Nguvu ya familia au taifa lolote hutegemea sana vijana wake na kutokana na ukweli huo ni wajibu wa familia pamoja na taifa husika kuhakikisha kwamba wanawapatia mafunzo vijana malezi na ujuzi ili waweze baadaye kutekeleza majukumu na kuendesha maisha kila siku. Katika kutekeleza hili rasilimali za kila aina huweza kutumika ili kuyafikia malengo hayo muhimu.
Lakini kwa bahati mbaya baadhi ya vijana wetu hujisahau kiasi cha kupuuzia kuweka fikra na nguvu zao katika kuyazingatia mafunzo hayo na badala yake kujitumbukiza katika mambo mengine kinyume na mategemeo.
Napenda kuwapa mfano toka kwa mmoja wa vijana wa siku nyingi kwa maana ya miaka ya 47 ambaye kutokana na sababu za wazi kabisa sitaweza kumtaja jina lake.
Yeye alisoma vizuri tena katika miaka ya mapema ya sabini alikuwa ameshahitimu elimu ya chuo kikuu, jambo ambalo utakubaliana nami kwamba kwa miaka hiyo alikuwa amebahatika kweli kweli.
Alipata kazi nzuri na kama ilivyo kwa mzazi makini alinuia vilivyo kuhakikisha kwamba watoto wake watano aliojaliwa kuwapata katika ndoa yake, wanasoma na kufanikiwa katika maisha yao kama alivyo yeye.
Kwa bahati mbaya sana juhudi zote zilikwama kutokana na watoto wake wote, kama vile walipatana kwa pamoja, walishindwa kufikia matarajio ya baba yao.
Watoto hawa ama walifukuzwa katika ngazi za sekondari au kumaliza elimu hiyo wakiwa wamefeli bila hata kupata cheti cha kuhitimu.
Alilazimika kuendelea kuwahudumia bila kujali umri wao huku wenyewe kwa wenyewe wakianza kutoleana macho kwa kuwa walijikuta wakihitaji mambo ya ziada nje ya chakula, malazi na mavazi kwani gharama za kupata mahitaji hayo ya ziada walishindwa kuzipata kwa sababu hawakuwa na vyanzo vyao huru vya mapato.
Mambo yalizidi kuwaharabikia pale ambapo Mzee alipostaafu na kuanza kubaini kwamba nguzo yao waliyokuwa wanajivunia, haikuwa na uwezo tena waliozoea kuuona. Hatua hiyo ilianza kumwakia kila mmoja kiasi cha kuanza kumtafuta mchawi ni nani katika familia yao na kwa mshangao wao walijikuta hakuna wa kuwapatia jibu la uhakika.
Mzee alikuwa na nyumba zake mbili jijini Dar es Salaam, moja alikuwa anaishi yeye mwenyewe na nyingine iliyokuwa na vyumba 10 aliipangisha.
Misukosuko ya maisha ya watoto wake, wa kike wawili na wa kiume watatu ilianza kuwarudi. Wakaanza kupanga mizengwe ya kutaka kuuza nyumba ya baba yao bila kumshirikisha mwenyewe ili wagawane pesa kukidhi mahitaji yao mengi ya kujikimu kisa ni kwamba ‘’tupate chetu mapema,’’ tugawane.
Kama vile walikuwa wameanzisha mkosi, baba yao alipata habari siku chake kabla ya kufanya mauzo hivyo yeye mwenyewe kusimamia zoezi la kuuza nyumba yake kwa kusaidiwa na wakili wake, majirani na marafiki.
Karibu wote ikiwa ni pamoja na majirani, jamaa na marafiki walimpa ushirikiano Mzee mwenzao kutokana na ukweli kwamba wao walikuwa mashuhuda wakati alipokuwa anawahangaikia watoto wake juu ya masuala ya msingi ya elimu na malezi lakini kwa bahati mbaya sikio la kufa halisikii dawa. Watoto waliishiwa nguvu baada ya dhamira yao mbaya kushindwa.
Wakagundua kwamba mzazi wao alijitahidi kila anachoweza kuwapangia maisha mema ya baadaye lakini wakapuuza wakadhani kila siku wataendelea kunyonya toka kwake. Ikabidi sasa wauvae ukweli.
Kwamba hawana namna ila kupambana kivyao na maisha na kwa vile hawakuwa na elimu nzuri basi walilazimika kufanya kazi ya vibarua na ukuli ili mkono uende kinywani na hawakuwa na wa kumlaumu isipokuwa wao wenyewe.
Ndugu zangu, tutumie vyema fursa tulizonazo maishani kabla hazijatuponyoka kama vijana hawa watano ambao sasa walijikuta wakifunzwa na ulimwengu
src
Habari Leo
0 comments:
Post a Comment