
Freddy Macha
Miaka ya karibuni wananchi wengi hasa vijana, wamejiingiza kwenye uhusiano wa kimapenzi na wageni hasa wazungu. Mapenzi hayakuanza leo, jana wala juzi.
Yamekuwapo wakati wote. Ukweli ni kwamba kuna baadhi ya watu katika mataifa mengi duniani, hutaka kuwa na uhusiano na wageni. Mosi, kutaka kuondokana na udhia wa wananchi wenzao; pili, kutafuta maisha bora; tatu, mapenzi na ndoa na nne, udadisi (kipya kinyemi).
Miaka arobaini au hamsini iliyopita, nakumbuka waliopenda uhusiano na wageni, walikuwa zaidi wanaume. Wanawake waliojamiiana na wageni waliitwa malaya na wachache ni wale tu waliofanya kazi kwenye hoteli kubwa za kitalii kutafuta ajira. Mathalan, nakumbuka miaka ya 1960/1970, Tanzania ilijazana wakimbizi. Sera ya TANU na siasa ya Azimio la Arusha ilisaidia walioathirika na udhalimu wa kikoloni, ubaguzi na kadhalika kutoka Kongo, Afrika Kusini, Palestina, Malawi, Marekani, Uganda na kwingineko.
Wengi wa wakimbizi wa Kongo (iliyoitwa Zaire enzi za utawala wa Joseph Mobutu) walikuwa wanaume, hasa wanamuziki, waliohusudiwa sana na wanawake wetu. Mzaire aliongea Kiswahili chenye lafudhi ya Kifaransa na Kilingala kilichomfanya avutie kwa tofauti yake na mwanaume wa Kitanzania. Au wakimbizi wa Afrika Kusini, Namibia na Zimbabwe, tuliwaita Waafrika Kusini, ‘Wasoweto’ kutokana na harakati au machafuko ya Kitongoji cha Soweto mjini Johannesburg mwaka 1976.
Wasoweto walikuwa tofauti. Walivalia suruali pana pana. Waliongea Kiingereza fasaha. Vijana wa kiume na kike tuliona ni heri kubwa kwenda na Wasoweto kuliko wazalendo wenzetu. Miye kwa mfano; nilikuwa na swahiba aliyependa fasihi, mashairi na kupiga muziki.
Awali, nilipata shida sana na miaka yangu ishirini na moja au miwili, kupata sahiba wa kike aliyependa fasihi na muziki. Wasichana wa rika langu, walitaka kwenda baa, kunywa bia na vile ka- mshahara kangu ka uanahabari magazeti ya Chama (Uhuru na Mzalendo) kalivyokuwa nyau, haikuwa rahisi kubembelezana na dada zangu, hata wawe wazuri namna gani. Aghalabu, kadri uzuri ulivyozidi ndivyo karaha ilivyoongezeka.
Wasoweto hawakujali. Azma yao ilidai uhuru; walipenda utamaduni wa michezo na kusoma vitabu. Mkikosa fedha ya basi au teksi mnatembea tu kwa miguu mkiongelea haiba ya mawingu, maua waridi, misufi, twiga, muziki wa jazz, taarabu, hadithi za Alinacha na siasa za Wapalestina. Mkifika hivyo hivyo ugali kwa maharage na ndizi kisukari. Mnasoma mashairi ya Shaaban Robert na Christopher Okigbo (Mshairi wa Nigeria aliyefariki angali kijana mwaka 1967), baadaye usingizi wa mapenzi ya joto la Dar es Salaam. Au mnakwenda tu ufukwe wa bahari kufurahia mandhari. Hayo ndiyo mapenzi ya kweli. Siyo mapenzi ya kutegemea mfuko kwanza. Fedha na baa hufuata baadaye. Kinachotangulia mapenzi asilia.
Kwa kina dada, mambo pia hayakuwa rahisi. Kijana wa kikwetu akishakutoa dada, akikununulia zito, jepesi na la wastani, ukishafurahi unakuwa sasa mtwana wake. Kuna siku utapigwa. Utasutwa. Iko miezi utawekwa hata mimba na jamaa hatoonekana kumtunza mtoto. Baadaye utagundua ala kumbe! Kapata mwingine.
