KUNA watu wanaamini kuwa Zanzibar ni nchi na wanaamini hivyo kwa sababu Katiba ya Zanzibar inasema hivyo (toleo la 2010).
Hii ni imani ambayo imejengekwa kwa sababu watu hawa wanaamini kuwa Zanzibar kupitia vyombo vyake vya kutunga sheria  ilikuwa na madaraka na uwezo wa kujitangaza kuwa ni nchi na ikawa ni halali.
Naomba kupendekeza kwa wasomaji wangu kuwa mabadiliko ya 2010 yenye kuitangaza Zanzibar kuwa ni nchi kwa maana ya ile iliyokuwepo kabla ya Muungano si tu ni batili bali pia hayana maana zaidi ya kufurahisha hisia tu za Wazanzibari.
Inasikitisha kuona kuwa hawajatokea viongozi katika nchi yetu wenye ujasiri na uthubutu wa kusema ukweli huu kuwa mabadiliko hayo ya Katiba ya Zanzibar ambayo yanapingana na vipengele kadha wa kadha vya Katiba ya Jamhuri ya Muungano hayana maana yoyote, ni potofu na kwa kweli yalifanywa kinyume cha  Muungano na ingewezekana kujenga hoja ya uhaini kabisa kwenye hili.
Zanzibar si nchi kwa mujibu wa Katiba ya  Muungano
 Ni muhimu kukumbuka kuwa kabla ya mabadiliko ya 10 ya Katiba ya Zanzibar (mwaka 2010) kutangaza Zanzibar kuwa ni ‘nchi’, kabla ya hapo Ibara ya 1 ya Katiba ya Zanzibar ilisema hivi (msisitizo wote wangu):
1. Zanzibar is an integral part of the United Republic of Tanzania.
Kwamba “Zanzibar ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania” na kuwa eneo lake inasema:
2.(1) The area of Zanzibar consists of the whole area of the Islands of Unguja and Pemba and all small Islands surrounding them and includes the territorial waters that before the Union formed the then People’s Republic of Zanzibar.
Na Katiba ile ilisema wazi kuwa ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (chini ya Katiba ya Muungano) ambaye ana mamlaka ya kugawa mikoa katika Jamhuri ya Muungano. Inasema hivi:
(2) For the purpose of the efficient discharge of the functions of the Government, the President of the United Republic in consultation with the President, may divide Zanzibar into Regions, Districts and any other areas in accordance with procedures prescribed.
Sasa hadi hapo tunaweza kuona kuwa kuanzia 1984 hadi mwaka 2010 Katiba ya Zanzibar ilikuwa inakubaliana kabisa na Katiba ya Muungano na hakukuwa na tatizo lolote lile la kimgongano baina ya hizo mbili; angalau hakukuwa na tatizo kubwa kama lililopo sasa.
Sasa Katiba ya Muungano kuhusu hayo mambo matatu (nchi, mahali na kuigawa nchi) inasema hivi:
1. Tanzania ni nchi moja na ni Jamhuri ya Muungano.
Kinyume na alivyotangaza Rais Kikwete Bungeni Dodoma miaka michache nyuma kuwa "Zanzibar ni nchi ndani ya Tanzania lakini nje ya Tanzania Tanzania ni moja", msimamo wa Pinda kuwa Zanzibar siyo nchi ni sahihi kikatiba na kiuhalisia.
Katiba ya Muungano (ambayo hadi sasa haijafanyiwa mabadiliko) inaeleza kuwa Tanzania ni nchi moja (si nchi mbili, au tatu).
Msimamo huo wa Katiba ya Muungano ni kinyume na kile kinachosemwa kwenye Katiba ya Zanzibar ibara ya 1 kwamba:
1. Zanzibar ni Nchi ambayo eneo la mipaka yake ni eneo lote la Visiwa vya Unguja na Pemba pamoja na Visiwa vidogo vilivyoizunguka na bahari yake ambayo kabla ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ikiitwa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar.
Sasa mabadiliko ya 2010 ambayo yamebadilisha uwepo wa Jamhuri ya Muungano kama alivyowahi kueleza Tundu Lissu hayana uhalali kwa sababu hayakuwa yameridhiwa Bara kwani yametangaza ‘nchi’ ndani ya nchi.
