia wakitambiana mno. Lakini sasa mambo yamebadilika
kabisa.
Mechi ya Azam fc na
Yanga inazungumzwa kila mtaa, pia mechi ya Yanga dhidi ya Mbeya City inaliteka
jiji.
Pia ukija upande wa
pili, Simba vs Azam fc, Simba vs Mbeya City, Simba vs Yanga zimekuwa mechi zenye
mvuto mkubwa zaidi kwa mashabiki.
Hali hii imechangiwa
na ujio wa Mbeya City na Azam fc kuzipatia changamoto Simba na
Yanga.
Kimpira ni hatua
nzuri. Unapokuwa na timu nyingi zenye ushindani na mvuto kwa mashabiki, unapata
ligi bora kabisa.
Angalia mashabiki wa
Mbeya City wanaokuja kuishangilia timu yao inapocheza uwanja wa Taifa, hakika
unagundua kuwa kuna hatua soka la Tanzania linapiga.
Asante sana Azam fc
na Mbeya City kwa kubadilisha utawala wa Simba na Yanga. Sasa wakongwe hawa huwa
hawalali mnapokutana.
Ingekuwa vizuri
zaidi ifike wakati tuwe na timu nyingi zaidi zenye mvuto kama Azam fc na Mbeya
City ili tabia ya kutabiri matokeo na kuamini Simba na Yanga wanashinda ife
kabisa.
Yanga na Azam fc
onesheni ubora uwanjani ili muwape raha mashabiki wenu.
Mpira unachezwa
hadharani, na hauchezwi kwa siri. Tafuteni matokeo ndani ya uwanja na si nje ya
uwanja.
Waamuzi chezesheni
mpira kwa weledi. Sheria 17 zipo wazi, zifuateni bila kuwa na unazi wa
timu.
Mkifanya kazi yenu
kwa ufanisi, mtasababisha mpira bora kuonekana baina ya miamba hii
miwili.
src
shaffihdauda
0 comments:
Post a Comment