Asilimia 80 ya Watanzania wanajishughulisha na kilimo ingawa kuna changamoto nyingi wanazokumbana nazo.
Miongoni mwa changamoto hizo ni mbegu bora, zana za kilimo za kisasa na masoko.
Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika ni moja ya wizara sita zinazotekeleza mfumo wa Matokeo Makubwa Sasa (BRM), lengo likiwa ni kubadili mfumo wa utendaji kazi na kuboresha huduma zinazotolewa na serikali kwa wananchi.
Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika Christopher Chiza, anasema mazao mengi yamekuwa yakiingia sokoni kutokana na mavuno mazuri ya msimu wa kilimo wa mwaka 2012 na 2013.
Anasema kuwa uzalishaji wa mazao ya kilimo katika msimu huo zilizalishwa tani 14,383,845 za chakula, zikiwemo tani 7,613,221 za nafaka na tani 6,770,624 za mazao yasiyo ya chakula.
Chiza anasema mahitaji ya chakula katika mwaka 2012 na 2013 ni tani 12,149,120 hivyo kuwepo kwa ziada ya tani 2,234,726 za chakula, ziada hiyo inajumuisha tani 354,015 za mahindi.
Chiza anasema hadi kufikia Februari 9, mwaka huu, tani 6,736.126 za chakula cha msaada zilichukuliwa na halmashauri 18 kwa ajili ya kusambazwa kwa walengwa katika maeneo yaliyobainika kuwa na upungufu.
Utekelezaji wa BRN
Chiza anasema wizara imeanza kutekeleza mfumo wa matokeo makubwa sasa katika mashamba makubwa ya uwekezaji yapatayo 25 kwa ajili ya kilimo cha mpunga na miwa, skimu za umwagiliaji 78 kwa ajili ya kilimo cha mpunga zinazoendeshwa kitaalamu na maghala 275 ya mahindi kwa kutumia mfumo wa pamoja.
Chiza anasema kuwa viashiria vya mafanikio ni pamoja na kuongezeka kwa uzalishaji wa mpunga kwa zaidi ya mara mbili kutoka tani 4 hadi 8 kwa hekta ifikapo mwaka 2016 katika skimu za umwagiliaji.
Anasema taarifa za awali kutoka mashamba ya mpunga ya Kilombero, Mkindo na Kiroka zinaonyesha kwamba kumekuwa na ongezeko kubwa la mavuno kwa zaidi ya tani 7 kwa hekta kutokana na kutumia mfumo wa kilimo cha mpunga.
Anafafanua katika kuongezeka kwa eneo la uwekezaji kwenye kilimo ni kuzifanya hekta 123,000 zitumike katika kilimo cha mpunga na miwa.
“Kwa sasa kuna hekta zipatazo 85,000 ambazo zitatumika kwa kilimo cha uwekezaji na tayari mashamba mawili yameshapata hati ambayo ni Bagamoyo lenye hekta 22,000 na Mkulazi lenye hekta 63,000.
“Lengo ni kuwa na wakulima 29,000 katika skimu 39 ifikapo mwaka 2016, ambapo kwa sasa skimu 26 zipo katika marekebisho ili ziweze kuendeshwa kitaalamu,” anasema Chiza.
Chiza anasema uhamasishaji wa jamii katika maeneo ya mashamba makubwa matatu ya Bagamoyo, Lukulilo na Ngalimila ambayo ni kati ya mashamba makubwa 7 yaliyopangwa katika awamu ya kwanza umeshaanza.
Anasema shughuli ya kutanbua eneo lililotengwa kwa ajili ya uwekezaji na wanakijiji ni kutoa elimu jinsi wakulima wadogo watakavyoshirikiana na mwekezaji, kuandaa ramani na zoezi la kuandaa hati miliki kwa mashamba ya wakulima wadogo.
Chiza anasema hatimiliki za mashamba kwa ajili ya wakulima wapatao 1,052 zimeanza kuandaliwa na kati ya hizo 185 zimekamilika ili kukabidhiwa kwa wahusika.
“Wizara inalenga kutengeneza hatimiliki kwa wakulima zipatao 52,500 katika skimu za umwagiliaji ifikapo 2016,” anasema Chiza.
Anasema utaratibu wa skimu 26 na uboreshaji wa vikundi vya umwagiliaji umeshaanza na unaendelea.
Anasema mafunzo kwa ajili ya maofisa ugani 98 na wakulima 495 kutoka katika skimu 78 umeshaanza katika kituo cha mafunzo cha Mkindo kilichopo wilayani Mvomero, Morogoro.
Chiza anasema mafunzo hayo yamejikita katika matumizi sahihi ya maji na njia bora za kilimo ikiwemo kilimo shadidi cha mpunga na mbinu za kupata masoko.
Hata hivyo, anasema uzalishaji wa mbegu za msingi za mpunga umeshaanza katika kituo cha utafiti wa Katrin ambapo tayari tani 1.5 ya mbegu hizo zimeshaanzishwa.
Anaongeza kuwa uhakika wa maghala 175 umeshafanywa ambapo maghala 113 yapo katika hali nzuri yakihitaji matengenezo madogo, lakini pia yapo maghala 74 yenye hali ya kati na yanahitaji marekebisho makubwa na mengine 87 yameharibika na hivyo yanahitaji kujengwa upya.
Anasema mfuko wa Bill and Melinda Gates Foundation umeahidi kutoa dola 750,000 kwa ajili ya matengenezo na kufanya ukarabati wa maghala 30 ili yaanze kazi.
src
Tz Daima
0 comments:
Post a Comment