2.-(1) Eneo la Jamhuri ya Muungano ni eneo lote la Tanzania Bara na eneo lote la Tanzania Zanzibar, na ni pamoja na sehemu yake ya bahari ambayo Tanzania inapakana nayo.
Kimsingi eneo zima la Zanzibar kama ilivyotangazwa na mabadiliko ya 10 ya Katiba ya Zanzibar ni eneo la Tanzania ile ile. Zanzibar haijachukua eneo lolote lile kwani eneo lake lote ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kumbe Tanzania haijaishia Chumbi! Tanzania ni kuanzia Forodhani, Darajani, Michenzani, Miembeni, Milimauni, Mikoroshoni hadi Misufini. Tanzania ni nchi moja basi siyo mbili.
Katiba ya Muungano inasema hivi:
2:2 Kwa ajili ya utekelezaji bora wa shughuli za Serikali ya Jamhuri ya Muungano au Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Rais aweza kuigawa Jamhuri ya Muungano katika mikoa, wilaya na maeneo mengineyo, kwa kufuata utaratibu uliowekwa na sheria au kwa mujibu wa sheria iliyotungwa na
Bunge
Isipokuwa kwamba Rais atashauriana kwanza na Rais wa Zanzibar kabla ya kuigawa Tanzania Zanzibar katika mikoa, wilaya au maeneo mengineyo.
Lakini Katiba ya Zanzibar inasema ni Rais wa Zanzibar ambaye anaweza kuigawa Zanzibar tena bila kushauriana na Rais wa Muungano.
Swali: Je, kesho Dk. Shein akiamua kugawa Mkoa wa Kusini Unguja na kuifanya kuwa mikoa miwili atakuwa sawa sawa?
Mzanzibari atasema “ndiyo”, kwa sababu Katiba ya Zanzibar inampa madaraka hayo lakini Mtanzania atasema “hapana”, kwa sababu madaraka hayo ni sehemu ya Mkuu wa nchi ya Tanzania.
Kitu kingine ambacho mabadiliko ya Zanzibar hayakusema kuhusu hili ni kuwa nani anawalipa wakuu wa mikoa ya Zanzibar?
Kwa ufahamu wangu ni kuwa wakuu wa mikoa ni watumishi wa Jamhuri ya Muungano (chini ya Ibara ya 61 ya Katiba ya Muungano).
Kama wakuu wa mikoa wa Zanzibar wanalipwa na Serikali ya Zanzibar basi ni wazi Rais wa Zanzibar atakuwa na nguvu ya kuongezea mikoa mingi kwa kadiri anavyojisikia!
Anachoweza kufanya Rais wa Zanzibar ni kuwateua wakuu wa mikoa ya Zanzibar baada ya kushauriana na Rais wa Muungano. Hawezi kuigawa Zanzibar kimikoa.
KWA UFUPI
1. Mabadiliko ya Katiba ya Zanzibar yaliyoitangaza Zanzibar kuwa ni nchi hayana maana yoyote na matokeo yoyote kwa sababu hayajabadilisha Katiba ya Muungano ambayo inatambua nchi moja tu.
2. Wabunge wa CCM ambao wanaunda wingi Bunge la Muungano ni dhaifu.
3. Serikali ya Muungano inayoongozwa na Rais Jakaya Kikwete na hasa Mwanasheria wake Mkuu ni dhaifu kwa kuacha uvunjaji mkubwa wa Katiba ya Muungano udumu kwa miaka miwili bila kutaka kuusahihisha huku wakiimba ati wanatawala kwa “kufuata sheria na Katiba.”
Lakini hii ni sehemu tu ya hoja yenyewe kuwa Zanzibar “ni nchi”, ni msimamo  usio na msingi wa Kikatiba kabisa zaidi ya geresha ya kisiasa. Lakini kuna sababu nyingine.
Zanzibar si nchi kwa mujibu wa mkataba wa Muungano.
Watu wote waliochukua muda kujifunza kuhusu Muungano wa Tanzania wanaweza kugundua kirahisi kabisa kuwa msingi wa Muungano huu ni Mkataba wa Muungano ambao ulitiwa sahihi na Julius Nyerere kwa upande wa Tanganyika na Abeid Aman Karume kwa upande wa Zanzibar.
Mkataba huu ndio ulioweka makubaliano ya mambo ya Muungano na mambo ambayo si ya Muungano.