Uafadhali ulionekana kwa Wamarekani weusi. Warefu, wazungu weusi, wenye tabia tofauti na zetu. Waliongea kile Kiingereza cha “bradha- man” na “sista-du” kiliichoonekana kitamu. Wakimbizi na watembezi wa Kimarekani walikuwa kwa wingi Tanzania kipindi hicho. Walizikimbia tafrani za Marekani: ubaguzi wa rangi, harakati za chama cha Black Panther kilichochukua bunduki kupigana na nguruwe weupe. Hadi leo haujaisha. Enzi hizo mwanamke wa Kitanzania akimwona ‘Mniga’ (kama tulivyowaita mitaani) ni kama kumshuhudia mdogo wake Mungu. Astakafurlah! Macho huwatoka kinadada; ndimi nje. Walijua kuongea na mwanamke, walifuzu mapenzi. Ni kama Wanigeria wanavyohusudiwa na wanawake wetu leo. Kipya kinyemi. Baadaye iligundulika hawakuwa tofauti na wanaume wazalendo.
Miaka imevuta miguu; leo wanawake weusi hawataki wanaume weusi kwa jumla. Mwanaume mweusi hakosi nyumba ndogo au tatu. Mwanamke mweusi kishamfahamu kaka yake. Kishamjua. Akishamkubalia, huba au mahaba, hatokuwa yeye tu. Hilo limeenea majuu yote. Limeenea kiasi ambacho dada weusi hawana imani na kaka zao. Wameanza kusaka wazungu. Zamani mzungu hakupendwa sana na mwanamke mweusi. Wapo dada wachache waliokwenda na wazungu ndiyo; ila wengi walidai ah mzungu hana nguvu kitandani. Au walilalamika wajihi wa ngozi haukuwavutia.
NGOZI IKOJE SIJUI...
Leo mengine. Kinachotafutwa ni mapenzi na uhusiano siyo kitanda au fedha tu..
Hivyo basi, mapenzi yanayodumu, yanayowezekana ni baina ya mwanamke mweusi na mzungu. Sikiliza...
Wakati harakati za ukombozi wa wanawake wa kizungu zilizofoka moshi miaka ya 1960, wanawake waligeuza uhusiano. Miaka ya 1970, uzunguni kote ulikuwa wakati wa wanawake kudai usawa kazini, kuwataka wanaume waache udhalimu. Leo wanawake wa kizungu ndiyo watawala wa nyumba, hata sehemu za kazi za kijamii. Wanawake wa kizungu wanatawala mazingira kiasi ambacho kura za kisiasa zinawaegemea. Hapa Uingereza kuna mfano mzuri, kisiasa.
Mwezi uliopita David Cameroon, Waziri Mkuu (na kiongozi wa chama cha Conservative) alibatilisha baraza lake la Mawaziri. Badala yake alichagua wanawake zaidi. Inadaiwa kafanya hivyo kutafuta kura za wanawake uchaguzi ujao wa 2015.
Mbinu hizi zilitekelezwa pia na Waziri Mkuu wa zamani, Chama cha Leba, Tony Blair, alipoingia madarakani, 1997. Alifanya historia kwa kuwa na wabunge 101 wa kike , baadhi walishika vyeo vya uwaziri! Waliitwa “Blair’s Babes.”
Hadi leo wengi bado wamo serikalini. Huo ni mfano mdogo unaodhihirisha namna uhusiano ulivyobadilika kuanzia mapambano ya haki za wanawake yalipochachamaa Ulaya miaka hamsini iliyopita.
Wanawake wanatawala na ni wakali. Baadhi ya wanaume wa kizungu huona afadhali kuwa na wanawake wa mataifa mengine ya Asia na Afrika.
Hawa nao huwa wamechoshwa na wanaume wasioaminika. Hapa basi watu wawili hawa walioshakereka, hukutana. Ndiyo maana leo uhusiano baina ya wanawake weusi na wanaume wa kizungu yanastawi sana.
Tanzania je? Wengi wanaandika kuulizia uhusiano na wazungu. Ugumu wa maisha unajenga ari za kumpata mgeni kujiendeleza. Je, kuna wepesi na uzito gani? Tuendelee na mazungumzo juma lijalo.
0 comments:
Post a Comment