Dar es Salaam. Siasa inabadilika kadri siku zinavyokwenda, hivyo kitendo cha kuungana kwa vyama vikubwa vya siasa  katika taifa lolote Afrika siyo jambo la kushangaza.
Ipo mifano ya vyama katika nchi kadhaa za Afrika vilivyojaribu hatua hiyo na kufanikiwa.
Kwa mara ya kwanza hapa nchini, vyama vya Chadema, NCCR Mageuzi na CUF vimeamua kuunda kambi moja ya kuelekea Ikulu ili kuongeza nguvu na ushawishi, umoja uliochochewa na mwenendo wa CCM wakati wa mchakato wa Katiba. (J M)

Baada ya kukerwa na mwenendo wa mchakato ndani ya Bunge la Katiba, vyama vya upinzani viliunda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kwa lengo la kutetea Rasimu ya Katiba iliyotokana na maoni ya wananchi. Lakini umoja huo sasa umejiegemeza katika  mkakati wa kuimarisha upinzani na kuiondoa madarakani CCM.
Msukumo wa kuunda umoja huo ulitokana na CCM kudaiwa kuhodhi mchakato huo kwa lengo kupenyeza ajenda zake, ikiwamo kulazimisha ajenda ya ya muundo wa serikali mbili kwenye Rasimu ya Katiba, ajenda ambayo haimo kwenye mapendekezo hayo.
Fukuto lao kwa sasa linaendelea nje ya Bunge kupitia ziara za Ukawa kwenye mikoa 17 huku CCM nayo ikifanya mikutano yake kwenye mikoa mbalimbali kudhibiti kukua kwa Ukawa.
Mmoja kati ya viongozi wa Ukawa ambaye ni mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba anasema  matumaini ya mpango wao kufanikiwa ni makubwa kutokana na maandalizi yao.
Anasema baada ya kumalizika kwa vikao vya Bunge Maalumu la Katiba, umoja huo uliunda kamati yenye wajumbe watatu kutoka kila chama kwa ajili ya kufanya kazi ya kuandaa tathmini, mipango na mikakati ya kutengeneza uwezekano wa kufanikiwa harakati hizo.
“Tulichokubaliana kwa sasa ni kukamilisha kwanza chaguzi za ndani kwa kila chama halafu ndiyo tuingie kwenye hatua hiyo baada ya kupata taarifa ya kamati hiyo,” anasema.
“Baadhi ya wajumbe wake ni pamoja na makatibu wakuu wa Chadema ambaye ni Dk Wilbroad Slaa, Julius Mtatiro (CUF) na Mosena Nyambabe (NCCR-Mageuzi). Matumaini ni makubwa kwani hata Watanzania wamepokea uamuzi huo kwa furaha na uzalendo mkubwa.”
Uchambuzi wa wadau
Hata hivyo, ajenda hiyo imejengewa hofu ya kukwama kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo mtandao wa CCM uliotapakaa nchi nzima, elimu ndogo ya kupiga kura ya wananchi, mchakato wa Katiba mpya na nyingine kadhaa.
MWANANCHI

0 comments:

Post a Comment

 
Top