Mwanzo kabisa kabla mkataba haujaorodhesha mambo ya Muungano na masharti mbalimbali ilitangaza kile ambacho ni msingi kabisa wa kuwepo mambo ya Muungano, yaani – kutangaza kuundwa kwa nchi moja. Mkataba huo unasema hivi:
It is therefore AGREED between the Governments of the Republic of Tanganyika and of the Peoples’ Republic of Zanzibar as follows: -
(i) The Republic of Tanganyika and the Peoples’ Republic of Zanzibar shall be united in one Sovereign Republic.
Yaani (Tafsiri ya Kiswahili ya kwangu),
Hivyo basi, imekubaliwa kati ya Serikali za Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar ya kwamba:-
  1. Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Zanzibar zitaungana kuunda Jamhuri moja yenye mamlaka kamili ya kujitawala.
Hivyo, si tu kwamba Katiba ya Jamhuri ya Muungano ambayo inatangaza uwepo wa Jamhuri moja au nchi moja bali mkataba wenyewe wa Muungano unatangaza hivyo tangu mwanzo na ndio msingi wa hiyo Katiba.
Kukubaliana huku kwa Mkataba wa Jamhuri ya Muungano na Katiba ya Jamhuri ya Muungano kunapaswa kuwafunza wote wanaofikiria tu kuwa Katiba ya Zanzibar imevunja Katiba ya Jamhuri ya Muungano. Katiba imefanya zaidi ya hivyo; imevunja Mkataba wa Muungano.
Inasikitisha kuona kuwa hili halijaelezwa vizuri kwa sababu labda watu wanadhania kuwa Katiba ya Muungano iko juu ya Mkataba wa Muungano kitu ambacho si sahihi. Mkataba wa Muungano uko juu ya Katiba zote mbili.
Ni kwa sababu hiyo basi naamini kazi ya kwanza kabisa kwa Bunge Maalumu la Katiba tena kabla ya kufikia sura ile ya Sita ya Muundo wa Muungano ni lazima watangaze kile kilichoko kwenye Mkataba wa Muungano kwamba Tanzania ni nchi moja.
Hawawezi kukubali kilichoko kwenye rasimu ya Katiba kwani nacho kinasababi sintofahamu (ambiguity) isiyo ya lazima.
Hakukuwa na sababu ya msingi kwanini rasimu haikutamka wazi ukweli huu ulioko kwenye Hati ya Muungano na kwenye Katiba hasa ukizingatia kuwa wajumbe wote wa Bunge la Katiba wamekula kiapo cha kuwa watii na waaminifu kwa Jamhuri hii ya Muungano.
Kwa kutangaza kuwa Tanzania ni nchi moja wabunge wa Bunge hili watakuwa wamesahihisha mara moja na daima kosa la Zanzibar kujitangaza nchi na wawakilishi wa Zanzibar ambao wote wako Dodoma watatakiwa wafanyie marekebisho Katiba ya Zanzibar kuakisi ukweli huu.
Hofu kuwa Wazanzibari hawatakuwa tayari kutokuitwa nchi ni hofu inayotokana na woga na hisia za kudeka. Kama kweli Wazanzibari wanataka kuendelea kuwa kwenye Muungano basi  jambo hili haliepukiki.
Kama kwenye hiki kifungu cha kwanza kabisa Wazanzibari watakataa kabisa kisiingizwe kwenye rasimu kuna njia moja tu ya kusuluhisha – kuvunja Bunge la Katiba kwani haliwezi kuendelea na mtindo wa kuendelea kukubali matakwa ya kuiua Tanzania kwa sababu ya kuogopa Wazanzibari “hawatakuwa tayari” umefika wakati ukome.
Kama ni Muungano ni Muungano wa nchi mbili zilizounda nchi moja. Asiyetaka lwake.
Inasikitisha si Warioba wala Kikwete waliokuwa tayari kuusimamia ukweli huu. Kwani bila kuusimamia ukweli huu ni wazi kuwa ukileta Serikali Tatu zitakuwa ni za nchi mbili kinyume na Hati ya Muungano na Katiba ya sasa ya Muungano.
Kama watu wanataka serikali tatu ni lazima wakubali kwanza uwepo wa nchi moja yenye serikali tatu si nchi mbili zenye serikali tatu. Kama watu wanataka serikali tatu kwenye nchi mbili njia ni moja tu – kukutana Umoja wa Mataifa

src
Tanzania Daima

0 comments:

Post a Comment

 
Top